MKE wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye sham...
MKE wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa
kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye shambulio hilo na
sababu za kufanya uovu huo.
Mke
huyo ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anasema kuwafahamu watu hao ni muhimu
kwa kuwa familia haijui kwa sasa watu hao wanatafakari na kupanga kitu gani
baada ya jaribio la kwanza la kumuua kushindikana.
Lissu,
mmoja wa wanasiasa wasio na hofu kusema lolote wanaloliamini, alishambuliwa na
watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa ndani ya gari lililokuwa limewasili kwenye
makazi yake Area D mjini Dodoma akitokea bungeni.
Tangu
wakati huo, wakili huyo wa kujitegemea na mwanasheria mkuu wa Chadema, amelazwa
Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hadi sasa Jeshi la Polisi halijaeleza kama
limeshapata fununu ya waliohusika zaidi ya kujibu kuwa linaendelea na upelelezi
kila waandishi wanapotaka kujua maendeleo ya suala hilo.
Na
sasa mke huyo wa Lissu na ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anataka kuwajua
waliomfyatulia mumewe zaidi ya risasi 30, aliyewatuma na sababu za kuwatuma.
Magabe
pia anasema familia yake kwa sasa ipo shakani kwa kuwa hajui hao waliofanya
shambulio hilo ambalo linaonekana la kukusudia kumuua, wanatafakari nini na
kupanga nini.
Akizungumza
na gazeti la Mwananchi katika Hospitali ya Nairobi, Wakili Magabe alisema Lissu
ametumia sehemu kubwa ya ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania,
hivyo angependa kuona haki inatendeka.
“Binafsi
nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba
nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.
“Sitaki
kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki
inatendeka.”
Alisema
tukio hilo limemfanya aanze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua Lissu,
lakini hawajafanikiwa na anaamini watu hao wapo, hivyo anahofia usalama wa
familia yake.
“Mpaka
sasa sijasikia kama kuna uchunguzi wowote umefanyika na sijawahi kusikia watu
wamekamatwa,” alisema Wakili Magabe.
“Hivyo
nawaza kuwa hayupo salama na mimi kama mke wake sijisikii kama niko salama
sana. Nawaza hawa watu watakuwa wanatafakari au wanapanga nini. Hiyo ndiyo hali
niliyonayo kwa sasa. Sijui hao watu wako wapi.”
Hata
hivyo, Magabe alisema Lissu yuko imara na shambulio hilo halijamrudisha nyuma
katika harakati zake za kupigania haki na za kisiasa.
Alisema
hilo alilionyesha mara tu alipopata fahamu.
“I
have survived to tell a tale, I have lived to tell a tale (nimeepuka kifo ili
nieleze jambo) ndivyo alivyosema baada ya kuzinduka,” alisema Wakili Magabe.
Alisema
baada ya fahamu kumrejea sawasawa amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria
kwamba ana ari zaidi.
“Spirit
yake ipo very high (ari yake iko juu sana). Si mtu wa kusema kuwa baada ya
tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua,” alisema wakili huyo.
“Sijawahi
kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma. Kama mke
nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani. Lakini wanapokuja
viongozi wenzake kutoka Tanzania; wastaafu na wa sasa na hata hapa Kenya, kauli
zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa.
“Anasema
‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na
wanaharakati.”
Kuhusu
mumewe kuendelea na siasa baada ya kupona, Wakili Magabe alisema Lissu ndiye
anaweza kulizungumzia suala hilo.
“Mimi
nikiwa msaidizi wake wa kwanza, nitakuwa mtu wa mwisho kusema Lissu asifanye
analotaka kwa kuwa hata akiyatamka hayatakuwa na nguvu mbele za Mungu,”
alisema.
“Binafsi
nasema alikuja duniani kwa makusudi. Mungu alimleta duniani kwa sababu na
alijua hata kabla hajazaliwa maisha yake yatakuwaje na atafanya nini hapa
duniani.
“Sidhani
kama kuna binadamu anaweza kuzuia yale ambayo Mungu amepanga. Sitaki kusema
kama ataendelea na siasa, hataendelea nazo, yupo kwa kusudi lake.”
Magabe
alisema kuna watu wanapigwa risasi moja na wanafariki dunia, lakini Lissu
alipigwa risasi 16 za moto ambazo zilipita kwenye mwili wake na anaendelea
kuishi.
Alisema
anafarijika kuona Lissu yu mzima kwa kutumia nguvu za watu wote ambao kwa namna
moja au nyingine wanapenda aishi, akianzia na waliochanga fedha,
waliomtolea
damu, walioomba, waliomnyanyua, waliomtibu mara ya kwanza na wanaoendelea
kumtibu.
“Hatujawahi
kuwa peke yetu na nimegundua kumbe kupigwa risasi kwa Lissu ni tukio ambalo
limewagusa Watanzania na mataifa mengi na wapo tayari kusaidia,” alisema
mwanamke huyo.
“Hii
ni kwa kuwa ametumia ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania.”
Magabe
alisema risasi zilizompata Lissu ziliharibu zaidi mifupa, tishu zilizo karibu
na mifupa ya mguu wa kulia na mikono, lakini hakuumia kwenye neva, mishipa mikubwa
ya damu, ya fahamu au ogani.
“Madaktari
wanasema risasi zilikuwa zinakwepa maeneo muhimu. Ni kitu ambacho hawajawahi
kukiona,” alisema.
“Hapa
kuna mshipa mkubwa wa damu, lakini risasi imepita pembeni. Walikuwa wanashangaa
inawezekana vipi risasi nyingi zikaingia lakini zikakwepa maeneo muhimu.”
Alisema
madaktari wamemweleza Lissu kuwa ataendelea kuimarika lakini itachukua muda
kabla hajapona na kuweza kutumia viungo vyake vyote kama kawaida.
Mama
huyo alisema awamu ya kwanza ilikuwa kumtibu majeraha na ya pili ni kumjengea
uwezo wa kutumia viungo vyake ili baadaye aweze kusimama na kurudi katika hali
yake.
Magabe
alisema ilichukua mwezi mmoja Lissu kutoka ICU na hakuweza kumhudumia kwa
ukaribu kutokana na masharti ya chumba cha uangalizi maalumu.
“Kila
siku naamka kama nakwenda kazini. Lazima niamke asubuhi kuja hospitali kisha
narudi usiku nyumbani. Siruhusiwi kulala hapa,” alisema.
Simulizi
ya siku ya tukio
Magabe
alisema siku ya shambulio alikuwa ametoka Kerege wilayani Bagamoyo na alipanga
kukutana na rafiki yake eneo la Mpiji, Bunju.
“Saa
6:30 nilifika kwake, akaniambia lazima nipate chakula cha mchana, baada ya
chakula nilimwambia nipumzike kwenye kochi,” alisema.
“Baada
ya dakika 25 akaniamsha akaniambia Alicia amka ukilala sana mchana huu usiku
unaweza usipate usingizi,” alisema.
Alipoamka
aliwasha simu zake na kukuta ujumbe usemao, “hello sister, kuna taarifa
inazunguka sina hakika kama ni ya kweli. Kama kweli pole sana dada yangu.”
Alisema
moja kwa moja wasiwasi ulimjia kwamba huenda mumewe amekutwa na jambo baya,
alisema alichowaza awali huenda amepata ajali na ndipo akamuomba rafiki yake
ampigie mtu huyo simu kujua zaidi kuhusu ujumbe huo.
“Niliingia
kwenye magroup ya Whatsapp ya Chadema nikakutana na hiyo taarifa. Nilipiga
kelele kwa nguvu, rafiki yangu aliniuliza umeona nini nikamwambia kuna ujumbe
huu,” anasema na kumpa rafiki huyo simu asome ujumbe huo uliosema “Tundu Lissu
amepigwa risasi.”
“Nilianza
kuwaza yupo hai au amekufa. Niliwaza nifanye nini nikamwambia nataka kwenda
nyumbani. Huko niliamini kuwa ningewaza kwa utulivu nini cha kufanya.”
Anasema
baadaye simu zilianza kuingia mfululizo na ndipo alipoamini kuwa habari hizo ni
za kweli.
“Nilimpa
jukumu hilo (la kupokea simu) kwa sababu ni rafiki yangu wa karibu tangu
sijaolewa,” alisema.
Baadaye
waliingia kwenye gari na yeye kuanza kuendesha huku rafikiye akizungumza na
waliokuwa wakimpigia simu.
Magabe
alisema baada ya kuiingia mtaa wa nyumbani kwake, aliona vijana wanamwangalia
katika namna ambayo ilionyesha kuna kitu wanakijua. “Mwonekano wao ulikuwa
tofauti wananiangalia kwa huruma, kwa mshangao. Wanatamani waongee,” alisema.
Anasema
nyumbani aliwakuta shemeji zake wawili na mtoto wa baba yake mdogo, lakini
alishindwa kuingia ndani na badala yake alikaa bustanini.
“Nilipigiwa
simu na watu waliokuwepo hospitali na wakaniambia ni kweli amepigwa risasi,
lakini yupo hai. Walinitaka nitulie mpaka nitakapopewa taarifa nini cha kufanya,”
alisema.
Alisema
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimweleza nini cha kufanya kwa wakati
huo.
Alisema
baadaye aliambiwa Lissu angepelekwa Nairobi na hivyo aende uwanja wa ndege kwa
ajili ya safari ya Dodoma na baadaye Nairobi.
Aliondoka
na kaka yake na marafiki wa karibu, lakini alipigiwa simu na kutakiwa kushuka
kwa kuwa muda haukuwa rafiki.
“Nilipanda
bodaboda,” alisema.
“Wale
vijana walikimbiza sana na ilikuwa ni mara ya kwanza kupanda pikipiki Dar es
Salaam. Niliogopa na kusali Mungu anisaidie kufika uwanja wa ndege salama.”
Alipofika
Dodoma ndipo alipomuona kwa mara ya kwanza Lissu tangu apate taarifa za
shambulio.
“Baada
ya dakika chache akaja akiwa kwenye kitanda kutoka chumba cha upasuaji. Kwa
kumuangalia nilijua ameumia sana hakuwa anajitambua,” alisema
COMMENTS