HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA TISA WA BU...
HOTUBA YA MHESHIMIWA
KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA
KUAHIRISHA MKUTANO WA TISA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
TAREHE 17 NOVEMBA,
2017
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, tarehe 7 Novemba, 2017 tulianza kikao cha kwanza cha mkutano wa tisa wa
Bunge lako tukufu na leo tunafikia tamati. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha kwa amani na afya njema shughuli zote
zilizopangwa.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kukupongeza kwa hekima, busara na uwezo
mkubwa wa kuliongoza Bunge hili ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na
Wenyeviti wa Bunge. Vilevile, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri,
michango, maoni na ushauri tulioupokea katika mkutano huu.
3.
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na kikao hiki cha Bunge, wapo baadhi ya Waheshimiwa
Wabunge na wananchi tunaowawakilisha katika majimbo yetu walipata misiba ya
ndugu, jamaa na marafiki.
4.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge lako
likiendelea, tarehe 9 Novemba, 2017 tulipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za
vifo vya wanafunzi watano wa shule ya msingi Kihinga wilaya ya Ngara mkoani
Kagera waliopoteza maisha kwa kulipukiwa na bomu wakiwa darasani. Katika tukio
hilo, wanafunzi 43 na mwalimu mmoja walijeruhiwa.
Aidha, tarehe 14
Novemba, 2017, Serikali ilipokea taarifa ya kaya 53 zenye wakazi 320 kutoka
kijiji cha Kabegi, wilaya ya Musoma, mkoani Mara, walioathiriwa na maafa ya
mvua na upepo mkali. Watu wanne walijeruhiwa na kupatiwa matibabu. Wakazi wote
wamepata hifadhi kwa ndugu, na wamepata misaada ya kibinadamu ili waweze
kujikimu kwa muda.
5.
Mheshimiwa Spika, vilevile,
tumepoteza maisha ya watu 11 katika
ajali ya ndege iliyotokea tarehe 15 Novemba, 2017 ambao walikuwa wakisafiri
ndani ya ndege aina ya Cessna Grand Caravan wakitoka kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda kwenye uwanja wa ndege wa Seronera uliopo
kwenye Hifadhi ya Serengeti, mkoani Mara.
6.
Mheshimiwa Spika, matukio mengine
yaliyowaathiri ndugu zetu ni mafuriko yaliyotokea Zanzibar ambapo watu wawili
walipoteza maisha kwa kuangukiwa na ukuta katika eneo la Bububu, Magengeni. Aidha, wanafunzi watatu wa sekondari ya Ndyuda
iliyopo katika mji mdogo wa Mlowo, mkoani Songwe walifariki dunia kwa kupigwa
na radi katika kipindi cha hivi karibuni. Nitumie nafasi hii kuwapa pole, wale
wote waliofikwa na misiba pamoja na maafa hayo.
Vilevile,
sote tunatambua kuwa walimu wote nchini ni zaidi ya asilimia 65 ya watumishi wa
umma nchini. Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anawapa pole walimu
wote kwa kufiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Yahaya
Msulwa ambaye amefariki
dunia jana katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam alikokuwa
akipatiwa matibabu. Tunatoa pole kwa mke wa marehemu pamoja na watoto.
PONGEZI
7.
Mheshimiwa Spika, tarehe 7 Oktoba, 2017 vilevile, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko katika
Baraza la Mawaziri pamoja na kumteua Bw. Stephen N. Kagaigai kuwa Katibu wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
8.
Mheshimiwa Spika, tarehe 27 Oktoba, 2017 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wapya, Naibu
Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa pamoja na Mabalozi.
9.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu, Bunge lako tukufu lilimuapisha Mheshimiwa Janeth
Maurice Masaburi aliyeteuliwa tarehe 21 Oktoba, 2017 kuwa Mbunge na Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
10.
Nitumie fursa hii
kuwapongeza Waheshimiwa wote kwa kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali.
Ninawatakia heri katika kutimiza majukumu yao mapya.
MASWALI,
MISWADA NA KAULI ZA SERIKALI
11.
Mheshimiwa Spika, katika mkutano huu,
Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa
Waziri Mkuu, maswali ya kawaida ya msingi yapatayo 142 na maswali ya nyongeza 358 na
kujibiwa na Serikali. Vilevile,
Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili miswada minne na kupokea kauli mbili za Serikali.
12.
Mheshimiwa Spika, Miswada ya Sheria
iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu ni:
(i)
Muswada
wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017 (The Tanzania Telecomunications Corporation Bill, 2017);
(ii)
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2017 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments
- No.4), Bill, 2017);
(iii)
Muswada wa Sheria ya
Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017. (The
Tanzania Shipping Agencies Bill, 2017).
(iv)
Muswada wa Marekebisho
ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017. (The Drugs Control and Enforcement
(Amendments) Bill, 2017).
13.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi za
msingi zilizopangwa, katika mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kupata
Kauli za Mawaziri ikiwemo kauli ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
kuhusu udahili na utoaji wa Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka
2017/2018 na kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
kuhusu fursa kwa wasichana kujipima uwezo katika riadha ili waweze kuiwakilisha
nchi yetu katika mashindano yajayo ya kimataifa ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki, “All
– Africa Games” na mengineyo.
MPANGO WA MAENDELEO
NA MWONGOZO WA MPANGO NA BAJETI
14.
Mheshimiwa
Spika, katika kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 94(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu,
mnamo tarehe 7 Novemba 2017, Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa
Maendeleo unaokusudiwa kutekelezwa kwa mwaka 2018/19. Hoja hiyo ilijadiliwa kwa
siku tano na kuhitimishwa tarehe 13 Novemba 2017.
15.
Mheshimiwa
Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango,
Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb.) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa
Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa
wakati wa kuhitimisha hoja hiyo. Vilevile, nawashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa
Wizara za Kisekta kwa mchango mzuri waliotoa wakati wa mjadala wa hoja hiyo
unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika mwaka 2018/2019. Naamini
mtakubaliana nami kwamba katika mjadala huo, tulipata darasa zuri ambalo
limetupa uelewa mpana wa upangaji wa Mipango na Bajeti katika nchi yetu.
16.
Mheshimiwa
Spika, Mpango wa mwaka 2018/19 utakuwa wa tatu katika mpangilio wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa
miaka mitano, ulioanza 2016/17 - 2020/21. Mpango huo utaendelea kutekeleza
maeneo manne ya kipaumbele ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, yaani: (i)
Viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda; (ii)
Kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu; (iii) Ujenzi wa mazingira
wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na (iv) Kuimarisha usimamizi wa
utekelezaji wa Mpango.
17.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na mapendekezo ya mpango huo, uliwasilishwa pia Mwongozo
wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2018/2019. Mambo muhimu yaliyoainishwa katika Mwongozo ambayo
yanapaswa kuzingatiwa kikamilifu na Maafisa Masuuli wote wakati wa maandalizi
ya bajeti ya mwaka 2018/19 ni pamoja na haya yafuatayo:
Moja: Ukusanyaji
wa Mapato ya Ndani: Maafisa
Masuuli wote wahakikishe kuwa makusanyo yote yanawekwa
kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali; Kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa
mapato; Kuhakikisha zabuni za watoa huduma na makandarasi zinatolewa kwa wanaotumia
mashine za kielektroniki; na kuhakikisha kuwa kampuni zote ambazo Serikali ina
hisa zinaendeshwa kwa ufanisi na hivyo kutoa gawio stahiki kwa Serikali.
Mbili: Kudhibiti
Matumizi na Kupunguza Gharama: Maafisa Masuuli wote waendelee kufanya uhakiki wa watumishi ili kuhakikisha kuwa mishahara
inalipwa kwa watumishi wanaostahili. Aidha, uhakiki wa kina uendelee kufanywa
kwa waliokwama madaraja ili wapandishwe, na malimbikizo ya Watumishi yabainishwe
na pia madeni ya Watumishi yawekwe vizuri ili kufikia hatua ya kuanza kulipa. Pamoja
na hatua hiyo, maafisa masuuli waendelee kuchukua hatua za kupunguza matumizi
ya Serikali kwa kufanya tathmini ya gharama za uendeshaji wa taasisi za Serikali
ili kuchukua hatua stahiki, na kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali zinazojiendesha kibiashara, zinapata faida na kuacha
kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu.
Tatu: Kulipa na Kuzuia Ongezeko la Madeni ya
Serikali: Maafisa
Masuuli wote wahakikishe madai ya watoa huduma yote
yamehakikiwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali na kuingizwa kwenye hesabu za
fungu husika, kutoingia mikataba ya miradi mipya bila kuwa
na uhakika wa upatikanaji fedha; na Kuzingatia matumizi ya hati za
ununuzi zinazotolewa kwenye Mfumo wa Malipo ili kudhibiti ulimbikizaji wa
madai.
18.
Mheshimiwa
Spika, uandaaji wa Mpango na Bajeti una mchakato na ratiba yake ya kila
mwaka ambayo inapaswa kufuatwa na kuzingatiwa na wadau wote. Aidha, baada ya
kupata maoni na ushauri wa Bunge kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na
Mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19, nitumie fursa hii
sasa kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha kazi hii na kusambaza mwongozo
wa maandalizi wa Mpango na Bajeti kwa Wadau wote ili kuwezesha Wizara, Mikoa,
Mamlaka za Serikali za Mitaa na taasisi zote za umma zianze mchakato wa
maandalizi wa Mpango na Bajeti wa Mwaka 2018/2019, kwa kuzingatia
tuliyokubaliana.
19.
Mheshimiwa
Spika, napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha viongozi na watendaji wote
Serikalini kuzingatia kikamilifu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya
Mwaka 2018/2019 ili kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.
20.
Mheshimiwa
Spika, naomba kutumia fursa hii kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kwa nafasi
zao kama Wajumbe wa Mabaraza ya Madiwani kwenye Halmashauri za Majimbo yao wawasaidie
kutoa elimu na ufafanuzi kuhusu mchakato wa maandalizi ya Mpango wa Bajeti wakati
wa Baraza la Madiwani. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwaelekeza
Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wazingatie miongozo hii iliyotolewa na wawashirikishe
wananchi na sekta binafsi katika kupanga Mipango ya Maendeleo ya maeneo yao.
HALI YA UCHUMI
21.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala
wa mapendekezo ya Mpango wa Bajeti, zipo hoja zilizotolewa na Waheshimiwa
Wabunge ambazo zilihitaji kupata ufafanuzi kuhusu mwenendo na hali ya uchumi
nchini. Napenda kutumia fursa hii
kulifahamisha Bunge lako tukufu kwamba viashiria muhimu vya uchumi jumla
vinaonyesha kwamba mwenendo wa uchumi wetu ni wa kuridhisha. Kwa mfano, ukuaji
wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka 2017 ulikua kwa asilimia 5.7; robo ya pili ilikuwa asilimia 7.8 na nusu ya kwanza ya mwaka huu ilikuwa ni asilimia 6.8. Vilevile, kufuatia
kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali,
nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufikia asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017.
Pia akiba ya fedha za kigeni inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje
ya nchi kwa zaidi ya kipindi cha miezi mitano (5); ikiwa ni zaidi ya lengo la
miezi minne.
22.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kasi
ya upandaji bei, takwimu zinaonyesha kwamba katika nusu ya mwaka 2017, mfumuko
wa bei uliendelea kubaki katika kiwango cha tarakimu moja. Aidha, taarifa za hivi karibuni kutoka
Taasisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kwamba mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Oktoba 2017 ulikuwa ni asilimia 5.1
ikilinganishwa na asilima 5.3 mwezi
Septemba, 2017. Kupungua kwa kasi ya ongezeko la mfumuko wa bei mwezi Oktoba,
2017 kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula, ambavyo
vimepungua kutoka wastani wa asilimia
9.3 mwezi Septemba, 2017 hadi asilimia
8.8 mwezi Oktoba, 2017.
23.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya bidhaa za
vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mtama kwa asilimia 9.3, viazi mviringo asilimia 6.9, unga wa mtama asilimia 5.5; ndizi za kupika kwa asilimia 4.2, unga wa muhogo asilimia 2.2 na mbogamboga asilimia 1.7.
24.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kuwa Serikali
itaendelea kusimamia kwa karibu viashiria vya uchumi jumla ili kuwezesha hali
bora ya maisha ya wananchi walio wengi hasa wa vijijini.
UBORESHAJI WA
MIUNDOMBINU
Ujenzi wa Reli kwa Standard Gauge
25.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza
utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge itakayokuwa na urefu wa Km. 1,219. Katika awamu
ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo, mkataba wa ujenzi wa reli kutoka Dar es
Salaam – Morogoro (Km. 205 na Km. 95 za njia za kupishana) ulisainiwa tarehe 3 Februari 2017 na
ujenzi ulizinduliwa tarehe 12 Aprili
2017. Mkandarasi anayejenga reli hii ni kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki yenye ubia na kampuni ya Mota-Engil Africa ya Ureno kwa gharama
ya shilingi trilioni 2.73. Mradi huu unatarajiwa kukamilika Agosti, 2019. Aidha,
kwa awamu ya pili ya ujenzi wa reli hiyo, kwa kipande cha kutoka
Morogoro-Makutupora (Km 442 pamoja na njia za kupishana), mkataba
wa ujenzi ulisainiwa tarehe 29 Septemba 2017 na mkandarasi ambaye ni kampuni ya
Yapi Merkezi ameanza maandalizi ya
kazi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2020 kwa gharama ya shilingi trilioni 4.29.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda (Hoima –
Tanga)
26.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza
utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika
Mashariki kutoka Kabaale-Hoima (Uganda) hadi Bandari ya Tanga (Tanzania). Napenda kukujulisha kuwa maandalizi ya
utekelezaji wa mradi huu yanaendelea vizuri ambapo hatua iliyofikiwa kwa sasa
ni uwekaji wa jiwe la msingi ili kuanza rasmi ujenzi wa bomba. Uwekaji wa jiwe
la msingi kwa upande wa Tanzania ulifanyika tarehe 5 Agosti 2017, katika eneo la Chongoleani lililopo katika Wilaya ya Tanga, Mkoa wa Tanga na
Tarehe 11 Novemba 2017 katika eneo
la Hoima kwa upande wa Uganda.
27.
Mheshimiwa Spika, matokeo chanya
kutokana na utekelezaji wa mradi huu yatakuwa ni pamoja na kuzalisha ajira za
muda mfupi na za muda mrefu wakati wa ujenzi na katika kipindi chote cha
uendeshaji. Ajira za moja kwa moja zinatarajiwa kuwa takribani 10,000 Katika kipindi cha ujenzi na takribani 1,000 katika kipindi cha uendeshaji. Mradi huu utahusisha
mikoa minane (8) ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara,
Tanga na Wilaya 24 pamoja na Vijiji 134 vya mikoa hiyo.
Manufaa
mengine ni pamoja na kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uganda,
kufunguka kwa biashara kwa ukanda wa Kaskazini (Northern Corridor), kuchochea shughuli za utafutaji wa mafuta
hususan katika Ziwa Eyasi na Ziwa Tanganyika na kuongeza matumizi ya bandari ya
Tanga hivyo kuongeza mapato katika bandari hiyo kwa takribani Dola za Marekani
milioni 200 kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya ujenzi.
28.
Mheshimiwa Spika, gharama za ujenzi
wa mradi zinakadiriwa kuwa jumla ya Dola
za Marekani bilioni 3.5, sawa na takribani shilingi trilioni 8.09 na utekelezaji wa mradi utachukua muda wa
takribani miaka mitatu hadi kuanza kusafirisha mafuta. Mradi huu ulianza rasmi
tarehe 12 Oktoba 2015 kwa kusainiwa
kwa mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) kati ya Serikali ya Tanzania na
Serikali ya Uganda. Kampuni zinazotekeleza Mradi huu ni TOTAL (Ufaransa), CNOOC
(China) na TULLOW (Uingereza). Mradi unatarajiwa kukamilika Mwaka 2020.
Uboreshaji
wa Bandari
29.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kuziboresha bandari za Dar es Salaam, Tanga, Bagamoyo na Mtwara ili kuziongezea
ufanisi zaidi wa kuhudumia mizigo. Uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam
utasaidia kuongeza usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za jirani ambazo hazina
bandari. Uboreshaji wa bandari ya Tanga utasaidia kuhudumia mradi wa mafuta
pamoja na usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Kwa upande wa
bandari ya Mtwara, uboreshaji wake utasaidia huduma za usafirishaji wa gesi,
chuma, makaa ya mawe na madini ya viwandani. Mradi wa Bandari ya Bagamoyo upo kwenye mpango
wa Special Economic Zone (SEZ)
inayojengwa kwa ubia kati ya China na Oman.
HIFADHI YA MAZINGIRA
30.
Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nitumie nafasi hii kuzungumzia
kidogo kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira ambayo ni muhimu kwa nchi yetu.
31.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu
ya Tano imeandaa mikakati mbalimbali ya kudhibiti na kukabiliana na changamoto
ya uharibifu wa mazingira, hususan uharibifu wa vyanzo vya maji, matumizi
yasiyo endelevu ya ardhi, misitu na bioanuai nyingine. Mikakati hiyo ambayo inatekelezwa na sekta
zote ni pamoja na Mkakati wa Taifa wa
kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Mkakati wa Taifa wa hatua za haraka za
kuhifadhi mazingira ya pwani, bahari, mito na mabwawa. Mikakati mingine ni
Mkakati wa Taifa wa kupanda na kutunza miti, Mkakati na Mpango Kazi wa
Taifa wa Hifadhi ya Bioanuai na Programu
ya Taifa ya kukabiliana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame nchini.
32.
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha
kwamba mikakati ya hifadhi ya mazingira inatekelezwa kwa ufanisi na tija,
Serikali imeweka utaratibu maalum wa ushirikishwaji wa wananchi na Mamlaka za
Serikali za Mitaa katika uhifadhi wa mazingira hasa kuhusu utunzaji wa vyanzo
vya maji, uhifadhi wa maeneo ya pwani na fukwe, upunguzaji wa gesijoto pamoja
na usimamizi na uhifadhi endelevu wa maliasili zikiwemo rasilimali za misitu,
wanyamapori, viumbe wa majini na bioanuai zilizopo nchi kavu na baharini. Hizo
ndio jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
33.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
utekelezaji makini wa Sera, Sheria na mikakati endelevu ya uhifadhi wa
mazingira, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi hiki kifupi imefanikisha
mambo yafuatayo:
Moja: Serikali imeongeza hamasa na ushirikishwaji
mkubwa wa wananchi katika suala la usafi, utunzaji na uhifadhi wa mazingira
katika maeneo yote ikiwemo makazi yao. Hatua
hiyo imetokana na ushiriki mkubwa wa Viongozi wa Kitaifa, Waheshimiwa Wabunge,
viongozi wa mikoa na watendaji wa ngazi zote katika shughuli za usafi na
uhifadhi wa mazingira.
Mbili: Baraza la Taifa na Usimamizi wa Mazingira
ambalo lipo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais limekubaliwa kuwa taasisi muhimu
duniani ya kusimamia shughuli za Mfuko wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabia Nchi (Adaptation Fund). Pamoja na mambo
mengine hatua hiyo, imewezesha pia kupatikana kwa rasilimali fedha zaidi ya
Dola za Marekani Milioni 100 kutoka
Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabia Nchi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa
kutoa maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka katika Mkoa wa Simiyu.
Tatu: Kikosi Kazi Maalum kilichoundwa na
Serikali kimekamilisha kazi ya kuandaa mapendekezo ya Mkakati wa hatua za
haraka na hatua za muda mrefu za kuongoa ikolojia ya bonde la mto Ruaha Mkuu ili kuhakikisha maji
yanatiririka mwaka mzima kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ya Kidatu na Mtera
na kwenye Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Nne: Ili kuimarisha ukaguzi wa masuala ya hifadhi
ya mazingira nchini, Serikali imeongeza idadi ya Wakaguzi wa Mazingira (Environmental Inspectors) kutoka 62 hadi kufikia 512 kwa mwaka 2017. Aidha, Serikali imefanya ukaguzi wa Viwanda 380 Nchini kwa lengo la kufanya
tathmini za mazingira pamoja na kutoa elimu na uelewa kuhusu uendeshaji
endelevu wa viwanda kwa kuzingatia utunzaji bora wa mazingira. Vilevile,
Serikali imetoa vyeti vya mazingira 1,500
kwa wawekezaji kwa ajili ya kuhakikisha uwekezaji endelevu.
Tano: Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanikiwa kufungua vituo viwili (2) vilivyoko eneo la Ras Mkumbuu huko Pemba na Mafia mkoani
Pwani kwa lengo la kuwajengea uwezo wataalam wa maeneo husika kuhusu taarifa za
ikolojia ya mawimbi, ukusanyaji wa taarifa za uchafuzi wa mazingira ya maeneo
ya pwani na mmomonyoko wa fukwe.
Sita: Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na ofisi za
kisekta imefanikiwa kuongeza usahihi wa taarifa za
utabiri wa hali ya hewa. Tumefunga mitambo (AWS-36)
jambo ambalo limesaidia kufanya utabiri kuwa sahihi kwa asilimia 82 hadi 87. Barani Afrika, vituo vya namna
hii viko katika nchi mbili tu, ambazo ni Tanzania na Ethiopia.
34.
Mheshimiwa Spika, mafanikio haya
yametokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambaye ameonyesha uongozi mahiri uliotukuka na wakupigiwa mfano barani
Afrika na duniani kote, hasa kwa kuwa amedhihirisha kuwa ana dira, maono na
kwamba anapenda Watanzania waweze kupata maendeleo endelevu na kuishi katika
mazingira bora na tulivu. Aidha, napenda kutumia fursa hii kumpongeza
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa uongozi wake mahiri wa kumsaidia Mheshimiwa Rias ikiwa ni pamoja
na kuhakikisha usimamizi makini wa masuala ya Hifadhi ya Mazingira unakuwa
endelevu.
SEKTA YA KILIMO
Mwelekeo wa
Upatikanaji wa Mvua na Msimu wa Mvua za Vuli
35.
Mheshimiwa
Spika, msimu wa mvua za vuli ulioanzia mwezi Oktoba 2017 na sasa unaendelea
hadi Desemba (vuli) ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa
mwaka (Ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini
na maeneo ya Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma).
36.
Mheshimiwa
Spika, katika msimu huu, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani katika
maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Dar es
Salaam, Tanga, Pwani, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, pamoja na Kaskazini mwa
mkoa wa Morogoro. Napenda kutoa wito kwa
wakulima wa maeneo hayo, watumie mvua hizi kulima mazao yanayoendana na msimu
huu.
37.
Mheshimiwa
Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya
kilimo ikiwa ni pamoja kuratibu kilimo, maandalizi, pembejeo (mbegu na madawa),
kuimarisha ushirika, masoko na, kuimarisha Bodi za Mazao, pale palipo na Bodi.
Vilevile, Serikali imekuwa ikitoa matamko ya kuwahimiza Maafisa Ugani na
Maafisa Ushirika wasimamie kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwenye
maeneo waliyoko. Aidha, Maafisa Kilimo wamekuwa wakihimizwa kutoa elimu ya
ugani na kuhimiza matumizi ya pembejeo zenye ubora. Vilevile, Serikali imekuwa
ikitenga fedha za kuimarisha vituo vya utafiti vya kilimo kama vile Naliendele,
Kilosa, Ukiriguru na Uyole. Pia Serikali imeondoa tozo mbalimbali zisizo na
tija kwenye mazao ya biashara na chakula.
38.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na
malalamiko ya wakulima juu ya tatizo la masoko ya mazao ya tumbaku na mbaazi.
Serikali imeendelea kutafuta masoko ya mazao hayo kwa kuzungumza na
wafanyabiashara na kwa sasa suala la mbaazi bado tunawasiliana na Serikali ya
India ili ikubali kununua mbaazi zote. Mazungumzo hayo yatakapokamilika,
tutatoa taarifa. Kwa upande wa tumbaku, tumefanikiwa kuyapata makampuni mawili
ya TGTS na Alliance One ambayo yako
tayari kununua tumbaku iliyobaki kuanzia Jumanne ijayo, kwa sasa wanaratibu
kufahamu vituo tumbaku ilipo ili wakaichukue.
SEKTA YA ELIMU
a)
Hali ya
Matokeo ya Darasa la Saba,
2017
39.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu tulikuwa
na watahiniwa 916,885 wa shule za msingi waliosajiliwa kufanya mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi. Kati yao, watahiniwa
909,950 sawa na asilimia 99.24 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani. Watahiniwa
6,935 sawa na asilimia 0.76 ya wote waliosajiliwa hawakufanya mtihani kutokana
na sababu mbalimbali, zikiwemo utoro na ugonjwa. Taarifa ya matokeo ya mtihani
huo, inaonyesha kuwa watahiniwa 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani huo sawa
na asilimia 72.76, ikilinganishwa na asilimia 70.36 kwa mwaka 2016, walikuwa wamefaulu.
Hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.4.
40.
Mheshimiwa Spika, takwimu za matokeo zinaonesha kuwa ufaulu katika
masomo ya Kiswahili, English Language
na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.25 hadi 10.05 ikilinganishwa na
mwaka 2016. Napenda kutumia fursa hii kwanza kuwapongeza sana Walimu kwa kazi
nzuri na pili kuwahimiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na
watendaji wa sekta ya elimu wasimamie kikamilifu maendeleo ya taaluma katika
maeneo yao ili ufaulu uongezeke. Pia, nawapongeza wanafunzi waliofaulu kwenye
mitihani yao. Ninawatakia heri wakapokwenda kujiunga na masomo yao ya
sekondari.
b)
Uboreshaji
wa Mazingira ya Kufundishia na
Kujifunzia
41.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
na uboreshaji wa miundombinu ya shule kwa lengo la kuimarisha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia. Mkakati wa kuimarisha miundombinu hii imejumuisha
ujenzi, upanuzi na ukarabati wa shule za Serikali zilizojengwa na wananchi,
maarufu kama shule za kata. Katika miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Tano
ujenzi umefanyika wa madarasa, vyoo, mabweni, mabwalo, ofisi za walimu, nyumba,
uzio wa shule, visima, maktaba na maabara katika shule mbalimbali za umma zenye
mahitaji makubwa pamoja na ukarabati wa miundombinu mingine chakavu katika
shule hizo. Napenda kutumia nafasi hii ya kipekee kuipongeza Ofisi ya Rais –
TAMISEMI kwa kusimamia ukarabati wa miundombinu chakavu kwenye shule kongwe ili
kuziwezesha kutumika kwa ufanisi zaidi. Pia niwapongeze viongozi wote wa Mikoa,
Halmashauri za Wilaya kwa usimamizi thabiti wa Mipango ya Elimu kwenye maeneo
yao. Malengo yetu ni kuhakikisha kuwa miundombinu hii inatumika vizuri na
inadumu kwa muda mrefu.
c)
Maboresho
katika Vyuo vya Elimu
ya Juu
42.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imekamilisha ujenzi wa mabweni mapya 20 kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mabweni hayo yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 3,840, yalizinduliwa tarehe 15
Aprili, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli. Aidha, ujenzi wa maktaba inayoweza kuchukua wanafunzi
2,500 kwa wakati mmoja unaendelea kujengwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
na Serikali inakamilisha ujenzi wa jengo la mihadhara katika Chuo Kikuu
Kishiriki cha Elimu Mkwawa. Jengo hili litakapokamilika litakuwa na uwezo wa
kuchukua wanafunzi 1,200 kwa mkupuo. Vilevile, Serikali imekamilisha awamu ya
kwanza ya ujenzi wa majengo ya Taasisi za Sayansi za Bahari, katika kijiji cha Buyu,
Zanzibar.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
na juhudi za kuongeza wanafunzi wa fani ya udaktari kwa kukamilisha ujenzi wa
majengo ya hospitali ya kufundishia ya Mloganzila iliyo chini ya Chuo Kikuu cha
Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, ambayo itazinduliwa rasmi tarehe 22
Novemba, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli. Aidha, ujenzi wa mabweni, madarasa, vyumba vya mihadhara,
maabara, maktaba na ofisi za walimu katika Kampasi hii umeanza na utakamilika
ndani ya miezi 18.
44.
Mheshimiwa Spika, kupitia kuimarika
kwa mahusiano yetu ya kidiplomasia kati ya mwaka 2016/17 na mwaka 2017/18,
Serikali imeratibu upatikanaji wa wanafunzi wa Kitanzania wanaofadhiliwa kusoma
nchi za nje hususani China (86), Uingereza (17), Misri (4), Korea (3), Urusi
(13) na Thailand (2) ambapo baadhi ya wanufaika ni wahadhiri wa vyuo vikuu na
taasisi nyingine za elimu ya juu nchini. Katika mwaka 2017/18, Serikali
imepanga kusomesha wahadhiri 100 katika ngazi za shahada za umahiri na uzamivu
ili kukabiliana na upungufu wa wahadhiri. Mwezi Septemba, 2017 Serikali ilitia
saini makubaliano na nchi ya Hungary ambapo itakuwa inatoa ufadhili wa masomo
kwa wanafunzi 30 kwa kipindi cha miaka mitatu kuanza mwaka 2018/2019.
d)
Maboresho
ya Vyuo vya
Ualimu nchini
45.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea
kujenga na kukarabati Vyuo vya Ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na
Shinyanga kwa thamani ya shilingi
bilioni 36.47. Mradi huu
utatekelezwa kwa miaka mitatu (2016/2017 - 2018/2019) na unalenga kuongeza
fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu. Ujenzi
na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali
kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka
2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019; ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300.
46.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia
imefanya ukarabati mkubwa wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia pamoja na
mabweni katika vyuo 10 vya ualimu, ambavyo ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu,
Korogwe na Tabora. Ukarabati huu
umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa
wanasoma Stashahada maalum ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA katika Chuo Kikuu cha
Dodoma kuhamishiwa katika vyuo hivyo.
Ukarabati wa vyuo hivi uligharimu shilingi
bilioni 11.9.
47.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza
maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya
Serikali. Vyuo hivyo ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka,
Patandi na Ilonga. Aidha, Vyuo vya Ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda
vitajengwa upya kufuatia taarifa ya Wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai
kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya
Tano katika kipindi cha miaka miwili imetoa mafunzo kwa wakufunzi 249 wa masomo
ya Sayansi na Hisabati ili waweze kufundisha masomo hayo kwa kutumia TEHAMA; imenunua na kusambaza kompyuta 370,
kompyuta mpakato 20 na projekta 27 kwa vyuo vya ualimu 12 ambavyo ni
Morogoro, Mpwapwa, Tabora, Mtwara Kawaida, Monduli, Butimba, Kleruu, Kasulu,
Songea, Marangu, Korogwe na Tukuyu. Sambamba na hatua hiyo Serikali kupitia
mradi wa ualimu itanunua vitabu na kuimarisha maktaba; kuimarisha maabara za
TEHAMA; kuimarisha ufundishaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati; kuimarisha
ufundishaji wa walimu wa elimu ya awali na kupitia Mitaala ya Elimu Ualimu ili iendane
na mahitaji ya sasa. Lengo la hatua hizi ni kuimarisha vyuo vya ualimu ili tuweze
kupata walimu mahiri.
SEKTA YA AFYA
Watanzania wote kuwa na Bima ya Afya
49.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imeendelea kutekeleza mikakati ya
kuhakikisha wigo wa wanufaika wa bima ya afya nchini inaongezeka.
Hadi kufikia
Septemba 2017, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa unahudumia wanufaika 3,346,631 sawa na asilimia 7 ya Watanzania wote.
Aidha, Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na wanufaika 11,779,338 sawa na asilimia
24 ya Watanzania wote. Wananchi wanaonufaika na mpango wa bima ya afya nchini
chini ya NHIF and CHF wamefikia 15,125,969
sawa na asilimia 31 ya Watanzania wote ikilinganishwa na
asilimia 20 iliyokuwa mwaka 2014/15.
50.
Mheshimiwa Spika, mafanikio hayo yanatokana na kuruhusu makundi mengi kujiunga na mifuko hiyo wakiwemo wajasiriamali, vikundi vya VICOBA, SACCOS, wavuvi, waendesha
bodaboda, watoto wenye umri chini ya miaka 18, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya
juu, n.k. Serikali itaendelea kusisitiza wananchi wajiunge na bima hiyo.
51.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeendelea kutekeleza
mpango wa NHIF/CHF kwa wanawake wajawazito na watoto, kwa kushirikiana na Benki
ya Maendeleo ya Ujerumani. Mpango huu una lengo la kupunguza vifo vya akinamama
na watoto ili kwenda sambamba na utekelezaji wa Malengo ya Kimataifa ya
Maendeleo Endelevu. Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2017, wanawake
71,102 katika mikoa ya Mbeya, Tanga, Lindi, Mtwara na Songwe
wamehudumiwa. Lengo ni kuwafikia wanawake 180,000 na hivyo kufanya jumla
ya wanawake 905,938 wanufaike na mpango huo.
52.
Mheshimiwa Spika, natoa wito wa
viongozi wa Wizara ya Afya, Mkoa, Halmashauri na Waheshimiwa Wabunge katika
kuhamasisha wananchi wajiunge na mifuko ya Bima za Afya (NHIF) na (CHF) katika
majimbo yetu.
Hali ya Upatikanaji wa
Dawa nchini
53.
Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji
wa dawa nchini imeendelea kuimarika
katika Bohari ya Dawa (MSD) na vituo vya kutolea huduma za Afya. Hadi kufikia
Oktoba, 2017 Serikali imetoa Shilingi
bilioni 53 kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Hii iliwezesha upatikanaji wa dawa
muhimu (essential medicines) katika bohari
kufikia asilimia 80.
Aidha, taarifa
zilizokusanywa kutoka Halmashauri mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa, dawa
muhimu (essential medicines) zinapatikana
kwa wastani wa asilimia 91.4. Dawa
hizi ni pamoja na za kutibu malaria, TB (Kifua Kikuu), maambukizi ya bakteria
na (antibiotics), dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) na dawa za uzazi
salama.
54.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
upatikanaji wa dawa kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU, napenda kulifahamisha
Bunge lako tukufu kwamba, kwa mara ya kwanza Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti
UKIMWI (AIDS Trust Fund) umetoa shilingi
milioni 660 kwa ajili ya kununua dawa za Cotrimoxazole (Septrin) ambazo hutumika kutibu na kuzuia magonjwa
nyemelezi (opportunistic infections)
kwa watu waishio na virusi vya UKIMWI (WAVIU).
Aidha,
kiasi cha shilingi milioni 200 kimetolewa kwa mkoa wa Manyara kuchangia ujenzi
wa kituo cha afya Mererani katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, ambacho
licha ya kutoa huduma nyingine za afya, kitatumika kutoa huduma za kufubaza VVU
(ARVs) kwa WAVIU. Kituo hiki pia
kitakuwa kitovu cha uelimishaji wa wananchi wote kujiepusha na maambuzi mapya
ya VVU. Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau wote wa maendeleo waliopo ndani
na nje ya nchi waunge mkono juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa malengo ya
kutokomeza VVU na UKIMWI yanafikiwa.
SEKTA YA KAZI NA
AJIRA
Uwezeshaji wa
Wahitimu
55.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Pili wa
Maendeleo wa Taifa unatafsiri maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha
Mapinduzi kwa kuweka maeneo mahususi ya kuwezesha vijana wawe na ujuzi stahiki
wa kuajirika au kujiajiri katika soko la ajira la ndani na la nje ya nchi. Ili kuwezesha
vijana hao wawe na ujuzi stahiki, katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali
ilianza kutekeleza Programu ya Taifa ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi ambayo
imejikita katika maeneo muhimu yafuatayo:-
Moja: Kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (Apprenticeship) ambapo mhusika anatumia asilimia 60 ya muda wa
mafunzo akiwa kazini na asilimia 40 akiwa darasani.
Mbili: Kutoa mafunzo ya ujuzi na uzoefu kazini (Internship) kwa wahitimu wa ngazi
mbalimbali za elimu na mafunzo hususan wale wa vyuo vikuu. Mafunzo haya yanahusisha vijana
waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu ambao wanapatiwa fursa ya kujifunza kwa
vitendo katika maeneo ya kazi ili wapate uzoefu wa kazi na kuwawezesha
kuajiriwa au kujiajiri.
Tatu: Kutoa mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa
mafunzo. Mafunzo haya yanahusisha kutambua watu wenye ujuzi uliopatikana katika
mfumo wa mafunzo usio rasmi, kuwapa mafunzo kutokana na mapungufu yatakayobainika
na kuwapatia vyeti. Kwa kutumia vyeti hivyo wanaweza kujiendeleza kielimu,
kuboresha huduma wanazotoa na kutafuta ajira.
Nne: Kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini. Mafunzo haya yanalenga
kujenga uwezo wa nguvukazi iliyoko kazini ili iendane na mabadiliko ya
teknolojia na kufanya kazi kwa weledi zaidi ili kuongeza tija na ufanisi kazini
na kuongeza uwezo wa ushindani wa nchi. Mafunzo haya yanawalenga walioajiriwa
na wale waliojiajiri katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
56.
Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa tangu
tuanze kutekeleza programu hii katika mwaka wa fedha 2016/17, tumetoa
mafunzo kwa jumla ya vijana 11,492 katika fani mbalimbali kupitia vyuo
vya umma, binafsi na makampuni mbalimbali.
57.
Mheshimiwa Spika, kati
ya hao, vijana 3,000 wamepatiwa mafunzo ya kubuni na kutengeneza nguo kwa kutumia teknolojia
za kisasa kupitia viwanda vya Tooku (Dar es Salaam) na Mazava (Morogoro). Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa zaidi ya vijana 2,600 wameajiriwa na viwanda
hivyo.
58.
Mheshimiwa Spika, Aidha, katika
mwaka huu wa fedha (2017/18) Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imetoa
fursa za mafunzo mbalimbali ya vitendo.
Serikali imekutana na sekta binafsi kupitia Chama cha Waajiri Tanzania
(ATE), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Baraza la Taifa la Biashara
(TNBC) na kukubaliana kuwa ifikapo Desemba, 2017 vijana wote wawe wamepatiwa
fursa za mafunzo katika maeneo ya kazi.
59.
Aidha, katika kujenga ujuzi wa
vijana kushiriki kwenye shughuli za kilimo, tumeshirikisha Wakuu wa Mikoa yote na
kuwaelekeza waandae maeneo ya kujifunzia vijana hao kwenye Halmashauri zote za mikoa
yao. Tayari ofisi yangu imepokea maombi ya kushiriki kutekeleza programu ya
kukuza ujuzi katika eneo la kilimo kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Green
House) kutoka mikoa ya Kagera, Manyara, Ruvuma, Kilimanjaro na
Shinyanga. Ofisi yangu imefika katika Halmashauri zote za mikoa hii ili
kujiridhisha kuwa imetenga maeneo kwa ajili ya kujenga vitalu vyumba vya
kufundishia. Mafunzo haya yataanza rasmi Desemba, 2017 katika Halmashauri zote
zilizowasilisha maombi.
60.
Mheshimiwa Spika, napenda
nilihakikishie Bunge lako tukufu kuwa, Serikali itahakikisha, sekta zote za
kipaumbele kama zilivyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano,
zinapata nguvukazi yenye ujuzi stahiki kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje
ya nchi. Nichukue fursa hii kutoa wito kwa viwanda na taasisi mbalimbali zishirikiane
na Serikali kutoa nafasi kwa vijana wetu kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya
kazi na kupata uzoefu na ujuzi stahiki.
Tuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu walioomba kushiriki mafunzo ya
vitendo na kupata uzoefu wa kazi. Natoa wito kwa waajiri watoe nafasi kwa
vijana wetu hawa kujifunza kwa vitendo. Serikali itaendelea kugharamia mahitaji
ya msingi ya vijana hawa wakati wa mafunzo hayo.
SEKTA YA ARDHI
61.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi
inatekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi nchini na Sheria ya Upangaji
Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Sura 116. Katika utekelezaji wa Sheria na Mpango
huo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na:
Moja: Kuandaa Mipango ya Matumizi ya
Ardhi ya Kikanda kama vile SAGCOT na Mpango wa Matumizi ya Ardhi Kanda ya
Kaskazini.
Mbili: Kutoa mafunzo kwa Halmashauri za Wilaya 110 kuhusu uandaaji, utekelezaji
na usimamizi wa mipango ya matumizi ya ardhi nchini.
62.
Mheshimiwa Spika, natoa wito
kwa Wizara ya Ardhi kushirikiana na Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba
zinakuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi na kupima ardhi yote kwa
kuzingatia mipango hiyo.
SEKTA YA MALIASILI
NA UTALII
Uendelezaji Utalii
63.
Mheshimiwa Spika, utangazaji utalii unaongozwa
na Mkakati wa Miaka Mitano ya Utangazaji Utalii wa Nje (International Marketing Strategy 2013-2018) ambao ulitayarishwa
kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kwa mwaka 2016/2017, Wizara ilibaini vivutio
vya utalii katika mikoa minne ya Rukwa, Katavi, Singida na Tabora kwa lengo la
kuvitambua, kuviendeleza, kuvitangaza na kuvutia uwekezaji katika maeneo hayo. Katika kuongeza idadi ya watalii nchini,
Wizara imeendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha
miundombinu kwa kukarabati kilometa
2,571.2 za barabara zilizopo ndani ya hifadhi.
Juhudi hizi zimesaidia kupata ongezeko la watalii kutoka 1,137,182 mwaka
2015 hadi kufikia 1,284,279 mwaka 2016 sawa na asilimia 12.9; Kuongezeka
kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka
2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2 mwaka 2016.
64.
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini ambako
kuna vivutio vingi vya utalii lakini pamekuwepo idadi ndogo ya watalii
wanaotembelea ukanda huu ukilinganisha na ukanda wa Kaskazini. Katika
kutekeleza hilo, Serikali imepokea Dola za Marekani milioni 150 kupitia mradi
wa Resilient Natural Resource for Tourism
and Growth (REGROW) ambao utaanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
Lengo la mradi huu ni kuongeza mchango wa sekta ya
utalii katika uchumi kwa kuongeza ubora wa vivutio vya utalii kwa kuboresha
miundombinu ndani ya hifadhi, usimamizi wa maliasili na kuongeza faida kiuchumi
kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo kuzunguka hifadhi hizo. Hata hivyo, tunaimarisha matangazo ya vivutio
kwa kuwaruhusu Wakuu wa Mamlaka za Mapori kuanza kutangaza vivutio vilivyo
katika Mamlaka zao. Kazi hiyo watashirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
ambao wana jukumu la utangazaji.
65.
Mheshimiwa Spika, ninamwagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za
Bahari na Maziwa ili kutangaza utalii na kuendeleza fukwe zote ambazo hazina
shughuli za kitalii. Fukwe za bahari ni eneo mojawapo ambalo likiendelezwa
vizuri, linaweza kuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi.
66.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kukusanya mapato, Serikali imeboresha mifumo ya
ukusanyaji kwa kutumia njia ya kielektroniki ambapo kwa Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro mapato yameongezeka kutoka shilingi
bilioni 60.1 mwaka 2014/2015 hadi kufikia
shilingi bilioni 102 mwaka 2016/2017. Natoa wito kwa Wizara ya Maliasili na
Utalii iongeze kasi ya kuleta mabadiliko katika sekta nzima ya maliasili ili
iweze kuchangia zaidi kwenye uchumi.
SEKTA YA MIFUGO
Upigaji chapa mifugo
67.
Mheshimiwa Spika, utambuzi wa mifugo
kwa njia ya chapa ya moto ni utekelezaji wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na
Ufuatiliaji Mifugo Sura Na 184 na Kanuni zake za Mwaka 2011 chini ya G.N. namba
362. Madhumuni ya Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo kama yalivyoainishwa
kwenye Sheria ni kudhibiti magonjwa ya mifugo na magonjwa yanayoambukiza
binadamu kutokana na wanyama na hivyo kuboresha afya ya mifugo na jamii,
kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake kulingana na mahitaji ya masoko ya
ndani na kimataifa na udhibiti wa uhamishaji wa mifugo kiholela.
68.
Mheshimiwa Spika, utambuzi wa mifugo
unasaidia kutambua na kuboresha mbari (kosaafu) za mifugo, kudhibiti wizi wa
mifugo na usafirishaji holela wa mifugo kutoka eneo moja kwenda lingine bila
kufuata taratibu zilizopo na hivyo kuepusha migogoro baina ya wafugaji na
watumiaji wengine wa ardhi. Aidha, utambuzi utawezesha Serikali kupata idadi ya
mifugo hivyo kuiwezesha kupanga mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo.
Hatua za utekelezaji
69.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa
zoezi la utambuzi wa mifugo upo kwenye hatua mbalimbali katika mikoa yote
ambapo Mamlaka za Serikali za Mitaa 113
zimeanza utekelezaji wa zoezi hilo na zinaendelea. Hadi kufikia tarehe 15
Novemba 2017, jumla ya ng’ombe 5,939,328
wamepigwa chapa ambayo ni sawa na asilimia
30 kati ya ng’ombe millioni 18,957, 227 ambao wana umri zaidi ya
miezi sita. Idadi ya ngombe wanaostahili kupigwa chapa ni theluthi mbili ya
mifugo yote iliyo nchini ambayo jumla yake ni 28,435,825. Sheria ya Ufuatiliaji na Utambuzi wa Mifugo inasisitiza
kuwa ng’ombe na punda wenye umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea ndiyo
wanaostahili kupigwa chapa.
Hadi
kufikia tarehe 15 Novemba, 2017, mikoa ya Dodoma, Singida na Iringa imeonyesha
mwitikio mzuri, ambapo katika Mkoa wa Iringa, ng’ombe 230,147 wamepigwa chapa kati ya 243,521 (asilimia 98), Singida ng’ombe 837,676 kati ya 1,016,630
(asilimia 82) na Dodoma ng’ombe 1,016,977 kati ya 1,331,308 sawa na asilimia
76. Mikoa ambayo inasuasua katika utekelezaji wa zoezi hili la upigaji
chapa ni Arusha, Lindi, Mtwara, Tanga,
Tabora na Shinyanga.
70.
Mheshimiwa Spika, ng’ombe wanaofugwa
kwa mfumo wa ndani (zero grazing) na
katika mashamba rasmi ya mifugo wanakadiriwa kufikia 750,000. Hawa wanatambuliwa kwa njia ya hereni masikioni. Hadi
kufikia tarehe 15 Novemba, 2017, jumla ya ng’ombe 23,486 walikuwa wamewekewa hereni katika mikoa ya Arusha (11,727); Kilimanjaro (4,577) na Mbeya (7,182).
71.
Mheshimiwa Spika, wakati wa utekelezaji
wa zoezi la utambuzi wa mifugo, kumekuwepo na changamoto za wadau kutokuwa na
uelewa mpana kuhusu dhamira njema ya zoezi hilo. Mikakati ya kukabiliana na
changamoto hizi ni pamoja na Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu malengo ya
zoezi hili, ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na wafugaji na wadau wengine
katika ngazi ya Halmashauri, Tarafa, Kata na Vijiji.
Ninatoa
wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi washirikiane na mikoa na Halmashauri
zikamilishe zoezi la upigaji chapa kwa haraka na kutoa elimu juu ya malengo ya
chapa hizo.
Kutenga ardhi ya
mifugo
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika
juhudi zake za kuhakikisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya mifugo na
kupunguza migogoro kati ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi imeendelea kutekeleza
mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kuandaa mipango ya matumizi
bora ya ardhi na kutenga ardhi kwa ajili ya viwanda na uwekezaji.
Serikali
imeamua kupata suluhisho la kudumu katika migogoro ya wafugaji, wakulima na
wahifadhi wa mapori kwa kuainisha mipaka katika maeneo tengwa kwa kuweka alama ili
kuwaondolea kero wananchi pamoja na kuzuia mifugo kutoka nje ya nchi. Natoa
wito kwa Wakuu Mkoa na Wilaya zinazopakana na nchi jirani kufanya doria
mipakani na kwenye mapori kubaini mifugo iliyoingia nchini.
HITIMISHO
73.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa
kuwashukuru tena wote waliosaidia kufanikisha mkutano tunaomaliza leo. Shukrani za
pekee ni kwako wewe Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na
Wenyeviti kwa kutuongoza vizuri katika kipindi chote cha mkutano huu wa tisa. Aidha, nawashukuru
Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao pamoja na watumishi wote wa Serikali
waliosaidia kujibu maswali na kuwasilisha hoja za Serikali hapa Bungeni.
74.
Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru
Katibu wa Bunge, Dkt. Stephen Kagaigai pamoja na watumishi wote wa Ofisi ya
Bunge kwa kufanikisha mkutano huu. Nawashukuru wale wote waliokuwa na jukumu la
ulinzi na usalama ili kuhakikisha mkutano huu unafanyika na kumalizika salama.
Napenda pia niwashukuru madereva wote kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi
mkubwa.
Ninawashukuru
pia waandishi wa habari kwa kuhakikisha kuwa habari za hapa Bungeni zinawafikia
wananchi kwa namna mbalimbali. Mwisho, niwashukuru wananchi wa Dodoma na hasa
wa Manispaa ya Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu na hivyo
kukamilisha mkutano huu kwa mafanikio makubwa.
75.
Nitumie nafasi hii sasa kuwatakia wote safari njema
wakati mnarudi katika maeneo yenu ya kazi.
Vilevile, niwatakie Watanzania wote sikukuu njema ya Maulid ambayo kwa
mara ya kwanza itafanyika wilayani Ruangwa, mkoani Lindi; sikukuu njema ya
Krismas na kheri ya Mwaka Mpya 2018. Ninamwomba Mwenyezi Mungu atuvushe sote
salama na atufikishe mwaka 2018 ili tuweze kukutana tena katika Mkutano wa Kumi
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
76.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema
hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu sasa liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 30 Januari, 2018 litakapokutana saa 3.00 asubuhi hapa mjini Dodoma.
77.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
COMMENTS