HOSPITALI ya rufaa ya mkoa wa Tanga, Bombo, haina chumba cha kuwalaza wagonjwa mahututi (ICU) hali inayosababisha wagonjwa wanaohitaji uang...
HOSPITALI ya rufaa ya mkoa wa Tanga, Bombo,
haina chumba cha kuwalaza wagonjwa mahututi (ICU) hali inayosababisha wagonjwa
wanaohitaji uangalizi wa matibabu, hulazimsihwa kuwekwa katika wodi za wagonjwa
wengine, wakiwa na mitungi ya mashine za gesi za kupumulia.
Uchunguzi uliofanywa na Majira takribani mwezi
mmoja katika hospitali hiyo ya rufaa inayopokea wagonjwa kutoka katika vituo
vya afya na hospitali za wilaya nane zilizopo mkoani hapa, na kuthibitishwa na
Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga (RAS) Injinia Zenna Said, Mganga Mkuu wa mkoa wa
Tanga, Dk. Asha Mahita na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. Jumanne Karia
kwa pamoja walielezea jitihada za mkoa za kuhakikisha wanajenga chumba hicho.
Hospitali hiyo kongwe hapa nchini, imekuwa na
tatizo hilo takribani miaka 7 sasa, kwa chumba hicho kukosekana ambapo awali
walikuwa wakitumia chumba kimoja kabla ya kusitisha kualza wagonjwa, kikawa
kinatumiwa na watoto wadogo lakini baadaye kikawa kinatumiwa na wagonjwa
wanaotumia kadi za huduma ya Bima ya Afya, lakini sasa kinatumika kwa shughuli
nyingine za hospitali.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Tanga, wamekuwa
wakilalamikia hali hiyo wakieleza kwamba wagonjwa Mahututi kuwachanganya na
wagonjwa wengine huku wakiwa na mitungi ya gesi ni kutowatendea haki, kwa kuwa
wanaporuhusiwa ndugu kuona wagonjwa kunakuwa na msongamano mkubwa na kelele za
hapa na pale za kufariji wagonjwa wengine.
“Nilishtuka nilipoingia wodi ya Galanosi kule
kwa akina mama nilimkuta mke wa diwani wa Kirare, Saleh Mwagilo akiwa amewekewa
mashine ya gesi huku akiwa mahututi, nilishangaa nilipouliza nikaambiwa
hospitali haina chumba cha wagonjwa mahututi,” alisema Haruna Magembe aliyekuwa
na mgonjwa katika wodi hiyo ya Galanosi.
Alisema kuwa licha ya kuwepo mgonjwa huyo katika
wodi nyingine mbalimbali zimekuwa na wagonjwa mahututi wengi wanaochanganywa na
wagonjwa wa kawaida haliambayo imekuwa ikileta tafsiri mbaya ya suala la
viongozi wa mkoa kuwajibika katika kuhakikisha chumba hicho kinapatikana ili
kuwawezesha wagonjwa hao kupata tiba stahili kwa mujibu wa taratibu na sera ya
wizara ya afya.
Alipotafutwa diwani huyo kwa ajili ya kuelezea
suala la mgonjwa wake huyo, hakuweza kupatikana lakini mtu wake wa karibu
aliyejitambulisha kwa jina la Kasirani kasirani, alisema amemhamishia mkewe
huyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako anaendelea na matibabu baada
ya kulazwa takribani wiki mbili akiwa na mtungi wa oksijeni bila mafanikio.
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo Katibu Tawala wa
mkoa wa Tanga, Injinia Zena alikiri kukosekana kwa chumba hicho, lakini alisema
kwa taarifa za jitihada zinazofanyika kupata chumba hicho, alimwelekeza
mwandishi wa habari hizi akakutane na Mganga Mkuu wa mkoa Mahita ambaye atakuwa
na majibu kuhusu kukosekana kwa ICU katika hospitali hiyo.
“Ni kweli lakini sisi kama mkoa tumekuwa na
mipango mbalimbali ya kupatikana lakini nenda kwa Mganga Mkuu atakupa tumefikia
wapi kuhusu kupatikana kwa ICU,” alisema Injinia Zenna.
Dk. Mahita alipoulizwa kuhusu suala hilo,
alisema kuwa ni kweli hawana ICU katika hospitali hiyo lakini wagonjwa wenye
mahitaji hayo wamekuwa wakiwahudumia vizuri licha ya kukosa chumba kinachofaa
kwa huduma hiyo na kwamba hawawezi kuwazuia watu wanaokuja kuwaona wagonjwa
waliowachanganya na wagonjwa wengine.
Hata hivyo, Dk Mahita ambaye alisema pamoja na
kukosa huduma hiyo hospitali hiyo katika kipindi cha hivi karibuni wameweza
kuboresha huduma mbalimbali na kuhusu ICU wamekuwa na jitihada mbalimbali za
kuhakikisha wanamaliza tatizo hilo baada ya kuomba mkopo kwa Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF).
“Tumeomba mkopo NHIF kwa ajili ya ICU, lakini
kwa sasa wagonjwa wanaokuja kwa mahitaji ya huduma ya ICU tunawapa huduma,
tunachokosa ni eneo la kutolea huduma hiyo tu,” alisema na kuongeza “Hatuwezi
kuwazuia watu wasiende kutazama wagonjwa wao waliokuwa na oksijeni, lakini
ukitaka taarifa zaidi nenda kamuone Dk. Karia ambaye ni Mganga Mfawidhi wa
hospitali, atakupa hadi sasa tumefikia wapi katika suala hilo,”.
Akizungumzia kuhusu hali hiyo Mganga Mfawidhi wa
hospitali hiyo, Dk. Karia alisema kuwa ni kweli chumba hicho kwa sasa hakipo
katika hospitali hiyo baada ya chumba kilichokuwa kikitumika zamani hakina
mfumo wa kutumia gesi pamoja na vifaa vya ICU, hivyo wakaamua kuwachanganya
wagonjwa wenye mahitaji hayo na wagonjwa wengine, lakini tangu mwaka 2013
wameanza ukarabati wa jengo ambalo litatumika kwa huduma hiyo.
Alisema chumba wanachokifanyia ukarabati sasa
ili kitumike kuwa ICU ni kile kilichokuwa kikitumika kama chumba cha Upasuaji
(Theatre) baada ya mradi wa KfW kutoa fedha za ujenzi wa chumba cha Upasuaji
kipya kinachotumika sasa na kwamba sasa wanaendelea kutafuta fedha ili waweze
kukamilisha katika kipindi kifupi kijacho.
“Ni kweli kile chumba cha mwanzo kilichokuwa
kikitumika kama ICU hatukitumii tena na tunachanganya wagonjwa huko katika
mawodi, lakini chumba kile kilikuwa hakina mfumo wa gesi, pia hakikuwa na vifaa
vinavyohitajika kwa wagonjwa mahututi ikiwemo vitanda,” alisema Dkt Karia.
Aliongeza kusema kwamba katika bajeti yam waka
2017/2018 itatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ICU na kiasi cha shilingi
milioni 231 ilitengwa mwaka 2016/2017 kwa jili ya kutengeneza mfumo wa gesi
katika chumba hicho ambapo hospitali kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu
Tawala, imeanza kushughulikia suala hilo la gesi ambayo pia wataiuza katika
hospitali nyingine baada ya kuanza kazi.
“Vile vile kuna vifaa vya msaada kutoka nchini
Ujerumani Mwenyekiti wetu wa bodi ya Hospitali Zahra Noor kwa kushirikiana na
kaka yake Habib Noor na baadhi ya wafanyabiashara wa hapa Tanga akiwemo
Selemani Rahaleo, watasaidia hiyo ICU yetu ikianza kazi,” alisema Dkt Karia na
kuongeza kwamba wameomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 560 kutoka NHIF.
Akizungumza na gazeti hili Meneja wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afy (NHIF) mkoani Tanga, Ali Mwakababu alisema ni kweli
hospitali hiyo imeomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 560 kwa ajili ya
ukarabati wa wodi ya akina mama na watoto pamoja na chumba cha magonjwa mahututi
(ICU).
COMMENTS