Habari Mpya

Tuesday, 31 October 2017

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amekagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na yakisasa itakayotoa huduma za usafirishaji katika  Ziwa Victoria.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamissi,akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa(Wa pili kulia), hatua zilizofikiwa za ukarabati wa meli ya Mv. Clarius na Mv. Umojakatika Bandari ya Mwanza.

Akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Prof. Mbarawa, amewataka wafanyakazi wa Kampuni hiyo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi ili kazi hiyo ianze mara moja na kukamilika kwa wakati.

“Mkandarasi ameshapatikana hivyo hakikisheni mnatoa ushirikiano na mnafanya uhakiki wa kimahesabu vizuri ili kazi hii ifanyike kwa gharama nafuu, ubora na muda mfupi”, amesema Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa, amekagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya Mv. Clarias na Mv. Umoja ambapo ameeleza kuridhishwa kwake na hatua zilizofikiwa, na hivyo kuwataka MSCL kutafuta mizigo ya kusafirisha kutoka Bandari ya Mwanza kwenda Bandari  ya “Port Bell”, nchini Uganda.

“Kukamilika kwa meli kuwiane na kasi ya kutafuta mzigo mwingi ili meli hizi zifanye biashara wakati wote na kuhakikisha Kampuni yenu inapata mapato mengi yatakayowawezesha kujiendesha kwa faida”, amesisitiza Waziri Mbarawa

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Erick Hamissi, amemhakikishia Prof. Mbarawa, kuwa wamejipanga kufanya ukarabati mkubwa wa meli za Mv. Victoria, Butiama na Liemba ili kuziwezesha meli hizo kufanya kazi katika ubora wake wa awali na kupunguza tatizo la usafiri katika ziwa Victoria na Tanganyika.

“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunazikarabati meli zetu zote ili ziwe katika ubora unaostahili wakati wote”, amefafanua Bw. Hamissi.

Katika kuhakikisha maendeleo ya kibiashara na kuichumi  yanafikiwa katika Ukanda wa maziwa makuu  nchini, Serikali imejipanga kuhakikisha inafufua usafiri wa meli za abiri na mizigo katika ukanda huo.

Leave a Reply

Subscribe to Posts | Subscribe to Comments

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -