Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kukopesha wakulima wa mazao ya ufuta na mihogo i...
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ameiomba Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kukopesha wakulima wa mazao ya ufuta na
mihogo ili waweze kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara hasa kwa wakulima
wadogo wadogo wa mkoani humo.
Zambi alitoa wito huo wakati wa mkutano wa Wadau wa
Korosho na Ufuta Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Zambi alisema kuwa mkoa wa Lindi ni mkoa
uliojaaliwa katika kuzalisha mazao ya ufuta na mihogo lakini changamoto kubwa
ni mtaji wa kulima kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya
nchi.
“Wakulima wa mkoa wa Lindi wapo tayari kushiriki
katika kuleta mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha
kibiashara lakini kwa sasa suala la mtaji wa kilimo cha kibiashara ni
changamoto kubwa,” alisema Zambi.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Lindi alisema kuwa ili
kuwezesha wakulima hao kulima kibiashara Benki ya Kilimo ina wajibu wa kutoa
mikopo yenye riba nafuu ili kuhamasisha wakulima hao wa mkoa wa Lindi waweze
kuongeza uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini
mkoani humo.
Aliongeza kuwa kama TADB itaboresha upatikanaji wa
mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa riba nafuu
zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko kutawezesha wakulima wa
Tanzania kufikia uchumi wa kati kama ilivyolengwa na Serikali ifikapo mwaka
2015.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis
Assenga alisema kuwa Benki ya kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa wakulima
wadogo wadogo waliokuwa kwenye vikundi ili waweze kukopeshwa.
Assenga aliongeza kuwa Benki ya Kilimo pia ipo
tayari kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa kuipatia mikopo yenye
riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko.
“Kwa kutambua umuhimu wa wakulima wadogo wadogo
nchini TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa
katika kuleta Mapinduzi yenye tija
katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa
ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa Benki yake
inaandaa mfumo mahususi wa uratibu kwa kushirikiana na halmashauri za mikoa ili
kuhakikisha kuna upatikanaji wa fedha kwa ajili ya minyororo ya ongezeko la
thamani kwa mazao ya Kilimo nchini.
“Tupo tayari kusaidia uzalishaji kwenye hatua mbali
mbali za uongezaji wa thamani, hadi masoko ya bidhaa za mwisho hadi kumfikia mlaji na kusaidia kuwaunganisha
wakulima na masoko kupitia halmashauri zao,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa
TADB, Augustino Chacha alisema kuwa TADB inalenga kuongeza upatikanaji wa
huduma zisizo za kifedha kwa wakulima kama vile kujengewa uwezo juu ya uandaaji
wa andiko la miradi ya Kilimo, pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko,
usimamizi wa biashara, mafunzo juu ya miradi ya Kilimo na mbinu za majadiliano
ya mikataba.
“Tupo tayari
kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali
kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya
umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo,” alisema.
Chacha aliongeza kuwa kwa upande wa mikoa ya kusini
Benki ya Kilimo imejipanga kueendeleza miundombinu ya umwagiliaji na maghala
pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo na kuimarisha
viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta, mihogo.
Chacha aliongeza kuwa Benki imejipanga kuwezesha
uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya mihogo, korosho na ufuta mkoani
Lindi.
COMMENTS