Habari Mpya

Tuesday, 28 November 2017

UONGOZI wa hospitali ya misheni Kaibara, iliyoko wilayani Bunda mkoani Mara, umetakiwa kubandika gharama za matibabu kwenye mbao za matangazo, ili kuondoa utata unaodaiwa kuwepo hospitalini hapo na kuleta manung’uniko kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma ya matibabu katika hospitali hiyo.
Mkuu wa wilaya ya BundaLydia Bupilipili,

Kauli hiyo ilitolewa jana na mkuu wa wilaya ya Bunda Lydia Bupilipili, wakati akizungumza na Radio Free Africa, kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Bupilipili alisema kuwa amekuwa akipata malalamiko mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wananchi, wakidai kwamba gharama za matibabu katika hospitali hiyo ziko juu na kwamba zimekuwa hazieleweki vizuri kwa sababu haziwekwi kwenye mbao za matangazo.

Kufuatia malalamiko hayo mkuu wa wilaya ya Bunda, aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kubandika kwenye mbao za matangazo gharama zote za matibabu ili kuondoa utata huo unaolalamikiwa na wananchi.

 “Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu hospitali ya Kibara, hasa kwenye gharama za matibabu. Sasa kupitia vyombo vya habari ninaagiza kuanzia sasa wawe wanabandika gharama za matangazo kwenye mbao za matangazo ili wananchi wazione” alisema.

Pia, alisema kuwa hospitali hiyo imekuwa ikipatiwa ruzuku na serikali, ili iendelee kutoa huduma za matibabu kwa wananchi pasipo gharama, kwa makundi maalumu wakiwemo wazee wanaotambuliwa.


Halikadhalika mkuu huyo wa wilaya ya Bunda, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kutoa lugha zisizofaa kwa wauguzi na madaktari, kwani wanawavunja moyo wa kutekeleza wajibu wao, huku akiwataka wataalamu hao kuwajibika ipasavyo  ikiwa ni pamoja na kuacha vitendo vya kuomba rushwa.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -