SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori wanapokuwa bungeni, badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na maswal...
SPIKA
wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori wanapokuwa bungeni,
badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na maswali kutoka kwa wabunge.
Ndugai
alitoa onyo hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu baada ya kuwataja
baadhi ya manaibu ili wajibu maswali lakini walishindwa kusimama kwa kuonyesha
hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa na wabunge.
“Waheshimiwa
mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana mnashindwa kusikiliza
kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite katika kusikiliza,” alisema
Ndugai.
Kiongozi
huyo alianza na naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ambaye
alimtaka ajibu swali la nyongeza la Mwantumu Dau Haji (viti maalum - CCM)
ambalo lililenga katika suala zima la upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo
cha umwagiliaji.
Kabla
ya swali hilo, tayari mbunge huyo alishauliza swali la msingi ambalo
lilielekezwa ofisi ya Makamu wa Rais na lilijibiwa na naibu waziri wa wizara
hiyo, Kangi Lugola likihusu masuala la mabadiliko ya tabia nchi.
Aweso
alisimama asijue nini cha kujibu huku akiendelea kutazamana na Spika Ndugai kwa
sekunde kadhaa ndipo akaamuliwa kuketi kwa kuwa alikuwa hajui swali gani
liliulizwa.
“Tatizo
lenu mawaziri hamsikilizi kinachoendelea ndani ya Bunge, mnapiga stori tu. Haya
naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais okoa jahazi hilo,” alisema Ndugai.
Baada
ya maswali kadhaa kupita aliwataka naibu mawaziri ofisi ya Rais (Tamisemi),
Joseph Kakunda na Joseph Kandege kujibu swali la nyongeza kuhusu umaliziaji wa
majengo ambayo yanaanzishwa na wananchi.
“Haya
naibu mawaziri Tamisemi, Josephat Kandege naomba ujibu swali hilo. Kama
hujajipanga naomba mwenzako Joseph Kakunda ajibu, jamani ndiyo haya niliyosema
wapo hapa tu lakini wanapiga stori na hawasikilizi kinachoendelea,” alisema
spika.
Ndugai
aliwaonya pia wabunge kutozungumza na waziri mkuu na kumtaka kiongozi huyo wa
shughuli za Serikali kuzungusha macho ili kuona namna ambavyo wabunge walikuwa
wamesimama na kutaka kuuliza maswali kuhusu maji.
“Mheshimiwa
waziri mkuu, naomba hao wanaozungumza na wewe wakuache kwanza, hebu geuka nyuma
na uangalie pande zote uone namna ambavyo wabunge wamesimama kutaka kuuliza
maswali kuhusu maji majimboni kwao, Serikali iangalie jambo hili,” alisema.
Wakati
huo spika aliitaka Serikali kutafakari namna ambavyo imekuwa ikitoa maagizo na
amri kila wakati kupitia mabaraza ya madiwani akisema siyo afya na haijengi.
Alikuwa
akitolea majibu mwongozo ulioulizwa na mbunge wa Babati Mjini (Chadema),
Pauline Gekul kuhusu mpango wa Serikali kuagiza wananchi kuendelea kumalizia
majengo ya zahanati, maabara na madarasa waliyoyaanzisha.
“Ndugu
zangu Serikali, anachokisema mbunge ni sahihi maana sasa imekuwa ni kero kubwa,
hebu angalieni jambo hilo kwani kila mahali ni maagizo maagizo na hata tukienda
kwenye baraza la madiwani utasikia kuna ajenda ya kudumu ambayo ni maagizo, hii
inakera jamani,” alisisiza Ndugai.
Pia,
aliwataka viongozi kuangalia namna bora ya kufanya ili kufikisha ujumbe kuliko
kuagiza kila mara ambako kunaondoa imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Hata
hivyo, alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya viongozi kujiona kama miungu
watu na wanaamini kuagiza kila wakati kwa kutumia amri ndiyo itakuwa maendeleo
wakati si kweli.
COMMENTS