Mtendaji Mkuu Wa Mahakama Ya Tanzania, Hussein Kattanga Akizungumza Jambo Na Mtaalam Kutoka Benki Ya Dunia, Waleed Malik Walipotembelea U...
Mahakama ya Tanzania
inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya watumishi wake pamoja na
wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.
Kituo hicho
kinachojengwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam
kitawaunganisha watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa njia ya video
(video conferencing).
Akizungumzia Kituo
hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma alisema ujenzi
wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za Mahakama ambacho pia wadau wa
Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa.
Alisema badala ya
Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda kupata baadhi ya mafunzo
kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa
wakiyapata katika kituo hicho.
Naye Mratibu wa Mpango
Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahara
Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango
Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya
Mpango huo, Majaji na Mahakimu hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha
upatikanaji wa haki kwa wakati.
Akizungumzia nguzo ya
tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana na urejeshaji wa
imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za
Mahakama ambapo kupitia kituo hicho wadau wa Mahakama watahusishwa kwenye
Mafunzo mbalimbali ili kurahisisha suala la upatikanaji wa Haki.
Kuhusu suala la
matumizi ya Teknolojia ndani ya Mahakama, Mratibu huyo alisema hivi sasa
Mahakama inao mpango wa kujenga vituo vya aina hiyo kwenye maeneo mbalimbali
nchini kwa lengo la kuunganisha Mahakama zote nchini kwa njia ya video (video
conferencing).
Ujenzi wa kituo cha
Mafunzo cha Mahakama ulioanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya
Tanzania na Benki ya Dunia unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi za
kitanzania milioni 78. Aidha, Jengo la kituo hicho cha mafunzo linajengwa kwa
kutumia teknolojia ya gharama nafuu iitwayo Moladi na linatarajiwa kukamilika
ndani ya wiki nane.
COMMENTS