SIKU chache baada ya kutoa notisi ya kuachia ngazi ndani ya Simba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez ameanza kuwaaga baadh...
SIKU chache baada ya kutoa notisi ya kuachia ngazi ndani ya Simba, Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez ameanza kuwaaga baadhi ya wafanyakazi aliofanya nao kazi klabuni hapo.
Barbara ameweka bayana kufikia Januari ataachia ngazi kwenye nafasi hiyo kwa sababu alizozianisha, lakini kabla hajatimiza lengo hilo juzi alifanya hafla fupi na wafanyakazi wote waliokuwa chini yake na kuwaaga rasmi na mwenyewe amefichua sababu ya kufanya hivyo.
Barbara alisema kulingana na majukumu yake mbalimbali anayoyafanya wakati huu huenda asipate nafasi nyingine ya kukutana na wafanyakazi wengine wote kwa pamoja na kuwaaga kama anavyotaka.
Alisema Simba inakwenda kucheza mechi tatu Kanda ya Ziwa na watu wa idara ya habari wasiopungua watatu watakuwa huko, huku Simba Queens ikiwa na mechi za ugenini na kuna watu watatoka ofisini kwa ajili ya kusimamia hilo.
“Baada ya hapo kuna shughuli mbalimbali za uchaguzi zinaendelea wakati huu. Kuna wafanyakazi watakuwa bize kusimamia suala hilo kuhakikisha linakamilika kwa ukamilifu ili kupata viongozi bora kama vile ambavyo Simba tunahitaji wapatikane,” alisema Barbara na kuongeza bado ataendelea kuipigania Simba na kufanya kazi za timu hata baada ya notisi yake ya mwezi mmoja kuisha.
“Hivyo jana (juzi) niliona ni siku sahihi kuagana na wafanyakazi wenzangu halikuwa tukio rahisi, kwani ni watu wazuri niliofanya nao kazi kwa pamoja hadi kufikia mafanikio mbalimbali.
“Kuna majukumu naendelea nayo huenda yakawa yanachukua muda na ikashindikana kupata nafasi ya kwenda ofisini mara kwa mara kama hapo awali.”
Katika hatua nyingine Barbara aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii akisema:“Moja ya sehemu ngumu kuondoka Simba ni kuwaaga watu wazuri kwenye sehemu ya uongozi. Popote ninapoenda, chochote kitakachofuata, wafahamu kuwa Barbara Gonzalez atapatikana kwa simu moja.”
Barbara aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu Septemba 2020 kuchukua nafasi iliyoachwa na Senzo Masingiza aliyeacha kazi ghafla kabla ya kuibukia Yanga na kufanya kazi hadi mapema mwaka huu alipotangaza kuondoka na kumpisha Mzambia Andreew Mtine.
CHANZO MWANASPOTI
COMMENTS