Habari Mpya

Tuesday, 28 November 2017

SHIRIKA la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limesema liko tayari kushirikiana na Serikali kujenga miundombinu ya kisasa ya usafiri, Nishati ya umeme, maji na usafi wa mazingira katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango(kushoto) akisalimiana na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan(JICA), Hiroshi Kato walipokutana kwa mazungumzo katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Hiroshi Kato wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Jijini Dar es Salaam.

Kato alisema kuwa mradi mwingine wanaotaka kuutekeleza katika mji wa Dodoma ni udhibiti wa taka ngumu na kwamba wanachosubiri ni Serikali kuainisha maeneo ya vipaumbele vilivyoko katika mpango mji wa Dodoma.

Aidha Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa Shirika lake litaendelea kusaidia eneo la kilimo hususan kilimo cha mpunga ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwakomboa wakulima.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amelishukuru Shirika hilo kwa kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa mji wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya nchi.

Alisema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuupanga mji wa Dodoma mapema ili kuondoa changamoto za msongamano wa huduma za jamii kwenye eneo moja kama ilivyo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) akisalimiana na Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan –JICA nchini Tanzania Toshio Nagase, alioambatana na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Hiroshi Kato (katikati) walipowasili katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.


“Pamoja na umuhimu wa miundombinu ya maji, umeme, usafiri wa mjini, lakini pia tunataka tujenge mapema njia za juu (ring roads) ili kudhibiti msongamano wa magari” alisema Dk. Mpango.



Wajumbe walioambatana na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi Kato wakifuatiia kwa makini majadiliano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) na mgeni wake ambaye ni Makamu wa Rais wa JICA Hiroshi Kato, Jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa mradi mwingine wa kipaumbele katika mji huo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa katika eneo la Msalato, karibu kilometa 20 kutoka katikati ya mji huo ili kurahisisha usafiri kwa njia ya anga.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazopata ufadhili mkubwa wa miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka Japan kupitia Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo (JICA).

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Isdor Mpango(kushoto) akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) Hiroshi Kato (hayupo pichani) katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa barabara ya juu (fly over) katika eneo la Tazara Jijini Dar es Salaam, upanuzi wa awamu ya kwanza ya barabara mpya ya Bagamoyo (Mwenge-Tegeta) na ufadhili mpya wa awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Morocco hadi Mwenge.
Kamishina Msaidizi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Shogholo Msangi akielezea kuhusu masuala ya kodi katika maendeleo ya Taifa katika mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dk. Philip Mpango na  Makamu wa Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi Kato (hawapo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa pia na Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) nchini Tanzania Toshio Nagase, pamoja na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -