Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewaasa wakulima wa korosho nchini kuongeza uzalishaji wa korosho ili kuchangamkia fursa za m...
Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB) imewaasa wakulima wa korosho nchini kuongeza uzalishaji
wa korosho ili kuchangamkia fursa za masoko ya zao hilo linalohitajika zaidi
katika masoko ya Marekani, Vietnam na India.
Wito huo umetolewa jana
na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akifungua
Warsha ya Siku ya Wadau wa Vyama vya Ushirika inayoendelea katika Ukumbi wa
Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.
Assenga alisema kuwa
mahitaji ya korosho ni makubwa sana katika soko la dunia hivyo wakulima wa zao
hilo hawana budi kujizatiti ili kuhakikisha wanazalisha kiasi kikubwa cha
korosho ili kufikia au kuzidi malengo ya mavuno kwa msimu ujao ambayo
yanakadiriwa kufikia kati ya tani laki tatu (3) hadi laki nne (4) ukilinganisha
na takribani tani laki mbili na nusu kwa msimu uliopita.
Assenga alisema kuwa
korosho ni zao la kimkakati ambalo likiwekezwa kwa usahihi linaweza kunyanyua
uchumi na kipato kwa wakulima wa mikoa ya kusini na pwani ambao niyo ni
wazalishaji wakuu wa zao hilo.
“Nawaasa mujitahidi
kulima kisasa ili kuweza kufikia au kuvuka malengo ya mavuno ya msimu huu hali
itakayowaongezea kipato hivyo kufikia malengo ya serikali ya kuwanyanyua
wakulima nchini,” alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa
TADB aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kusaidia mfumo wa Stakabadhi ya
maghala ili kuhakikisha kuwa malengo ya mavuno ya korosho kwa msimu huu
yanafikiwa.
“TADB iko tayari
kuratibu mfumo wa malipo ya fedha zitokanazo na mauzo ya korosho kwa njia ya
TEHAMA, pia kwa kushiriakiana na soko la mazao (TMX), kusimamia ununuzi wa
mazao kwa njia ya mtandao (electronic auction),” aliongeza
Aliongeza kuwa Benki ipo
tayari kusimamia uuzaji wa mazao kwa mifumo ya salama ya kimataifa ya malipo
kama vile dhamana ya malipo.
Naye Mkurugenzi wa
Biashara wa Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema kuwa Benki ya Kilimo
ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji
na maghala na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo.
Aliongeza kuwa TADB pia
ipo tayari kuviwezesha viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na
kusindika ufuta, mihogo pamoja na uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya
korosho na ufuta.
“Tupo tayari kutoa
mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali kupitia
mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya umwagiliaji
na ununuzi wa zana za kilimo (kama matrekta, pump),” alisema.
Chacha aliongeza
kuwa kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazao ya kilimo, Benki ya Kilimo ipo
tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kujenga maghala mapya au kuboresha yaliyopo
pamoja na kununua mizani ya kisasa na ununuzi wa magari ya usafirishaji mazao.
Akizungumzia nafasi ya
taasisi za kifedha katika kudhibiti upotevu wa mapato kwa wakulima, Mkuu wa
Kilimo na Fedha Vijijini wa Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha (FSDT), Bw. Mwombeki
Baregu alisema taasisi na mitandao ya simu nchini zina wajibu wa kubuni
teknolojia rafiki wa wakulima itakayosaidia kudhibiti utapeli na wizi wa fedha
za wakulima.
Baregu alisema
teknolojia duni na ukosefu wa elimu sahihi juu ya matumizi na uhifadhi wa fedha
umepelekea wakulima wengi nchini kupoteza mapato yao kwa kushindwa kufahamu
uwekezaji sahihi wa fedha hizo.
“Naziomba taasisi za
kifedha na mitandao ya simu za mkononi kuwasaidia wakulima katika kuhifadhi
fedha zao ili kujiwekea akiba itakayowasaidia wakati wa maandalizi ya kilimo
kwa msimu ujao na shughuli nyingine za kimaendeleo,” alisema.
COMMENTS