KUTOKANA na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kuendelea kutokea katika jamii yetu, katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mashirika na asa...
KUTOKANA na vitendo vya unyanyasaji wa
kijinsia kuendelea kutokea katika jamii yetu, katika maeneo mbalimbali hapa
nchini, mashirika na asasi mbalimbali, zikiwemo za serikali na binafsi zimekuwa
zikiendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuachana na vitendo hivyo
unavyovota ni vikinyama
Mwanamke mmoja akitoka shambani kulima huku akiwa amebeba mzigo mkubwa wa kuni, mtoto mgongoni na mwingine akiwa amemshikilia mkono. mume wake amemwachia kufanya kazi zote. Huo ni ukatili wa kijinsia |
Mbali na kutoa elimu hiyo pia asasi na
mashirika hayo yamekuwa yakitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanajamii madhara ya
ukatili huo, ikiwa ni pamoja na adhabu inayotolewa kwa mtu au kikundi chochote
kilichofanya ukatili wa kijinsi dhidhi ya mtu au watu furani.
Lakini pamoja na kutolewa kwa elimu ndani ya
jamii yetu baadhi ya watu wamekuwa na vichwa vigumu kuachana na vitendo hivyo
na badala yake kila kukicha wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo vya ukatili wa
kijinsia dhidi ya wananchi wenzao, wasiostahili adhabu hiyo.
Mara kwa mara vitendo vya ukatili wa kijinsia
vimekuwa vikisikika kutokea kwa wanawake, pamoja na watoto. Lakini pia kwa siku
za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu tunaambiwa baadhi ya
wanawake nao wameonekana kuwa wanyama kwa kufanyia ukatili wa kijinsia waume
zao.
Baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwafanyia
ukatili wa kijinsia wake zao, kwa sababu ya mfumo dume, kwa kuwapa kipigo
kikali, ukatili wa kingono na ukatili wa kila aina kwa kutumia mfumo huo dume.
Aidha, watoto nao wamekuwa wakifanyiwa vitendo
hivyo vya ukatili, vikiwemo vya kupigwa pindi wanapopatikana na makosa ambayo
hata adhabu yake ilitakiwa kuonywa tu, kwa mfano mtoto anapokomba mboga
chunguni ama kwa kusikia njaa ama vinginevyo, ama anapopoteza fedha alizopewa
kwa ajili ya kununua kitu furani dukani, utakuta mzazi au mlezi anampatia
adhabu kali ambayo haiendani kabisa na umri wake.
Wazazi au walezi wengine wamekuwa wakiwapatia
adhabu ya kuwafunga na kamba mikono watoto wao na kisha kuwachoma na
kuwasababishia majeraha mwilini.
Hali hiyo ya ukatili ndiyo inayoweza kumshinda
mtoto husika na kuamua kukimbilia mitaani, na kuzalisha mtoto wa mitaani ambaye
kwa namna nyingine maisha yanavyozidi kuwa magumu kwake hataimaye uamua
kujiingiza kwenye makundi ya kiuharifu na kasha kuiishia jela au kuuawa na
wananchi wanaojichukulia sheria mikononi pindi wanapomtuhumu kutenda kosa
lolote la kiuharifu.
Lakini pia wazazi ama walezi wengine wamekuwa
wakifanya ukatili kwa watoto, ambao ni wakuwanyima haki yao ya msingi ya kuwapatia
elimu, ambayo ingemsaidia katika maisha yake ya baadaye.
Ama wazazi na walezi wengine wamekuwa
wakiwatumikisha watoto wao ambao umri wao hasa unafaa kuwa shule kwa kazi
ambazo haziendani na umri wao, kwani baadhi yao uwatumikisha katika kazi za mashambani,
uwatumikisha katika kazi za uvuvi, uchungaji wa mifugo, kazi za migodini na
kazi nyingine hatarishi kwa maisha yao.
Kwa mfano mimi hainiingii akilini kumtumikisha
mtoto mwenye umri wa miaka saba katika kazi ya uvuvi, kwani ajali ya kuzama mtumbwi
ikitokea, kamwe mtoto huyo hawezi kujiokoa kwa sababu hajui hata kuogelea
kulingana na umri wake kuwa mdogo. Kwa jinsi hiyo hicho ni kitendo cha kumtoa
kama sadaka mtoto mwenye umri huo.
Pia baadhi ya wanaume wanawafanyia vitendo vya
ukatili wa kijinsia wake zao, kwani utakuta mwanaume kazi yake ni kukaa
vijiweni tu muda wote akipiga soga, kuanzia asubuhi hadi jioni. Na kazi ya
shambani au ya uzalishaji mali anamwachia mwanamke na watoto wake pekee.
Baadhi ya wanaume hao wamekuwa ama
wakikalia kulewa pombe tu na muda wa chakula unapowadia urejea nyumbani na
kudai chakula tena kwa sauti kubwa, ilihali hajui chakula hicho kimedhalishwa
kutoka wapi na hata hiyo mboga anayoitumia kulia hajui imenunuliwa na nani?
Lakini bila soni mwaume mtu mzima ujikalisha kwenye meza na kuanza kubugia
chakula hicho kana kwamba kakizalisha yeye.
Na kibaya zaidi anapokuta mwanamke hajaandaa
chakula, ugeuka kuwa mbogo na kuanza kumtolea matusi na kejeri na hata
kumshushia kipigo kikali kama kwamba ni mbwa mwizi.
Wakizungumza kwa nyakati na maeneo tofauti na
mwandishi wa makala hii, baadhi ya wanawake wilayani Bunda, Mara, walisikika
wakisema kuwa hata wakati wa mavuno, licha ya waume zao kutoshiriki kikamilifu
katika shughuli za kilimo hicho, waume zao wamekuwa wakinyang’anywa fedha zote
walizouza mazao yao na kupewa kamgao kidogo tu, nyingi zikichukuliwa na waume
zao na kwenda kufanyia mambo ya starehe ukiwemo unywaji wa pombe na vimwana
vingine vya pembeni maarufu nyumba ndogo.
Mashirika pamoja na asasi mbalimbali za hapa
nchini na hata nje ya nchi zimekuwa zikijitahidi sana kuhakikisha vitendo
hivyo vinakomeshwa ndani ya jamii yetu, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua
za kisheria wale wote wanaoendesha vitendo hivyo.
Nao baadhi ya kina mama wamekuwa wakiwafanyia
unyama usiovumiliwa watoto wao, tena wengine wakisikika wakisema si ni mwanganu
hata kama ni kimuua. Labda hapa niwakumbushe akinamama wa aina hiyo kwamba
mtoto ukisha mzaa ni wa serikali, iwapo ukimfanyia ukatili wa aina yoyote
sheria itachukuliwa dhidi yako bila kujali kwamba wewe ndiye uliyemzaa.
Kutokana na elimu inayotolewa na mashirika,
pamoja na asasi hizo, hivi karibuni serikali wilayani Bunda mkoani Mara,
ililipongeza shirika lisilokuwa la kiserikali la Zinduka lililoko wilayani
humo, linalofadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society, kwa
kuwapatia wananchi elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ili vitendo
hivyo viweze kukomeshwa ndani ya jamii.
Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa wilaya ya
Bunda, Lydia Bupilipili, aliyewakilishwa na katibu tarafa cha Nansimo, Jonas
Nyaoja, kwenye mafunzo ya kupinga vitendo hivyo.
Mafunzo hayo ambayo yalikuwa ni mwendelezo wa
mafunzo mengine ambayo yamekwishafanyika, yalifanyika katika ukumbi wa kituo
cha walimu katika mji mdogo wa Kibara, uliko katika makao makuu ya jimbo la
Mwiabara.
Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda alisema kuwa
serikali wilayani hapa inatambua mchango mkubwa wa shirika hilo katika kutoa
elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili jamii iweze kupata uelewa na
kuachana na vitendo hivyo.
“Serikali
wilayani Bunda inatambua mchango mkubwa unaaotolewa na shirika hili la Zinduka
katika kutoa elimu kwa jamii juu ya ukiukwaji haki na unyanyasaji wa kijinsia.
Sasa elimu hii wananchi wetu wakiipata itawasaidia kubadilika na kuacha vitendo
hivyo” alisema Nyaoja kwa niaba ya DC Bupilipili.
Aidha, baadhi ya wadau mbalimbali wanaopinga
vitendo hivyo wilayani hapa, pia wamelishukuru shirika hilo kwa kuwapatia
mafunzo hayo kwa sababu vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekithiri sana ndani
ya jamii yetu, ukiwemo ukatili wa kiuchumi pamoja na ule wa tendo la ndoa.
Wadau hao ambao ni pamoja na wazee wa mila,
wazee maarufu, viongozi wa madhehebu ya dini, vyama vya siasa, watendaji wa
vijiji na kata, pamoja na wenyeviti wa vijiji, walisema kuwa Shirika la Zinduka
limejikita sanan katika kutoa elimu hiyo kwa jamii.
Waliyaomba mashairika mengine kuiga mfano huo,
kwani wananchi wengi wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo kwa sababu ya kukosa
uelewa na kwamba ni shirika la kwanza kufika mkatika maeneo yao na kuwapatia
elimu hiyo.
Walisema kuwa ukatili mwingine ni ubakaji wa
wanawake, utumikishaji wa watoto wadogo kwenye shughuli hatarishi ambazo
haziendani na umri wao, ukatili wa kutokupeleka watoto shule hususani wa kike,
pamoja na unyanyasaji wanawake na wanaume ndani na hata nje ya ndoa.
Waliongeza kuwa ukatili mwingine ufanywa na
wanaume kuachia shughuli za kilimo na uzalishaji mali wanawake tu, huku wanaume
wengi wakikalia ulevi na uzululaji, ambapo nyakati za chakula ufika majumbani
mwao na kudai chakula tena kwa kuamrisha, ambapo wanawake wanaposema hakuna
chakula uambulia kichapo au matusi ya uzalilishaji.
Walisema kuwa wamridhika na mafunzo hayo
ambayo yamewapatia mwanga, ambapo wataisambaza elimu hiyo katika maeneo yao ili
jamii iweze kubadilika.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika
la Zinduka, mhasibu wa shirika hilo, Godfrey Anatory, alisema kuwa wanatoa
mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika kata tisa za jimbo la
Mwibara na kwamba katika awamu ya kwanza walitoa mafunzo hayo katika kata 13 za
majimbo ya Bunda na Bunda mjini.
“Mafunzo haya tunayaendesha kwa kata tisa za
jimbo la Mwibara, lakini pia mafunzo kama haya tulikwishayaendesha katika kata
13 za majimbo ya Bunda na Bunda mjini. Na baadaye tuendesha mafunzo haya kwa
viongozi mbalimbali wakiwemo maasikari polisi, mahakimu na wanasheria, ili
jamii iweze kujua athari za ukatili wa kijinsia na adhabu yake” alisema.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dk. Stanely
Maendeka, alisema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kupata uelewa sahihi wa dhana
za kijinsia na dhana ya ukatili wa kijinsia, na kupata uelewa na uwezo wa
kutetea na kukomesha ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Dk. Mahendeka aliyataja maelengo mengine kuwa
ni pamoja kurekebisha mapendekezo ya awali ya mradi, ili ibebe shughuli
zinazogusa kukomesha ukatili wa kijinsia, kurekebisha bajeti iweze kuingiza au
kuchukuwa shughuli zilizopendekezwa, kukomesha ukatili wa kijinsia na kuweza
kutekeleza mradi vizuri zaidi na kupata matokeo yaliyotarajiwa.
Mkurugenzi wa shirika la Zinduka Maximillian
Madoro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo na elimu
mara kwa mara kwa jamii, ili kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsi katika
wilaya ya Bunda, mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla vitokomezwa.
Madoro amesema kuwa kupitia elimu hiyo kwa
kiasi furani jamii imekwisha badilika na kuachana na vitendo hivyo ingawa bado
kuna changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika baadhi ya wanajamii na
kwamba pamoja na changamoto hizo wanaendelea kutoa elimu hiyo ili kufikia
malengo yao ambayo kikubwa ni kutokomeza vitendo hivyo.
Kwa kumalizia makala yangu napenda
kuwakumbusha wananchi wote kwamba tushirikiane na serikali pamoja na mashirika
kama haya ya Zinduka, kupinga vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, kwani pia
vinavunja haki za msingi za binadamu.
Wote kwa pamoja tukipiga kelele na
kukemea vitendo hivi, ikiwa ni pamoja na kuwafichua ama kuwataja bayana wale
wote wanaoendesha vitendo hivi, vikiwemo na vile vya kukata watu wenye ualbino
viungo vyao na kukata mapanga na kuwaua wazee wenye macho mekundu eti kwa imani
ya ushirikina, hakika vita hii tutaishinda. Na kuwa na jamii iliyostarabika.
Pia tutowe ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi
na usalama, pindi tunaposhuhudia matukio kama hayo ndani ya jamii yetu, basi
tuwe mstari wa mbele kutoa ushahidi mahakamani ili mhusika au wahusika waweze
kuchukuliwa hatua na kuhukumiwa adhabu anayostahili kulingana kosa lake
alilotenda kwa mjibu wa sheria za nchi yetu.
COMMENTS