SERIKALI wilayani Bunda mkoani Mara, imeripongeza shirika lisilokuwa la kiserikali la Zinduka lililoko wilayani humo, linalofadhiliwa na sh...
SERIKALI wilayani Bunda mkoani Mara,
imeripongeza shirika lisilokuwa la kiserikali la Zinduka lililoko wilayani
humo, linalofadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society, kwa
kuwapatia wananchi elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ili vitendo
hivyo viweze kukomeshwa ndani ya jamii.
Pongezi hizo zilitolewa jana na mkuu
wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, aliyewakilishwa na katibu tarafa cha
Nansimo, Jonas Nyaoja, kwenye mafunzo ya kupinga vitendo vya ukatili wa
kijinsia yanayofanyika katika mji mdogo wa Kibara wilayani humo.
Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda alisema
kuwa serikali wilayani hapa inatambua mchango mkubwa wa shirika hilo katika
kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili jamii iweze kupata
uelewa na kuachana na vitendo hivyo.
Mkuu wa Wilaya Bunda Lydia Bupilipili . |
“Serikali wilayani Bunda inatambua
mchango mkubwa unaaotolewa na shirika hili la Zinduka katika kutoa elimu kwa
jamii juu ya ukiukwaji haki na unyanyasaji wa kijinsia. Sasa elimu hii wananchi
wetu wakiipata itawasaidia kubadilika na kuacha vitendo hivyo” alisema Nyaoja.
Pia, baadhi ya wadau mbalimbali
wanaopinga vitendo hivyo wilayani hapa, pia wamelishukuru shirika hilo kwa
kuwapatia mafunzo hayo kwa sababu vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekithiri
sana ndani ya jamii yetu, ukiwemo ukatili wa kiuchumi pamoja na ule wa tendo la
ndoa.
Wadau hao ambao ni pamoja na wazee
wa mila, wazee maarufu, viongozi wa madhehebu ya dini, vyama vya siasa,
watendaji wa vijiji na kata, pamoja na wenyeviti wa vijiji, walisema kuwa
Shirika la Zinduka limejikita sanan katika kutoa elimu hiyo kwa jamii.
Waliyaomba mashairika mengine kuiga
mfano huo, kwani wananchi wengi wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo kwa sababu
ya kukosa uelewa na kwamba ni shirika la kwanza kufika mkatika maeneo yao na
kuwapatia elimu hiyo.
Walisema kuwa ukatili mwingine ni
ubakaji wa wanawake, utumikishaji wa watoto wadogo kwenye shughuli hatarishi
ambazo haziendani na umri wao, ukatili wa kutokupeleka watoto shule hususani wa
kike, pamoja na unyanyasaji wanawake na wanaume ndani na hata nje ya ndoa.
Waliongeza kuwa ukatili mwingine
ufanywa na wanaume kuachia shughuli za kilimo na uzalishaji mali wanawake tu,
huku wanaume wengi wakikalia ulevi na uzululaji, ambapo nyakati za chakula
ufika majumbani mwao na kudai chakula tena kwa kuamrisha, ambapo wanawake
wanaposema hakuna chakula uambulia kichapo au matusi ya uzalilishaji.
Walisema kuwa wamridhika na mafunzo
hayo ambayo yamewapatia mwanga, ambapo wataisambaza elimu hiyo katika maeneo
yao ili jamii iweze kubadilika.
Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi
wa shirika la Zinduka, mhasibu wa shirika hilo, Godfrey Anatory, alisema kuwa
wanatoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika kata tisa za
jimbo la Mwibara na kwamba katika awamu ya kwanza walitoa mafunzo hayo katika
kata 13 za majimbo ya Bunda na Bunda mjini.
“Mafunzo haya tunayaendesha kwa kata
tisa za jimbo la Mwibara, lakini pia mafunzo kama haya tulikwishayaendesha
katika kata 13 za majimbo ya Bunda na Bunda mjini. Na baadaye tuendesha mafunzo
haya kwa viongozi mbalimbali wakiwemo maasikari polisi, mahakimu na wanasheria,
ili jamii iweze kujua athari za ukatili wa kijinsia na adhabu yake” alisema.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dk.
Stanely Maendeka, alisema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kupata uelewa sahihi
wa dhana za kijinsia na dhana ya ukatili wa kijinsia, na kupata uelewa na uwezo
wa kutetea na kukomesha ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.
Dk. Mahendeka aliyataja maelengo
mengine kuwa ni pamoja kurekebisha mapendekezo ya awali ya mradi, ili ibebe
shughuli zinazogusa kukomesha ukatili wa kijinsia, kurekebisha bajeti iweze
kuingiza au kuchukuwa shughuli zilizopendekezwa, kukomesha ukatili wa kijinsia
na kuweza kutekeleza mradi vizuri zaidi na kupata matokeo yaliyotarajiwa.
COMMENTS