SERIKALI imesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kw...
SERIKALI imesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA), unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa
sasa umefika zaidi ya asilimia Tisini.
Meneja Miradi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi, akimuonesha
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius
Kwandikwa (Mb), (Kushoto), upanuzi wa maegesho ya ndege uliofanyika uwanjani
hapo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elius
Kwandikwa, mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la kupumzikia abiria na
upanuzi wa maegesho ya ndege katika uwanja huo leo mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elius Kwandikwa (Mb),
akikagua maboresho ya mfumo wa majitaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za
ukarabati wa uwanja huo.
"Nimeridhishwa na ukarabati unaoendelea katika uwanja huu na nafikiri
mmejionea wenyewe kazi inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii
kazi itakamilika hivi karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa ukarabati huo ambao pia umehusisha
maboresho ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa
ujumla kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.
Mafundi wakiendelea na
ukarabati katika jengo la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA). Ukarabati huo umefika zaidi ya asilimia Tisini na unatarajiwa kukamilika
mwezi Desemba mwaka huu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya
ndege nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo
likiwa ni kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika
uchumi wa kati.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa,
akifafanua jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Arusha,
Mhandisi Johny Kalupale, alipokagua barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1) na
Barabara ya Mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass KM 42.4) mkoani Arusha.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi,
amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha jumla ya
ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.
Ameongeza kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka laki nane kwa mwaka
hadi kufikia milioni moja na laki mbili mara baada ya kukamilika kwa uwanja
huo.
Muonekano wa Barabara ya
Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha, ambayo imekamilika kwa kiwango cha
lami. Kukamilika kwake kumesaidia kupunguza ajali na msongamano katika eneo
hilo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina
- Tengeru (km 14.1) na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4)
ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru ni
mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia katika mkoa
huo kwani kumepelekea kupungua kwa ajali na msongamano wa
magari katika eneo hilo.
Ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara na kutunza mazingira
yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa vizazi vya
sasa na vijavyo.
Muonekano wa Daraja la
Ndurumo lililopo katika barabara ya Sakina
– Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha.
Awamu ya pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny Kalupale, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa
Kilimanjaro na Arusha ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na
Wizara yake.
COMMENTS