SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC), limefanikiwa kukusanya madeni ya muda mrefu kutoka kwa taasisi za Serikali, mashirika ya umma na sekta bi...
SHIRIKA
la Posta Tanzania (TPC), limefanikiwa kukusanya madeni ya muda mrefu kutoka kwa
taasisi za Serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi kiasi cha shilingi
bilioni 7.6.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani katika kikao cha
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
Shirika hilo kilichofanyika mjini Dodoma ambapo amesema makusanyo hayo ni kati
ya jumla ya shilingi bilioni 12 ambazo Shirika hilo linadai wateja wake kuanzia
mwaka 2011 hadi mwezi Juni mwaka huu.
"Hakikisheni
mnamalizia makusanyo ya deni lililobaki, kwani Shirika linahitaji kuendelea na
kupata faida kupitia makusanyo haya”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Prof. Norman Sigala King ameiomba
Serikali kuliondoa Shirika hilo kwenye orodha ya mashirika yanayotaka
kubinafsishwa.
Ameongeza kuwa Serikali
ikitekeleza jambo hilo, italiwezesha Shirika hilo kujiendesha kibiashara,
kuzalisha faida na kukabiliana na changamoto za ushindani kwenye soko.
Pia, amelitaka Shirika hilo
kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi kwa kutumia Teknolojia
za kisasa zaidi badala ya kutumia mifumo ya kizamani.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo Luteni Kanali mstaafu Haruni Kondo, ameiomba
Kamati hiyo kuendelea kushirikiana na Shirika hilo na kulisaidia ili liweze
kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Taasisi za Serikali na
Mashirika ya Umma yanaendelea na utekelezaji wa agizo la Rais wa Awamu ya Tano
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha kuwa
yanajiendesha kwa faida, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudai madeni ya muda
mrefu ili fedha hizo ziweze kutumika kuwahudumia wananchi katika nyanja mbalimbali
kama vile za elimu, afya na ujenzi wa miundombinu.
COMMENTS