SERIKALI inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto...
SERIKALI inatarajia
kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi
kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika
Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na
watumishi wengine wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga,
alipofanya ziara ya kikazi kukagua namna Mamlaka hayo inavyokusanya kodi.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza na baadhi ya Viongozi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu kufanya juhudi ya
kukusanya mapato ili azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kikamilifu
itimie.
Ahadi hiyo imetolewa
Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa
akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati wa
ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.
Dk. Kijaji amesema
kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa
na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na
kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza na baadhi ya Viongozi
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu kufanya juhudi ya
kukusanya mapato ili azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kikamilifu
itimie.
“Tunatambua changamoto
ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana tumeamua
kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze
kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi
zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema .
Alisema kuwa pamoja na
uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya shilingi
trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa
kutumia wafanyakazi waliopo.
Dk. Kijaji alitoa rai
kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika kukiuka maadili
yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.
Awali Meneja wa
Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Jumbe Samson, alieleza kuwa mkoa wake
umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba wanauhakika wa
kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo
kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Kaimu
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Beatus Nchota alisema kuwa
Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila wilaya hapa nchini
ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato
ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17 liweze kufikiwa.
Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa
Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo itahakikisha kuwa TRA inatimiza
malengo yake ya kukusanya kodi na kumhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dk. Ashatu Kijaji kwamba watasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya
Serikali.
COMMENTS