MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na usalama wa ab...
MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na
usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.
Maafisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli
hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo
mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa husika.
Mkuu wa msafara wa maafisa hao, ambaye ni Mkuu wa
Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Shaaban Kombo alisema JNIA inaulinzi
madhubuti kwa abiria na mizigo hukaguliwa kwa kutumia mitambo maalum kabla ya
kupanda ndege au kuingia ndani ya jengo kwa kazi mbalimbali, ambapo wameahidi
kufuata nyayo hizo ili kuzuia uhalifu unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.
Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi
ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia
katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa
vitambulisho unavyofanyika, ukiwa ni tofauti na AAKIA ambao hutoa vitambulisho
vya kudumu mara baada ya taratibu kukakamilika, wakati JNIA hutoa vitambulisho
vya muda kwa muombaji ili aweze kuendelea na kazi, wakati akisubiri cha kudumu kikamilike
kutengenezwa.
“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu
hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja
anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la
kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda
kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika
matengenezo,” alisema Kombo.
Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha
JNIA, Lugano Mwansasu alisema ziara ya maafisa wa AAKIA imewafariji na kuanza
ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na
maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.
Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), kuiga mfano huu wa kupeleka maafisa wake kwenye viwanja
mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la
kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo
chini ya serikali.
“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi
tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu
tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa
ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Lugano.
Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na
mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.
Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika
kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na
masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.
COMMENTS