MAMBA Wawili waliokwishaua watu wawili pamoja na mifugo kadhaa, wakiwemo ng’ombe na mbuzi, wameuawa na wananchi wa kijiji cha Igundu wilaya...
MAMBA Wawili waliokwishaua watu wawili pamoja
na mifugo kadhaa, wakiwemo ng’ombe na mbuzi, wameuawa na wananchi wa kijiji cha
Igundu wilayani Bunda, mkoa wa Mara, baada ya kutaka kukamata ng’ombe
waliokwenda kunywa maji katika ziwa Victoria.
Kaimu afisa mtendaji wa kata ya Igundu, Tekele
Muligawe juzi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lililotokea hivi karibuni
katika kisiwa cha Chugu kilichoko ndani ya ziwa Victoria wilayani Bunda.
Muligawe alisema kuwa mamba hao walikuwa ni
kero kubwa kwa wakazi wa kata hiyo, pamoja na kata za jirani, wanaokwenda
kufanya shughuli za kibinadamu katika ziwa hilo.
Alisema kuwa kwa kipindi kisichozidi miezi
miwili mamba hao walikuwa wamekwishaua watu wawili na ng’ombe watatu na
kujeruhi ng’ombe wengine kadhaa, huku baadhi ya watu wakinusurika kukamatwa na
mamba hao.
Alisema kuwa matukio hayo yalitokea wakati huu
wa kiangazi na kwamba tayari taarifa hiyo alikwishaiwasilisha katika ngazi ya
Wilaya hiyo.
“Kwa kipindi cha miezi isiyozidi miwili tayari
hao mamba wameshakamata na kuua watu wawili na ng’ombe watatu. Kwa ujumla wake
walikuwa ni kero, kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo” alisema.
Alisema kuwa siku ya tukio mamba hao walitaka
kukamata ng’ombe waliokuwa wamekwenda kunywa maji katika ziwa Victoria, hali
iliyosababisha wananchi kuanza msako na kufanikiwa kuwaua.
Alisema kuwa baada ya kufanikiwa kuwaua
walitoa nyongo zao na kuzitupa ndani ya shimo lefu la choo kwa ajili ya usalama
wa watu kwani hiyo ni sumu kali.
COMMENTS