Serikali imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipati...
Serikali imesema kuwa imetumia
shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili
kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)
kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.
“Mfuko huu unaendelea
kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan
vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo Takwimu
zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano
yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939 kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”,
amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Ameongeza kuwa tayari
Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti mwaka
huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine 75 na vijiji
154.
Pia, ametanabaisha kuwa
hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini na
kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya Halotel
imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu
walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia
kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Kwa upande wake, Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso,
amezitaka kampuni za simu za mkononi zinazopeleka mawasiliano vijijini na
maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na Serikali kuhakikisha
kuwa zinatoa taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo hatua zilizofikiwa za ujenzi na
usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji husika.
Amewataka UCSAF kujitangaza na kuweka mabango
yao kwenye minara yote nchini iliyojengwa kupitia ruzuku ya Serikali ili kuwawezesha
wananchi kutambua uwajibikaji wa Serikali katika kufikisha mawasiliano kwa
wananchi wake.
Naye, Naibu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng.
Angelina Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF itahakikisha kuwa kila
mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na jukumu la msingi la Mfuko huo la
kufikisha mawasiliano kwa wote.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko
huo Eng. Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu
ya Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi zilizofanywa na kampuni za simu za mkononi za
ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji mbalimbali
nchini.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
COMMENTS