Habari Mpya

Habari Zote

Showing posts with label MICHEZO. Show all posts

SIKU chache baada ya kutoa notisi ya kuachia ngazi ndani ya Simba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez ameanza kuwaaga baadhi ya wafanyakazi aliofanya nao kazi klabuni hapo.


 Barbara ameweka bayana kufikia Januari ataachia ngazi kwenye nafasi hiyo kwa sababu alizozianisha, lakini kabla hajatimiza lengo hilo juzi alifanya hafla fupi na wafanyakazi wote waliokuwa chini yake na kuwaaga rasmi na mwenyewe amefichua sababu ya kufanya hivyo. 

 Barbara alisema kulingana na majukumu yake mbalimbali anayoyafanya wakati huu huenda asipate nafasi nyingine ya kukutana na wafanyakazi wengine wote kwa pamoja na kuwaaga kama anavyotaka. 

Alisema Simba inakwenda kucheza mechi tatu Kanda ya Ziwa na watu wa idara ya habari wasiopungua watatu watakuwa huko, huku Simba Queens ikiwa na mechi za ugenini na kuna watu watatoka ofisini kwa ajili ya kusimamia hilo.

 “Baada ya hapo kuna shughuli mbalimbali za uchaguzi zinaendelea wakati huu. Kuna wafanyakazi watakuwa bize kusimamia suala hilo kuhakikisha linakamilika kwa ukamilifu ili kupata viongozi bora kama vile ambavyo Simba tunahitaji wapatikane,” alisema Barbara na kuongeza bado ataendelea kuipigania Simba na kufanya kazi za timu hata baada ya notisi yake ya mwezi mmoja kuisha.

 “Hivyo jana (juzi) niliona ni siku sahihi kuagana na wafanyakazi wenzangu halikuwa tukio rahisi, kwani ni watu wazuri niliofanya nao kazi kwa pamoja hadi kufikia mafanikio mbalimbali. “Kuna majukumu naendelea nayo huenda yakawa yanachukua muda na ikashindikana kupata nafasi ya kwenda ofisini mara kwa mara kama hapo awali.”

 Katika hatua nyingine Barbara aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii akisema:“Moja ya sehemu ngumu kuondoka Simba ni kuwaaga watu wazuri kwenye sehemu ya uongozi. Popote ninapoenda, chochote kitakachofuata, wafahamu kuwa Barbara Gonzalez atapatikana kwa simu moja.” 

Barbara aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu Septemba 2020 kuchukua nafasi iliyoachwa na Senzo Masingiza aliyeacha kazi ghafla kabla ya kuibukia Yanga na kufanya kazi hadi mapema mwaka huu alipotangaza kuondoka na kumpisha Mzambia Andreew Mtine. 

CHANZO MWANASPOTI

Barbara wa Simba Sc kuaga

TIMU ya Dodoma FC ya mkoani hapa, wamejinasibu kuwa hakuna kitu kitakachoweza kuwazuia kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Dodoma FC imefikia hatua ya kusema hivyo kama kujibu malalamiko ya wadau wa soka mkoani hapa walioingiwa na mashaka kuhusu kupanda VPL msimu ujao kwa timu yao kufuatia kufanya vibaya katika mechi zake mbili za mwisho kabla ya mapumziko ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili.

Dodoma FC ilijikita kileleni mwa kundi C' kwa kipindi chote cha mechi za Ligi Daraja la Kwanza, kufuatia matokeo mazuri waliyokuwa wanayopata, lakini mzunguko wa pili umewaanzia vibaya mara baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo ikiwemo ya hivi karibuni dhidi ya pamba huko Mwanza.

Katibu mkuu wa Dodoma FC Fourtnatus Johnson alisema kuwa nafasi yao ni namba moja hivyo mapema mechi ya Desemba 16 mara baada ya dirisha dogo la usajili kufungwa lazima warudi katika nafasi yao kwa kuvuna pointi tatu.

"ligi daraja la kwanza ni ngumu asikuambie mtu, lakini Tunashukuru Mungu hatuko katika nafasi mbaya, hivyo niwaambie wadau wetu wa Dodoma wasiwe na wasiwasi kwani mwakani lazima tucheze ligi kuu hivyo matokeo yasiwatishe"

Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri ripoti ya kocha wao Jamhuri Kiwelu "Julio" juu ya wachezaji watakaofanikiwa kubaki na wanaondoka ili kujua nafasi za kufanya usajili ili kukazia kikosi chao katika makali ya kuhakikisha wanatimiza ndoto za wana Dodoma kushuhudia Ligi Kuu


"Niwaombe Shirikisho la Soka nchini waache timu zicheze mpira na matokeo yaamue siyo kuangalia kanda wanazotoka iwe kigezo cha kupigania timu husika zipate hata kama kiwango chao cha kucheza ni mbovu."

Dodoma FC kutinga Ligi Kuu

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -