Habari Mpya

Thursday, 2 November 2017

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa (Mb), amewapongeza Wakala wa barabara nchini (TANROADS), kwa mikakati wanayotumia kudhibiti vitendo vya rushwa katika vituo vya mizani hapa nchini.

Akifungua Mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi la TANROADS mjini Kigoma, Kwandikwa, amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha watendaji wake wote wanakuwa waadilifu ili rasilimali chache zitumike kwa manufaa ya wote.

“Hakikisheni kila mtakaye mkamata kwa vitedo vya rushwa hatua za kisheria anachukuliwa ikiwemo na kufukuzwa kazi ili kuonyesha kuwa jambo la rushwa tunalichukia na hatulipendi katika Serikali”, alisema.

Naye Mtendaji Mkuu Wa Wakala huo Eng. Patrick Mfugale, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja watumishi 71  wamefukuzwa kazi katika vituo mbalimbali vya mizani hapa nchini kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Ameongeza kuwa TANROADS wamejipanga kuhakikisha miradi yote ya ujenzi na vituo vya mizani vinafanya kazi kwa weledi na uaminifu ili kujenga imani kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS Hawa Mmanga, amemuhakikishia Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa wakala wake umejipanga kutekeleza kikamilifu ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja hapa nchini kwa wakati, ubora na kuzingatia thamani ya fedha.


Wajumbe wa baraza la TANROADS kutoka mikoa yote  nchini wamekutana katika mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi ili kutathimini utendaji kazi wao na kuibua mikakati mipya itakayowezesha wakala huo kufanya kazi zake kwa weledi na kwa kukidhi mahitaji ya nchi.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -