WANAFUNZI wawili wa shule ya msingi Sarawe iliyoko katika tarafa ya Chamriho halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamekufa na wengin...
WANAFUNZI
wawili wa shule ya msingi Sarawe iliyoko katika tarafa ya Chamriho halmashauri
ya wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamekufa na wengine sita kujeruhiwa katika
ajali mbaya ya kuangukiwa ukuta wa chumba cha darasa wakati wakipembua mahindi
kwa ajili ya chakula chao shuleni hapo.
Tukio hilo limetokea juzi majira saa kumi
jioni wakati wa saa ya mapumziko katika eneo la shule hiyo.
Wanafunzi waliokufa katika tukio hilo ni
pamoja na Anastazia Wazilana (8) aliyekufa papo hapo na Amosi Stima Igala (8)
aliyekufa wakati akikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza
kwa ajili ya matibabu zaidi, ambapo wote walikuwa wanasoma darasa la pili
shuleni hapo.
Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Bunda
Dk. Nuru Yunge amethibitisha vifo hivyo na kwamba majeruhi walipelekwa kituo
cha afya Ikizu na wengine wamehamishiwa katika hospitali ya DDH Bunda.
“Pale kituo cha afya Ikizu tulipokea majeruhi
saba, na wengine wawili tukawahamishia katika hospitali ya DDH Bunda, kutokana
na hali zao kuwa mbaya, lakini kwa taarifa niliyopata majeruhi mmoja amekufa
wakati akipelekwa katika hospitali ya rufaa ya Bugando” alisema.
Afisa tarafa ya Chamriho Boniphace Maiga,
aliwataja wanafunzi waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na Happynes Mussa (13) wa
darasa la tano, Wambura Nyamrosha (12) wa darasa la nne, Sara Wazilana (14) wa
darasa la sita, Emmanuel Mkiriti (8) wa darasa la pili, Mugaya Galinde (8) wa
darasa la pili na Pili Juma Matwiga (7) wa darasa la kwanza.
Maiga alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni
ukuta wa darasa hilo kuwa na ufa wa siku nyingi, ambapo uliporomoka na
kuwaangukia wakati wakianda mahindi kwa ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni
hapo, kinachotolewa na shirika la PCI.
“Wakati wa mapumziko wanafunzi hao walikuwa
nje ya dasrasa hilo wakipembua mahindi ya PCI na ghafla ukuta huo ulidondoka na
ulikuwa na naufa mkubwa siku ninyingi. Mwanafunzi mmoja alifia hapo hapo na
mwengine amekufa wakati akikimbizwa Bugano baada ya kuwapatiua rufa.
Baadhi ya mashuhuda akiwemo katibu wa huduma
za jamii katika serikali ya kijiji cha Sarawe, Richard Karangi, walilielezea
tukio hilo kuwa ni la kusikitisha, ambapo muuguzi mmoja katika hospitali ya DDH
Bunda, alizungumzia hali ya majeruhi mmoja aliyempokea kwamba inaendelea
vizuri.
Kamanda wa polisi mkoani Mara kamishina
msaidizi wa polis, Jafari Mohamed hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, lakini
polisi wilayani hapa wamethimitisha kuwepo kwa tukio hilo.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi
waliozungumza na waandishi wa habari walisema kuwa ipo haja ya wakaguzi wa shule
kukagua majengo ambayo hayana ubora na kuagiza yasitumiwe na wanafunzi ili
kuepusha majanga kama hayo ambayo siyo
ya lazima yasitoke tena.
COMMENTS