- Home >
- Azam FC Yamshikia Simba:
Saturday, 30 May 2026
Mazungumzo na Himid Mao Yaanza, Yataka Pesa Ndefu"
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Azam FC wameanza rasmi mazungumzo na kiungo wao mkabaji Himid Mao kwa lengo la kumpa mkataba mpya kabla ya msimu wa 2026/2027. Hatua hiyo inakuja huku tetesi zikidai kuwa wapinzani wao Simba SC wanyatia huduma ya nyota huyo aliyerejea klabuni hapo msimu uliopita.
Chanzo cha ndani klabuni hapo kimeiambia Lenzi Media kuwa ingawa Azam wapo mbele ya Simba katika kumsajili Mao, kiungo huyo anataka ongezeko kubwa la mshahara ikilinganishwa na mkataba wa mwaka 1 aliosaini aliporejea. “Tayari mazungumzo mapya yameanza, lakini si rahisi kwani anahitaji pesa ndefu. Viongozi wanaendelea kuzungumza naye,” kilisema chanzo hicho.
Mao alicheza Azam FC kuanzia 2008 hadi 2018 kabla ya kuelekea Misri kuichezea Petrojet, ENPPI, Ghazl El Mahalla na Tala’ea El-Gaish SC hadi 2025.
Akizungumzia usajili huo, staa wa zamani wa Azam Erasto Nyoni anayeichezea Kagera Sugar amesema: “Kiwango cha mchezaji ndiyo thamani ya pesa yake. Mao amewaonyesha Azam kwa vitendo kuwa bado ana kiwango cha juu.”
Chanzo: Azam FC
NA: PETER MWAMKMBA