https://lenzimedia.blogspot.com/2017/08/mpango-wa-equip-wainua-kiwango-cha-elimu.html KATIKA kuinua kiwango cha elimu kwa shule za msingi a...
https://lenzimedia.blogspot.com/2017/08/mpango-wa-equip-wainua-kiwango-cha-elimu.htmlKATIKA kuinua kiwango cha elimu kwa shule za msingi ambazo
zilikuwa hazifanyi vizuri kitaaluma, serika liiliamua kuanzisha mpango wa
kuinua ubora wa elimu Tanzania (Equip) katika shule hizo ambapo halmashauri ya
mji wa Bunda iliyoko katika mkoa wa Mara, ni kati ya halmashauri ambazo
zinatekeleza mpango huu.
Halmashauri hiyo yenye shule za msingi za serikali ziapatazo
61 na shule binafsi zipatazo tano, zinatekeleza mpango huo lengo likiwa
ni kuhakikisha kiwango cha elimu katika shule hizo kinaboreka.
Mpango huu wa kuinua ubara wa elimu Tanzania una
malengo mengi yakiwemo ya kuinua ubora wa elimu na taaluma kwa ujumla, ikiwa ni
pamoja na kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.
Katika shule za halmashauri ya mji wa Bunda, tangu
mpango huo ulivyoanza kutolewa mwaka 2015 tayari mafanikio mengi yamekwishaanza
kupatikana na kuleta matokeo chanya ya kielimu, hali ambayo imeleta faraja
kubwa kwa wazazi, walezi, wanafunzi, walimu, pamoja na wadau mbalimbali wa
elimu katika halmashauri hiyo.
Mpango huu mbali na kuinua kiwango cha taaluma katika shule
hizo, pia umewezesha wanafunzi kufanya kazi za kujitegemea pindi wawapo shuleni
na hata majumbani mwao, kwa kulima kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula,
pamoja na bustani za mboga na matunda.
Chakula wanachozalisha wanafunzi hao kwa kutumia nguvu zao
wenyewe pamoja na mboga na matunda hayo wamekuwa wakiyatumia wakati wakiwa
shuleni, pamoja na nyumbani kwao kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha afya zao.
Shule tatu za halmashauri ya mji wa Bunda, ambazo ni pamoja
na shule ya msingi Mazoezi, iliyoko katika chuo cha ualimu Bunda, shule ya
msingi Ushashi na shule ya msingi Mugaja, ambayo ni shule mama ya shule mpya ya
Mbugani ni kati ya shule zilizoko katika mpango huo na tayari zimekwishayapata
mafanikio makubwa, ya kuchumi, kiafya na kitaaluma.
Bonji Emmanuel Bugeni ni afisa maendeleo ya jamii katika
halmashauri ya mji huo, anaelezea kuwau mpango huo, ambapo kikubwa ni kuinua
kiwango cha elimu katika shule hizo pamoja na kuanzisha miradi ambayo
itaziwezesha shule husika kutatua changamoto mbalimbali kupitia njia ya
kujitegemea, ikiwa ni pamoja na kuwapatia chakula wanafunzi.
Anasema kuwa kupitia mpango huo shule ya msingi Ushashi kwa
sasa wanao mradi wao wa kilimo cha mazao ya chakula, ambao umewasaidia watoto
kupata chakula pindi wawapo shuleni hapo.
Aliongeza kuwa pia afya za watoto wanaosoma katika shule
hizo kutokana na lishe bora wanayopata zimeboreka kwa kiasi kikubwa na kwamba
pia hali ya utoro kwa wanafunzi umepungua sana na sasa watoto wanaipenda elimu.
Alibainisha kuwa hali ya ufundishaji kwa walimu pia
imeboleka sana kwani walimu wamepata mori na hali na bidii katika kuwafundisha
wanafunzi imeongezeka kwa kiwango kikubwa na walimu wanaonesha kuipenda kazi
yao.
Aidha, anasema kuwa pia shule ya msingi Mazoezi nayo inao
mradi wa kilimo cha Bustani ya mboga na matunda, mradi ambao pia umeshirikisha
wazazi, walimu na wanafunzi, ambapo pia wanafunzi wamekuwa wakipatiwa mboga na
kwenda nazo nyumbani kwao kwa ajili ya kuboresha afya zao na za wazazi wao pia.
“Wanafunzi pia wamekuwa wakipewa mboga kwa zamu zamu na
kwenda nazo majumbani kwao, kwa ya kuzitumia pamoja na wazazi wao hapo
nyumbani” alisema Bonji Emmanuel Bugeni afisa maendeleo ya jamii wa halmashauri
ya Mji huo.
Anasema kuwa kuna shule mpya ya Mbugani ambayo ilianzishwa
kwa malengo mahususi likiwemo la kuokoa maisha ya watoto waliokuwa wanatembea
umbali mrefu na kuvuka barabara kuu ya Mwanza-Musoma ambapo baadhi yao walikuwa
wakigongwa na vyombo vya moto pindi wanapovuka katika barabara hiyo ya lami.
Anasema kuwa mpango huo ndio uliosababishwa kuanzishwa kwa
shule hiyo, ambapo wazazi, kamati ya shule, walimu na wananchi kwa ujumla
waliweka mikakati kadhaa ya kujenga shule hiyo kwa kutumia nguvu zao.
“Huu mradi ni mkombozi katika suala zima la elimu na lishe
kwa wanafunzi wetu, pamoja na maisha yao. Kulikuwa na changamoto nyingine ya
wanafunzi kugongwa na vyombo vya moto wakati wakivuka barabara kuu ya
Mwanza-Musoma wakati wa kwenda na kutoka shuleni.
“Hali hiyo iliwafanya wazazi, kamati ya shule pamoja na
walimu kwa ujumla kukaa na kuanzisha wazo la kujenga shule nyingine ya Mbugani.
Lakini pia hali hiyo iliasaidia kuondoa msongamano wa wanafunzi katika shule
mama ya Mugaja” alisema Bonji Bugeni.
Halikadhalika afisa maendeleo huyo wa jamii alielezea
changamoto zinazowakabili, ikiwemo ya kutokuwa na vyombo vya usafiri kutokana na
halmashauri hiyo kuwa changa.
Lakini pia pamoja na maendeleo hayo aliwataka wazazi na
walezi kuwa karibu zaidi na walimu kwani ni walezi wazuri wa watoto wao, kwa
sababu muda mwingi wao ndio wanaokaa na watoto pindi wawapo shuleni kwao.
Alisema kuwa wazazi wanapokuwa karibu na walimu ikiwa ni
pamoja na kufuatilia masomo ya watoto wao pamoja na mienendo yao, itawafanya
walimu nao kuwa karibu na wazazi na wote kwa pamoja kuhakikisha wanafunzi
wanapata elimu na maarifa yanayotakiwa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Naye afisa elimu vielelezo katika halmashauri ya mji huo
Christina Lubaka, alisema kuwa mpango huo umeleta mafanikio makubwa katika
shule hizo, ambapo anatoa mfano wa shule ya msingi Mazoezi ambayo imekuwa
ikitekeleza miradi mingi ya kiuchumi.
“Kwa mfano wa shule moja tu ya Mazoezi ambayo iko kwenye
chuo cha ualimu Bunda, imekuwa ikifanya vizuri katika miradi mbalimbali ya
kuchumi, ambapo bidhaa wanazozalisha mashambani baadhi imekuwa ikiuzwa na
kupata mahitaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kununua chaki” alisema Christina
Lubaka afisa elimu vielelezo halmashauri ya mji wa Bunda.
Kaimu afisa elimu wa halmashauri ya mji wa Bunda, Undi
Tanga, anathibitisha kuwepo kwa maendeleo makubwa ya kiucumi, kielimu na
kitaaluma kwa ujumla katika shule hizo zote 66 za msingi katika halmashauri
hiyo tangu mpango huo uanze kutekelezwa.
Tanga anasema kuwa kutokana na mpango huo ulioanzishwa mwaka
2015, kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu katika mikoa iliyofanya vibaya hapa
Tanzania, ukiwemo na mkoa wa Mara, umesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua taaluma
katika shule hizo, ikiwa ni pamoja na kupunguza hali ya utoro kwa wanafunzi.
Alisema kuwa kwa jinsi hiyo utaona kwamba kuna mafanikio
mengi sana yaliyotokana na mpango huu.
Alifafanua kuwa mpango huo wa kuinua ubora wa elimu Tanzania
ulianzishwa na serikali katika mikoa ambayo ilionekana kufanya vibaya kielimu
na kwamba halmashauri ya Mji huo nayo iliingizwa katika mpango huo ambao lengo
lake kubwa ni kuhakikisha kiwango cha ubora wa elimu unakuwa juu.
Tanga alisema kuwa pamoja na kuboresha afya za wanafunzi
kupitia miradi ya kilimo cha vyakula, matunda na mboga, lakioni pia kiwango cha
taaluma kipanda kwa asilimia kubwa, sanjari na utoro kupungua, ambapo kabla ya
mradi mahudhuri kwa wanafunzi katika shule hizo yalikuwa ni wastani wa asilimia
62 tu, lakini kwa sasa ni zaidi ya asilimia 90.
“Tangu mpango huu ulipoanza kutekelezwa katika shule za
halmashauri yetu kwa ujumla tumekwishapata mafanikio mengi sana kwa ujumla.
Mafano utoro umepungua sana katika shule zetu, maana kabla
ya mradi huu mahudhurio shuleni kwa wanafunzi yalikuwa ni wastani wa asilimia
62, lakini kwa sasa ni zaidi ya asilimia 90” alisema.
Anasema kuwa kabla ya kuanza kutekelezwa mpango huo katika
shule zote kwanza ulianza uhamasishaji kwa wazazi, walimu, kamati za shule na
wadau mbalimbali wa maendeleo, lengo likiwa nikutaka kufikia malengo
yaliyotarajiwa.
Alisema kuwa pia walimu walipatiwa mafunzo ya masomo
mbalimbali yakiwemo yale ya KKK yaani kujua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu,
ambapo pia kamati za shule zilipatiwa mafunzo rasmi ili ziweze kupata uelewa
kuboresha elimu katika shule zao.
Aliongeza pia katika kufikia malengo hayo vilabu mbalimbali
vya wanafunzi, hususani vya kuhusu afya, elimu ya kutigemea na mambo kadha wa
kadha vilianzishwa katika shule hizo, ambapo kupitia vilabu hivyo wanafunzi
walifundishwa mambo mbalimbali ya kuwajengea uwezo wa kiakili na kimaarifa.
Kufuatia maendeleo hayo Tanga anatoa wito kwa wazazi, kamati
za shule na walimu wote kwa pamoja kushirikiana ili kuinua kiwango cha elimu
katika shule hizo, kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha.
Nao baadhi ya walimu wa shule za msingi katika halmashauri
ya mji wa Bunda, walielezea furaha yao kuhusu mpango huo, pamoja na kuelezea
mafanikio ambayo wamekwishayapata kwamba ni mengi sana, ikiwa ni pamoja na
kuweka mikakati kadhaa ambayo imewasaidia kuinua kiwango cha elimu katika shule
zao.
Mwalimu Madaraka Rusarika ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi
Ushashi, ambaye anabainisha wazi kwamba kwa ujumla mpango huo umewaletea
maendeleo mengi sana katika shule yao, huku akiishukuru serikali kwa ubunifu
huo.
Lakini pamoja na mafanikio hayo mwalimu huyo anasema kuwa
kuna changamoto kadhaa ambazo inabidi zifanyiwe kazi, ikiwemo ya baadhi ya
wananchi kuingilia mipaka na shule na kuendesha shughuli za kibinadamu, ambapo
anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuingilia mipaka ya shule.
Nao baadhi ya wazazi wanaelezea mikakati waliyoifanya kwa
ushirikiano wa walimu kwa pamoja na kufikia mafanikio ambayo wanayo kwa
sasa katika kuboresha elimu katika shule hizo.
Joseph Mtara ni mwenyekiti wa kamati ya shule Ushashi na
Wasato Nyamsha ni mzazi na mjumbe wa kamati ya shule hiyo ambao wanasema kuwa
umoja wao kati ya kamati ya shule, wazazi na walimu kwa ujumla ndicho chanzo
cha mpango huo kufikia malengo yake ya kuinua ubora wa elimu katika shule hiyo
ya Ushashi.
