NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kw...
NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii katika miradi yote inayopewa na Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Akikagua hatua zilizofikiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota, Kwandikwa, amesema Serikali itaendelea kuainisha miradi mingine ili kuhakikisha fedha za Serikali zinaokolewa na kusimamiwa kwa uzalendo.
“Hakikisheni mnafanya kazi zenu kwa weledi, uzalendo na kukamilisha miradi kwa wakati na kuokoa fedha ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mingine hapa nchini”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Muonekano wa mtambo wa kuchakata zege unaotumiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam. |
Ametoa wito kwa wataalamu wengine kuja kupata mafunzo kwa TBA ambao ni chachu ya utekelezaji wa miradi mingi hapa nchini kwa kuwa wanatumia mfumo wa kisayansi na mitambo yenye kusaidia kupunguza gharama za ujenzi.
Pia, Naibu Waziri huyo ameushukuru uongozi wa TBA kwa kutoa ajira za vibarua takribani 200 kwa siku katika mradi huo na kuwataka wafanyakazi hao kuwa waadilifu na waaminifu ili kuwa na sifa za kupata ajira za kudumu.
Muonekano wa baadhi ya vitalu vya makazi eneo la Magomeni Kota zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 35.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kukamilika mradi huo kwa wakati, ubora na kwa gharama nafuu.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kukamilika mradi huo kwa wakati, ubora na kwa gharama nafuu.
Amefafanua kuwa mradi huo utakuwa una jumla ya vitalu vitano ambapo vitalu vinne vina majengo ya ghorofa nane na kitalu kimoja kina jengo la ghorofa tisa na hivyo mradi utatoa makazi kwa kaya 656.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi mwakani na utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 zote ikiwa ni fedha za Serikali.
COMMENTS