Habari Mpya

Friday, 1 September 2017



MKUU wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili, amemuagiza mkuu wa polisi (OCD) wilayani humo kumkamata na kumuhoji katibu wa mbunge wa jimbo la Bunda mjini Yohana Kahunya, kwa kile alichodai kuwa ni kumkashifu kwa kupitia mitandao ya kijamii, ili ikithibitika afikishwe mahakamani.
 
wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili
Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda alitoa agizo hilo juzi ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo wilayani hapa.

Bupilipili alisema kuwa katibu wa mbunge Esther Bulaya, hivi karibuni ameendelea kumshambulia  kwa kumchafua kupitia mitandao ya kijamii.

Alisema kuwa kwa jinsi hiyo ameamua kuchukua hatua ya kumwagiza mkuu wa jeshi la polisi katika Wilaya hiyo, kumkamata na kumhoji na kwamba iwapo ikithibitika afikishwe mahakamani kwa kosa la mtandao.

“Amenichafua sana kwenye mitandao ya kijamii hivyo ninamwagiza OCD, amkamte katibu huyo na ahojiwe na iwapo ikithibitika afikishwe mahakamani kujibu tuhuma hiyo kwa kushitakiwa kwa kosa la mtandao maana sheria tayari ipo inayokataza matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii” alisema.

Pia, alisema kuwa katibu huyo ahojiwe na polisi kuhusu kauli zake ambazo amekuwa akizitoa kwamba mawasiliano yake na polisi wilayani hapa, eti mbunge Bulaya pamoja na katibu huyo wamekuwa wakiyapata kwa haraka na mapema sana.

“Polisi wamhoji aseme taarifa hizo amekuwa akizipata wapi, na wao polisi wajitathmini kama wao ndio wanaotoa siri za serikali wakiwa watumishi wa umma na kama ikithibitika ni uongo achukuliwe hatua” alissistiza.

Na katika hatua nyingine Bupilipili, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wote, kwa kushiriki kikamilifu katika mbio za mwenge wa uhuru uliokimbizwa wilayani hapa hivi karibuni na kusema kuwa wameutendea haki hali ambayo imeonyesha umoja na mshikamano.

Alisema kuwa mwakani pia wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi na kuutendea haki mbenge wa uhuru, kwa kushiriki kikamilifu maana ukimbizwa ili kueneza ujumbe mahususi na maalumu kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vya siasa, wala dini au kabila


Alisema kuwa hali hiyo ni ya kizalendo nay a kumuenzi baba wa taifa mwalimu Julius Nyerere ambaye ndiye mwasisi wake.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -