WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atahakikisha anafuatilia kwa kina ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya maji ili kuhakikisha ka...
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atahakikisha anafuatilia kwa
kina ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya maji ili kuhakikisha kama
inalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa katika kugharamia miradi
hiyo.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Julai 31, 2017)
alipozungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya akiwa katika ziara yake
ya kikazi mkoani Mbeya.
Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo,
inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na
salama. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 imetenga sh. bilioni 237.8
kugharamia miradi ya maji nchini.
Alisema
atafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa ujenzi wa miradi yote ya maji nchini ili
kuhakikisha malengo ya kampeni hiyo ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji
safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao
yanatimia.
“Nitafuatilia
katika maeneo yote nchini ili kujua kama kiasi cha fedha kilichotolewa kwa
ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maji iwapo kinalingana na thamani
halisi ya miradi husika. Lengo ni kuhakikisha kwamba thamani ya miradi yote
inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.”
Alisema
katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni
10.383 kwa ajili ya utekelezaji miradi ya maji, ambapo kati yake sh.
bilioni 1.693 zinatarajiwa kutumika kwenye Halmashauri ya Jiji la Mbeya huku
sh. milioni 622.049 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maji ya Halmashauri ya
wilaya ya Mbeya.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi
umuhimu wa kuzingatia sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za
kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya
mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuendelea kutekeleza kwa
vitendo kauli ya Rais Dkt. Magufuli ya Hapa Kazi Tu kwa kufanya kazi kwa bidi
ili kuweza kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Majaliwa alitoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa jimbo la Mbeya
Mjini, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi kumuomba Serikali iruhusu mikutano ya hadhara
kwa ajili ya viongozi wa vyama vya siasa, ambapo alimweleza kwamba hakuna
kiongozi aliyezuiwa kufanya mikutano katika eneo lake la kiutawala.
COMMENTS