Na Ahmed Makongo, Bunda: MBUNGE wa Bunda mjini Esther Bulaya, amesema kuwa yeye hana vihoja, jehuri au fujo kama inavyotafasiriwa na ba...
Na Ahmed Makongo, Bunda:
MBUNGE wa Bunda mjini Esther Bulaya,
amesema kuwa yeye hana vihoja, jehuri au fujo kama inavyotafasiriwa na baadhi
ya watu wasiomtakia mema, baada ya kufungiwa kutokushiriki kwenye vikao vya
Bunge, bali yeye ni mkweli na mwenye hoja na anayezijua haki zake
na kwamba amekuwa akinyimwa haki hizo.
MBunge wa Bunda mjini Esther Bulaya |
Mbunge huyo aliyasema hayo juzi
wakati akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya stendi ya zamani mjini
Bunda, mkutano ambao lengo lake ulikuwa ni kuwaelezea wananchi juu ya
ushindi wa kesi ya uchaguzi iliyokuwa imefumguliwa ma wapiga kura wanne wa
jimbo hilo, pamoja na kuhusu kufungiwa kushiriki kwenye vikao vya Bunge.
Alisema kuwa yeye kamwe havunji
taratibu, bali anazijua haki zake na kwamba kufungiwa na bunge kwamba ni
kwa sababu ya vihoja na vurugu zake kama inavyotafasiriwa na baadhi ya watu si
kweli na kuongeza kuwa kilichosababisha kufungiwa ni kile alichokiita ni
kusimamia haki zake pamoja na ukweli kwani yeye pia ni waziri kivuli wa Sera,
Uratibu na Bunge.
“Mimi pia ni waziri kivuli wa Sera,
Uratibu na Bunge, na mimi sina vihoja bali bali ni hoja za msingi, siwezi
kukiuka utaratibu maana ninaujua na pia ninatambua haki zangu” alisema.
Alisema kuwa kuhusu kesi ya kupinga
matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo, amemshinda mara tano mfululizo mpinzani wake
Stephen Wassira, pamoja na wapiga kura wanne, waliokuwa wamefungua kesi hiyo,
baada ya mahakama ya rufaa hivi karibuni kutupilia mbali rufaa iliyokuwa
imekatwa na wapiga kura hao, baada ya kushindwa katika mahakama kuu kanda ya
Mwanza mjini Musoma.
Hata hivyo, alisema kuwa amekuja
kuwauliza wapiga kura ambao ndio waajiri wake kama wanamruhusu afunguwe kesi ya
madai dhidi ya wapiga kura hao, ambao walishindwa katika kesi hiyo ili waweze
kulipa gharama zote za kesi hiyo, ambapo wananchi hao walisikika wakisema kwa
sauti kuwa fungua kesi wakulipe.
Alisema kuwa atawasiliana na
mwanasheria wake Tundu Lissu ili waweze kufungua kesi hiyo ya madai kwani
katika hukumu, mahakama ya rufaa ilisema kuwa warudishe gharama za zote za kesi
hiyo.
Alisema kuwa hilo litakuwa fundisho
kwa watu wengine kuacha kupotezea muda watu bure pasipo sababu za msingi,
wakati wakijua fika kuwa alishinda katika uchaguzi huo wa mwaka 2015 kihalali
kabisa.
Alisema kuwa wananchi wa jimbo lake
amewamisi kwa kukosa mawasiliano na kupata maoni, changamoto na matatizo yao
kwa kipindi chote cha miaka miwili, ambacho alikuwa akishughulikia kesi, wakati
jimbo lake lina changamoto nyingi zikiwemo za maji, na wanyama waharibu kutoka
katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushambulia mazao ya wakulima.
“Niliwamisi sana eti na nyinyi
mumenimisi si ndiyo” alisema huku akishangiliwa na kuitikiwa na wananchi kwamba
walimumisi kwa kipindi kirefu.
Katika hatua nyingine pia mbunge
huyo alisema kuwa kutokana na hali ya maji katika mji wa Bunda, kuwa ya
kusuasua, sasa atatoa kiasi cha shilingi milioni 20 kutoka kwenye mfuko wa
jimbo, na kununua mabomba kwa ajili ya kuunganisha maji katika kata zote za mji
huo, ambapo pia amewataka wananchi kutokulazimishwa kununua vifaa vya maji
katika duka la mtumishi mmoja wa mamlaka ya maji kama waziri mwenye dhamana
alivyokwishaagiza.
Pia, alisema kuwa pia atahakikisha
inapatikana gari nyingine ya kituo cha polisi Bunda kwa ajili ya kufanyia doria
na kupambana na uharifu na vitendo vya uharifu, ambapo amewataka wananchi
jimboni humo kutoa ushirikiano wa kutosha kwa askari polisi ili waweze
kutekeleza wajibu wao ipasavyo ya kulinda raia pamoja na mali zao.
Alisistiza kuwa yeye ni mbunge wa
vitendo lazima ahakikishe jimbo hilo linakuwa na maendeleo.
Mkutano huoambao ulihudhuriwa na
maelefu ya wananchi, pia walikuwepo viongozi mbalimbali wa chama hicho,
wakiwemo wabunge pamoja na Naibu katibu mkuu wa Chadema Salumu Mwalimu.
COMMENTS