WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na...
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini wasimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi.
Waziri mkuu Kassim Majaliwa |
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Ijumaa, Septemba 8,
2017 wakati akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini
Dodoma kujadili mbinu za kufufua zao hilo.
Wakuu wa mikoa walioitwa kwenye kikao hicho ni kutoka mikoa ya
Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na
Geita.
“Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni
pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku na leo nimetaka nianze na ninyi wakuu
wa mikoa ili mwende mkawasimamie watu wenu tunapokaribia kuanza msimu mpya,”
alisema.
Majaliwa alisema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia
maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta
masoko na akawataka wasimamie katika maeneo yao ili kilimo cha zao hilo kiweze
kubadilika.
“Kuna maafisa kilimo kwa kila Halmashauri iliyoko kwenye mikoa yenu.
Maafisa kilimo hawa lazima wahusike kikamilifu. Moja ya majukumu yake kwa cheo
chake, kazi kubwa aliyonayo ni kusimamia zao la pamba. Kama hajafanya kazi
hiyo, usiridhike kuwa na afisa kilimo wa aina hiyo,” alisema.
“Ni lazima kila mmoja awe na mpango kazi, ausimamie na atoe matokeo ya
kuwa zao hili limefanikiwa katika eneo lake. Tunataka zao hili lichukue nafasi
yake ya namba moja. Heshima ya “Dhahabu Nyeupe” lazima irudi lakini pia ni vema
mkumbuke kuwa zao la pamba ni uchumi, zao la pamba ni siasa katika mikoa yenu,”
alisisitiza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba; Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI; Suleiman Jafo, Makatibu Wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya
Kilimo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Tito Haule na Mkurugenzi Msaidizi
wa Uhamasishaji Mazao, Beatus Malema.
COMMENTS