SIKU mbili zikiwa zimepita tangu Dk Louis Shika kuelezea siku 28 za mateso aliyoyapata nchini Urusi, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini hu...
SIKU
mbili zikiwa zimepita tangu Dk Louis Shika kuelezea siku 28 za mateso
aliyoyapata nchini Urusi, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo wakati huo,
Patrick Chokala amefichua siri jinsi walivyomsafirisha kijasusi ‘bilionea huyo
wa nyumba za Lugumi’ kurudi Tanzania.
Balozi
Chokala aliyekuwa Urusi kati ya mwaka 2002 na 2008 katika kipindi ambacho
sakata la utekwaji wa Dk. Shika lilijitokeza, amethibitisha kuwa ni kweli
Mtanzania huyo ni daktari na kwamba ni kweli amewahi kutekwa.
Dk.
Shika anatuhumiwa kuvuruga mnada wa majumba ya mfanyabiashara maarufu, Said
Lugumi uliofanywa na kampuni ya Yono baada ya kufika bei ya kuzinunua nyumba
hizo tatu kwa Sh3.2 bilioni, lakini akashindwa kutimiza sharti la kulipa
asilimia 25 ya fedha hizo.
Baada
ya kushindwa kulipa kulisababisha awekwe rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi
Dar es Salaam kwa siku sita hadi alipoachiwa kwa kujidhamini mwenywe Novemba 14
na kutakiwa kuripoti kila siku.
Mara
baada ya kutoka polisi kwa dhamana, Dk Shika ambaye anaishi nyumbani kwake
Tabata Mawenzi alieleza mambo mbalimbali ikiwamo kutekwa na kuteswa akiwa Urusi
Juni 2004, ikiwa ni pamoja na kukatwa vidole viwili mkono wa kushoto na kimoja
mkono wa kulia.
Pia
alieleza jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka watekaji hao.
Katika
mahojiano na gazeti hilo Balozi Chokala alisema analikumbuka vizuri tukio la
kutekwa kwa Dk. Shika na jinsi ubalozi ulivyomsaidia asipatwe na kadhia kubwa
zaidi. “Ni kweli huyo jamaa ni daktari wa binadamu. Alisoma Chuo Kikuu cha
Lumumba kilichopo Moscow, Urusi,” alisema Balozi Chokala.
Alisema
kutokana na upekee wa yaliyomsibu Dk. Shika, ubalozi ulilazimika kuingilia kati
ili kunusuru maisha yake.
Alisema
Dk. Shika alitekwa na majambazi waliokuwa wanataka fedha ambazo yeye mwenyewe
(Dk. Shika) alikuwa anajigamba kuwa nazo na kuwashawishi watekaji hao
kumfuatilia. “Majigambo ya kumiliki fedha nyingi hajayaanza leo.
Tangu akiwa
Urusi alikuwa anasema anamiliki fedha nyingi. Watu walimuamini kwa sababu
alikuwa daktari anayetambulika, matokeo yake alitekwa,” alisema Chokala, ambaye
amewahi kuwa mwandishi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Balozi
huyo alisema baada ya kufanikiwa kuwatoroka majambazi hao ambao baadaye
walikamatwa na polisi nchini humo kisha kufunguliwa mashtaka, Dk. Shika
alipelekwa hospitali kwa matibabu akiwa amepoteza vidole kadhaa vya mikono yote
miwili.
Alisema
majambazi hao walimtesa kwa muda mrefu kwa kuwa mpaka anapatikana vidole hivyo
vilikuwa vimeanza kuoza.
“Walimshikilia
kwa muda mrefu kwa kuwa walihitaji fedha ambazo Dk. Shika hakuwa nazo,”
anakumbuka balozi huyo aliyestaafu mara baada ya kurudi nchini.
Alisema
baada ya ubalozi kupewa taarifa zake, ulifuatilia na kugundua kwamba alipelekwa
nchini humo na Wizara ya Afya, na alikuwa amelipiwa kila kitu ikiwa ni pamoja
na tiketi ya ndege.
Wakati
anatekwa, alisema Dk. Shika alikuwa ameshahitimu lakini hakuwa na nauli ya
kurudi nyumbani, hivyo akawa anahangaika kupata nafasi ya kuendelea na shahada
ya uzamili. “Tulipowasiliana na wizara walithibitisha kuwa ni mtu wao.
Tuliandaa utaratibu wa kumrudisha bila yeye kujua kwa sababu hakuwa anataka
kufanya hivyo,” alisema.
Akiwa
anaendelea kuhudumiwa, ubalozi ulimuandalia safari ya kurudi bila yeye kufahamu
kuepuka asitoroke. Balozi Chokala alisema ilikuwa ni lazima Dk. Shika arudishwe
kuepusha janga jingine linaloweza kumkuta endapo angeendelea kuishi nchini
humo. “Kujirudia kwa tatizo kama hilo kungeupa ubalozi lawama. Hatukutaka
kujiweka kwenye nafasi hiyo,” alisema.
Baada
ya mipango yote kukamilika, askari wa ubalozini walimpeleka uwanja wa ndege na
kumkabidhi kwa wahudumu wa ndege iliyokuwa inakuja Tanzania wakiwaelekeza
wasimshushe popote isipokuwa Dar es Salaam ambako Wizara ya Afya ilikuwa
inamsubiri.
Mpango
huo ulitekelezwa kama ulivyopangwa na wizara ikathibitisha kumpokea mtumishi
wake huyo ambaye balozi Chokala anasema alipewa nyumba na akawa anaendelea na
majukumu yake. “Akiwa Urusi, nilielezwa kuwa alikuwa ana matatizo ya kijamii
ambayo yaliendelea kumuandama hata aliporudi. Nasikia kuna wakati alienda kwao
na hakurudi tena kazini,” alisema.
Kuhusu
Dk. Shika kuwa ni Rais wa kampuni ya Lancefort aliyoianzisha akiwa Urusi ambayo
Serikali ya nchi hiyo ilitilia shaka mwenendo wake, hivyo kuifuatilia, Balozi
Chokala alisema hafahamu chochote.
COMMENTS