HUJAFA hujaumbika, msemo huu wa lugha ya Kiswahili unawiana na hali ya kijana, Joseph Chacha, aliyezaliwa akiwa mzima mwenye kutembea kwa...
HUJAFA hujaumbika,
msemo huu wa lugha ya Kiswahili unawiana na hali ya kijana, Joseph Chacha,
aliyezaliwa akiwa mzima mwenye kutembea kwa kutumia miguu yake
miwili, lakini leo hii amejikuta akihitaji msaada wa kutumia baiskeli ya
walemavu kwa ajili kumsaidia katika matembezi yake.
Kijana Chacha
alizaliwa mwaka 1995 Bunda, mkoani Mara, ambapo mwaka 1998 alipata homa ya
kichocho na kumsababishia ulemavu wa kupooza viungo vyote mpaka hivi sasa.
Anasimulia kuwa
umasikini wa kipato unao ikabili familia yake unamchango mkubwa katika ulemavu
alionao, kwani kulikua na uwezekano mkubwa wa kupona nakumaliza tatizo hilo
kama angepata matibabu stahiki.
“Magonjwa mengi
nchi za Afrika yanasabisha kukwamisha ndoto za watu wengi hususan sisi masikini. Tatizo
langu lilikuwa gumu na kuniathiri siku hadi siku kutokana na umasikini,
kama familia yangu ingekuwa na pesa basi ningepata matibabu
yanayostahili,” anasema Chacha.
HARAKATI ZA
MATIBABU
Katika mahojiano
na mwanasafu wa kurasa hii (Tuishivyo), kijana huyo anaeleza baada ya kutokea
kwa tukio hilo wazazi wake walimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Bunda ambako
alipata matibabu, lakini hayakumsaidia, ndipo wakaamua kwenda kwa mganga wa
tiba za asili kwa ajili ya kupata matibabu lakini nako hakupata nafuu
badala yake wakaamua kurudi nyumbani kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya
kuendelea kupata matibabu.
“Nilipelekwa
hospitali nikapata matibabu madaktari wakasema nina homa ya kichocho nikapata
nafuu lakini baadae homa iliendelea ndipo wazazi wangu wakaamua kunipeleka
kwenye tiba za asili homa ikaisha bali viungo vyangu vikaanza kushindwa kufanya
kazi mpaka hivi sasa.”
HARAKATI ZA
MAISHA
Pamoja na hali
yake hiyo ya ulemavu, umasikini wa familia yake, kushindwa kumudu matibabu na
mahitaji ya kila siku ya nyumbani kutokana kuishiwa kabisa pesa ya kupata
mahitaji, alimuomba mama yake ampeleke katika shule za wanafunzi wenye ulemevu
ili ajue kusoma na kuandika kwa ajili ya kuendeleza ndoto zake.
Mwaka 2007
alipelekwa Shule ya Msingi Nyansror iliyopo Bunda ambako alijifunza kusoma na kuandika lakini mwaka 2012 aliacha
kusoma akiwa darasa la tano kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama
za mahitaji ya shule pamoja na kumwongoza kutokana na uzee.
“Sikupenda
kuacha shule kwani nilikuwa na ndoto za kuendelea na shule ndio maana
nilichelewa kuanza lakini nikaona bora nisome ili niweze kufanikisha malengo
yangu, sikukata tamaa kwasababu ya hali yangu ila ilinilazimu kuacha
masomo baada ya mama yangu ambae ndio msaidizi wa maisha yangu kufariki, hapo
ndipo ugumu wa maisha ulipoanza kutokana baba yangu alikuwa mzee pia alikuwa
mlemavu wa mguu mmoja,” anasema.
CHANGA MOTO ZA MAISHA
Kijana Chacha anaeleza
katika maisha yake amepitia changamoto nyingi sana, ikiwamo baada ya kufiwa na
mama yake akanza kuombaomba misaada mbalimbali ikiwamo kanisani ili apate fedha
kwa ajili ya kusukuma maisha yao. Anasema alipoona hali inazidi kuwa ngumu
aliamua kwenda kutafuta maisha jijini Dar es Salam.
Anasema
alifika Dar es Salaam mwaka 2012 na kuanza kuombaomba na kwamba alipata changamoto mbalimbali ikiwamo kukoswa
kugongwa na magari alipo kuwa barabarani, huku akilala na kuomba misaada stendi
ya mabasi ya mikoani ya Ubungo.
Anasimulia kuwa
alipatwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hivi karibuni kutokana na kulala nje
kila siku.
WITO
Chacha anatoa
rai kwa wanajamii wote wanaoguswa na changamoto zinazowakabili walemavu kumsaidia
kwa kumchangia fedha ili aweze kupanga
na kuishi katika chumba chake na kupata mahitaji muhimu ya kila siku.
Aidha, anaiomba
serikali na wadau mbalimbali kumuonea huruma na kumnunulia bajaji pamoja na kumpatia
mtaji wa kufanyia biashara ili aweze kufanya biashara na kuendesha maisha yake.
“Nawaombe wadau
mbalimbali na serikali kunisaidia kupata mtaji ili nifanye biashara
nijimudu kimaisha, Watanzania wenzangu mimi sikupenda hii hali naumia
kulala nje kila siku nalazimika kuishi barabarani sina pa kukaa, nakula kwa
kutegemea wasamaria wema ambao wanafanyakazi maeneo hayo, pia namshukuru Mbunge
wa Ubungo, Saidi kubenea, alinipatia baiskeli hii kipindi cha kampeni ingawa
hivi sasa imeisha matairi yamepasuka kama unanyo yaona,” alisema Chacha kwa
huzuni kubwa.
COMMENTS