Habari Mpya

Sunday, 19 November 2017

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka  ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuuwezesha mkoa wa Simiyu katika kufanya mapinduzi ya Kilimo kupitia miradi ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.
Mkuu wa wilaya ya Busega, Tano Seif Mwera (kulia) akiwakaribisha wageni kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania waliofika kijijini Mwamanyili kujionea chanzo cha maji na eneo litakalotumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Wageni hao waliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo, Rosebud Kurwijila (kushoto).

Mtaka amesema mkoa wa Simiyu umejipanga kutumia fursa za mikopo nafuu inayotolewa na TADB ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuhakikisha wakulima wanalima kisasa ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.

Mtaka aliongeza kuwa Mkoa wa Simiyu uko tayari kufanya kazi na Benki ya Kilimo kupitia vikundi vya uzalishaji, Halmashauri na Miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani humo.

Akaongeza kuwa hivi karibuni Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu Mkoani Simiyu yaliridhia Halmashauri hizo kukopa jumla ya shilingi bilioni 17.1 kutoka TADB kwa ajili ya kutekeleza Miradi mikubwa miwili  ya Maendeleo.
Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Eng. Tumbu akitoa maelekezo kwa ugeni kutoka TADB juu ya chanzo cha maji cha maji kitakachotumika katika mradi wa umwagiliaji wa Mwamanyili.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili ulio chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambao utekelezaji wake umepanga kukopa shilingi bilioni 10.7 na mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Meatu ulio chini ya Halmashauri ya Meatu unaohitaji shilingi bilioni 6.4.

“Tungehitaji kuwa Mkoa ambao kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo tungetengeneza namna ambayo ingewasaidia wakulima na ikasaidia mikoa mingine kuja kuona maendeleo ya kilimo  ambayo ni matokeo ya Serikali kuwekeza katika Benki ya Kilimo” amesema Mtaka.

"Sisi kama Mkoa tumejipanga, tumetoa elimu ya utayari na
namna ya utekelezaji wa shughuli zote kwa wataalam wetu pamoja na wananchi na isitoshe tayari tumeshafanya utafiti na kuandaa mwongozo wa uwekezaji ndani ya mkoa, hivyo tunawakaribisha kuwekeza,” aliongeza.

Aidha, Mtaka ameongeza kuwa Mkoa wa Simiyu unatekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda chini ya Kauli Mbiu ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo hadi sasa kuna kiwanda cha chaki na maziwa na miradi mingine minne ya viwanda iko katika upembuzi yakinifu.

“Hivyo Benki ya Kilimo inaweza kuwekeza katika miradi hii kwa kuwawezesha wakulima na wafugaji kuzalisha malighafi ya Viwanda hivyo au kuwa mdau katika viwanda hivyo,” aliomba.

Kwa upande, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Rosebud Kurwijila alisema kuwa Benki ya Kilimo imejizatiti katika kuchangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa wakulima wa Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
Bibi Kurwijila alisema kuwa katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini TADB imejipanga kutoa huduma kupitia kongani mpya nane (8) ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.
Alizitaja Kongani hizo kuwa ni pamoja na Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Mashariki. Nyingine ni Kanda ya Magharibi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kusini na Zanzibar.
“Kongani ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za kilimo zinazohusiana, wasambazaji, na taasisi zinazohusishwa katika kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau, hivyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini, benki ya kilimo itawafikia kupitia njia hii,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB Augustino Matutu Chacha  amesema wamefurahishwa na utayari wa Mkoa wa Simiyu juu ya kuwawezesha wakulima na Benki hiyo iko tayari kutoa mikopo pia kwa wakulima wa zao la pamba ambao wanazalisha zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini ili izalishwe kwa wingi zaidi na katika ubora wa hali ya juu.

Amesema wataalam wa kilimo wa Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na wataalam wa benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) watakutana ili kuona namna watakavyofanya kazi kwa pamoja ili mikopo itakayotolewa iweze kuwa wa manufaa kwa wakulima na nchi kwa ujumla.

Aidha amewaeleza Wakurugenzi wa Halmashauri zote kuwa, Halmashauri zinaweza kupatiwa mikopo ili ziweze kuendesha miradi ya kilimo itakayoweza kuwa  vyanzo vipya vya mapato kwa Halmashauri zao.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -