SERIKALI imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2 kila mwezi ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini. Kauli hiyo ime...
SERIKALI imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2 kila mwezi
ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 2, mwaka huu na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, George Simbachawene wakati akizungumza na
wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin Luther, kwenye
sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa ya Dodoma.
Simbachawene ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali kwa
niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Serikali itaendelea kuboresha
elimu ya sekondari kwa kuajiri walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi.
“Wazazi wa wanafunzi wanaohitimu tunawakaribisha kwenye shule za
sekondari kwa sababu zote zina walimu wa kutosha, madawati na vifaa vya
kufundishia. Kila mwezi tunatenga sh. bilioni 22.2 kuendesha shule za msingi na
za sekondari hadi kidato cha nne,” alisema.
Alisema hivi sasa, baadhi ya shule zinakabiliwa na changamoto
ndogo ya upungufu wa walimu wa sayansi lakini nayo itatuliwa hivi karibuni kwa
sababu vibali vya ajira vimeanza kutolewa.
“Tunaendelea kuziboresha na tumeshuhudia miaka ya karibuni
wanafunzi bora kitaifa wakitoka katika shule za Serikali ambazo wengi wamezoea
kuziita ni shule za kata. Hakuna shule za kata. Zote ni zimejengwa na
Serikali,” alisisitiza.
“Ukienda vyuo vikuu, wanafunzi na ufaulu wa juu wengi wao ni
wale waliotoka kwenye shule za Serikali,” aliongeza.
Aliwataka wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao Septemba 6
na 7, wasiwe na hofu kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwafanya wachanganye
mambo na kisha kufeli.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa
shule hiyo, Rabbiely Mmanga aliwaasa wazazi na kuwaomba wasiwaingize watoto
kwenye migogoro kwani matendo hayo yanawajisi watoto na kuwaathiri kisaikolojia
hata wawapo shuleni.
“Ninawaomba sana wazazi, tofauti zenu ziishie chumbani na
zisifike masikioni mwa watoto kwa sababu zinawasumbua kisaikolojia na
kuwaharibia concentration yao kimasomo. Tumewahoji baadhi na wamesema wanaumia
kwa kukumbuka adha ambayo mama anaipata kutoka kwa baba, au baba anaipata
kutoka kwa mama,” alisema.
Katika mahafali hayo, wanafunzi mbalimbali walipewa vyeti kwa
kufanya vizuri kwenye masomo mbalimbali huku Ismail Milambo na Nise-Magreth
Malila wakiibuka kidedea kwenye masomo yote (best academic performers). Tuzo za
nidhamu bora (discipline) zilichukuliwa na Michael Nyalusi na Sayuni Kampuni.
Wanafunzi wengine waliopata tuzo na masomo yao kwenye mabano ni
Ismail Milambo (Hisabati), William Terry William (Kiingereza), Majaliwa K.
Majaliwa (Sayansi), Nise Malira (Kiswahili), Clinton Dotto (Social Studies) na
Justin Kilimali (Kompyuta).
Wengine walipewa tuzo kwenye vipengele vya michezo, uchoraji na
sanaa, usafi, uongozi shuleni, uimbaji na uongozi wa ibada.
Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu
walisema wanaamini misingi ya elimu walioipata kwenye shule ya
Martin luther haitapotea bure na wakaahidi kufanya mitihani yao kwa umakini ili
watoke na ufaulu wa hali ya juu.
Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini, wanatarajiwa kufanya
mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.
COMMENTS