Katika shule ya msingi Mazoezi, ambayo pia ni kati ya shule
zinazonufaika na mpango huo, mwalimu mkuu wa shule hiyo Vicent Ndunguru,
anaelezea mradi wao wa bustani jinsi unavyowasaidia katika shule hiyo,
ambapo pia anatoa pongezi kwa serikali kwa kutoa elimu bure.
Baadhi ya wazazi waliozungumza na mwandishi wa makala hii
wanaendelea kuelezea kuhusu ushirikiano wao na walimu kupitia umoja wao wa unaojulikana
kwa jina UWW, kwamba ndicho chanzo kikuu cha mafanikio na kwamba kupitia mpango
huo majumbani mwao pia wana miradi hiyo ya kilimo cha mboga na matunda kwa
ajili ya kuboresha afya zao.
“Kupitia mpango huu wa Equip hata sisi umetusaidia sana tukiwa
kama wazazi, maana tumeanzisha bustani za mboga na matunda ambayo kwa sasa
utusaidia kuboreesha afya zetu maana tunapata lishe bora sisi na watoto
wetu” alisema Lugembe Lugembe, ambaye ni mratibu wa ushirikiano (UWW) shule ya
msingi Mazoezi.
Mwandishi wa makala hii alipata fursa ya kutembelea shule ya
msingi Mugaja na kuzungumza na mwalimu mkuu wa shule hiyo Mwaliki Biseko,
ambaye anaelezea changamoto zilizokuwa zinawakabili kabla ya mpango huo kuanza
kutekelezwa shuleni hapo, kwamba zilikuwa nyingi, ikiwa ni pamoja na utoro na
matokeo kutokuwa ya kuridhisha, ambapo kwa sasa hali imebadilika kwa kiasi
kikubwa kwani m afanikio ni mengi sana.
Naye Daudi Masalu ni mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi
Mugaja pamoja na baaadhi ya wazazi wengine wao pia wanaelezea mikakati hiyo
ikiwemo ya kuanzisha shule nyingine mpya ili kukabiliana na changamoto
mbalimbali, ikiwemo ya kujenga shule mpya ya Mbugani.
Katika hatua nyingine mtoto Nacy January, aliyepata ajali
wakati akivuka barabara akiwa anakwenda shuleni, pamoja na mama yake mzazi
Joyce Willison, walielezea changamoto iliyokuwepo kwam kutokuwa na shule katika
eneo hilo, ambapo kwa sasa motto huyo anasoma katika hiyo shule mpya tena kwa
ukaribu zaidi.
Hata hivyo mama yake anaiomba serikali kuendelea kuiboresha
shule ya msingi mbugani, ili iweze kupata mahitaji yote kwa kuongeza vyumba vya
madarasa, nyumba za walimu na miundombinu nyingine mbalimbali.
“Nilipata ajali nikagongwa na bodaboda wakati nikivuka barabara
ya lami kwenda shuleni lakini nilikaa nyumbani nikitibiwa lakini sasa nashukuru
Mungu nilipona na sasa naendelea na masomo yangu katika hii shule.
Nashukuru sana serikali kuleta mpango huu ni mkombozi kwa
sisi wanafunzi” alisema Nacy aliyegongwa na bodaboda akiwa darasa la pili mwaka
2013 ambapo hali hiyo ilisababisha baada ya kupona arudi nyuma darasa moja
ambapo sasa katika shule hiyo mpya.
Kwa ujumla serikali imekuwa na mipango kadhaa ya kuhakikisha
watoto wanapata elimu inayostahili ambayo itawasaidia katika masiaha yao ya
baadaye, ukiwemo mpango huu wa Equip ambao lengo lake ni kuinua ubora wa elimu
kwa shule ambazo zilionekana kufanya vibaya kitaaluma
Hivyo ni jukumu la kila mdau wa elimu kuiunga mkono serikali
katika mpango huu, wa kuinua ubora wa elimu Tanzania, kwa kutoa ushirikiano wa
kutosha kwa walimu na kuwahamasisha wazazi wengine kupeleka watoto wao shule
ikiwa ni pamoja na kuwahimiza wanafunzi kuhudhuria shuleni bila kutoraka.
Na Ahmed Makongo,
Bunda
COMMENTS