JAMII imeshauriwa kujiunga kwenye vikundi ili kuunganishwa kwenye mfumo wa teknolojia ya usafishaji wa maji taka kwa ajili ya matumizi me...
JAMII imeshauriwa kujiunga kwenye vikundi ili
kuunganishwa kwenye mfumo wa teknolojia ya usafishaji wa maji taka kwa ajili ya matumizi mengine ili
mfumo huo uwasaidie kutumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali zenye tija badala
ya kuyateketeza baada ya matumizi.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya maji taka
(OSWAMS), Juma Mohamed Nasoro katika ziara ya maofisa mbalimbali wa
serikali walipokuwa wakitembelea mradi
huo unaotekelezwa katika nyumba za maofisa wa jeshi la polisi, mikocheni jijini Dar es Salaam.
Alisema tekonolojia ya usafishaji wa maji taka ni
muhimu wakati huu taifa likihitaji watu wake kuwajibika ipasavyo kwa kuanzisha
miradi ya uzalishaji mali kufikia uchumi
wa kati kwa njia ya viwanda.
Kwa bahati mbaya, sehemu kubwa ya watu hawajatambua
fursa zilizopo katika matumizi ya teknolojia hiyo na kusababisha maji taka yanayozalishwa
kuteketezwa wakati yangetumika kwa ajili
ya shughuli za kilimo, ufugaji wa samaki, ujenzi na bustani.
“Maji machafu ni fursa sio tatizo. Kwa hali ilivyo
sasa kila hitaji la maji lazima yatumike maji ya Dawasco. Tunataka maji taka
yasafishwe na yatumike kwa shughuli za kuongeza kipato sio kutegemea maji ya
Ruvu chini na Juu. Ili kufikia malengo haya ni lazima elimu ipelekwe kwa
wananchi ya umuhimu wa teknolojia hizi ambayo pia huzuia magonjwa hasa ya
mlipuko,”alisema.
Akifafanua kuhusu mfumo huo wa kutibu maji taka,
Nasoro alisema kabla ya maji hayo kutumika hupitia hatua kadhaa kuanzia
utengenezaji wa chemba ambayo ni ya kwanza ya matibabu ya maji hayo.
Kisha maji taka hupitishwa kwenye mfumo wa pili wa tiba unaojulikana kitaalamu kama
anaerobic (ABR) na U-Flow Anaerobic (UAF ) ambapo wadudu hula takataka kabla ya
kufikia kiwango cha juu cha udhibiti, alisema.
“Maji yanayotibiwa kwa njia hizo yanakuwa yametibika
kwa asilimia 85 na kiasi kingine huenda aridhini. Kwa hali hii sio rahisi
kusababisha magonjwa, ni salama kwa matumizi kwani yamesafishwa kitaalamu.
Yanafaa sana kwa kilimo na ufugaji kwani yana mbolea, nitrogen na
phosphorus,”alisema.
Alisema kampuni yake imefanikisha teknolojia hiyo
katika taasisi za umma na shule binafsi ya Libermann ya pia ya jijini Dar es
Salaam.
Baadhi ya maofisa waliotembelea mradi huo kutoka
wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto, Jiji la Dar es
Salaam na Manispaa za Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo waliridhishwa na
utekelezwaji wa mpango huo na kusema hatua inayotakiwa ni jamii kuhamasishwa
kujiunga baada ya kuutathimini na kuingizwa kwenye mipango ya ya serikali.
Afisa afya wa Manispaa ya Ubungo Wilson Msangi
alisema teknolojia hiyo ni hupunguza gharama ya ukusanyaji wa maji taka,
huchukua nafasi ndogo na kushauri Halmashauri kuihamasisha kwenye maeneo kama
shule na hospitali kutokana na maeneo hayo kuzalisha kiasi kingi cha maji taka.
COMMENTS