Habari Zote
WAZIRI wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezungumzia umuhimu
kwa wafanyakazi wote waliopata fursa ya kujenga reli ya kisasa (SGR) kufanya
kazi kwa moyo na uzalendo mkubwa ili kuandika historia katika maendeleo ya
Tanzania.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Yapi Merkezi Abdullah Kilic, anayejenge reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam-Morogoro yenye urefu wa KM 205 eneo la Soga, mkoani Pwani.
Mbarawa amesema
hayo alipokuwa anakagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), inayojengwa usiku na
mchana kuanzia Dar es Salaam-Morogoro
yenye urefu wa KM 205 ambayo kwa kiasi kikubwa ameonesha kurizishwa na kasi
ya ujenzi huo.
“Hii ni fursa
kubwa ambayo mmeipata kujenga mradi mkubwa utakaocha historia katika nchi hii
hivyo fanyeni kazi kwa bidii, weledi na uzalendo”, alisema.
Amewataka viongozi
wa Shirika Hodhi la Rasilimali za Reli (RAHCO), kuwa katika eneo la mradi wakati
wote ili kuhakikisha mkandarasi anapata ushirikiano wa kutosha na hivyo
kuwezesha mradi kukamilika kama ilivopangwa.
Meneja
Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mhandisi Maizo Mgedzi, akifafanua jambo
kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, alipokagua ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es
Salaam-Morogoro yenye urefu wa KM 205 eneo la Soga, mkoani Pwani, inayojengwa
usiku na mchana.
Pia amemuagiza
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Edward Malima, kuhakikisha wanafunzi wa
uhandisi wanapata nafasi ya kutosha ya kushiriki kwa vitendo katika ujenzi huo
ili kuiwezesha nchi kuwa na wataalamu wa kutosha wenye uzoefu kwenye ujenzi na
usimamizi wa miradi ya reli.
“Ongezeni
wahandisi wanafunzi katika mradi huu, nia yetu ni kupata reli lakini pia na
wataalamu wengi katika ujenzi na uendeshaji wa reli”, alisisitiza.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akimpongeza mwanamke anayeendesha mtambo wa kutengeneza tuta la reli ya kisasa (SGR), Miriam Juma alipomkuta saa 4 za usiku akichapa kazi katika eneo la Soga, mkoani Pwani.
Kwa upande wake Malima,
amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kufanya ziara ya
kustukiza usiku ambayo imechochea hamasa kwa wafanyakazi na mkandarasi na
kuahidi kumsimamia mkandarasi kikamilifu
ili mradi huo ukamilike kwa wakati na uwiane na thamani ya fedha.
Muonekano wa Mitambo ya
kisasa inayojenga Reli ya Kisasa (SGR), kutoka Dar es Salaam-Morogoro yenye
urefu wa KM 205 eneo la Soga mkoani Pwani, inayojengwa kwa saa 24.
Takribani
shilingi trilioni 2.8 zinatarajiwa kutumika kkstika ujenzi wa reli hiyo awamu
ya kwaza kati ya Dar es Salaam na Morogoro yenye urefu wa KM 205 itakayowezesha
treni ya umeme yenye kasi ya KM 160 kwa saa kupita na hivyo kuhuisha mfumo wa
usafiri wa reli hapa nchini.
MKUTANO wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)
umefanyika leo tarehe 19 Oktoba, 2017 mjini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Mkutano huo
umetanguliwa na ule wa awali ngazi ya Wataalamu wa Masuala ya Fedha, Wakuu wa
Vyombo vya Usalama, Majeshi na Waratibu wa Nchi (ICGLR National Coordinators)
pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk.
Augustine Mahiga, ametoa ujumbe akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli mkutanoni hapo.
Mkutano huu umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Wawakilishi
wao kutoka nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudani, Sudani Kusini,
Tanzania, Uganda na Zambia ukiwa na ajenda kuu ya kupitia na kujadili hali ya
Siasa, Ulinzi na usalama katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu hasa katika nchi
za Burundi, Kongo, Jamhuri ya Kongo, Afrika ya Kati na Sudani Kusini.
Ajenda zingine zilikuwa ni pamoja na kupokea taarifa ya Michango ya
nchi wanachama ambapo Kuhusu
hali ya usalama katika Nchi hizo kwa ujumla iliripotiwa kuwa inaendelea
kuimarika kwa kiwango kikubwa isipokuwa nchini DRC ambapo kwa sasa operesheni zinaendelea
kufanywa na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC- MONUSCO (FIB) dhidi ya
vikundi vya waasi ndani na nje ya DRC.
Mkutano huu ulifuatiwa na Mkutano wa Nane Wakuu wa Nchi na Serikali wa
Mpango wa Amani na Usalama katika Maziwa Makuu (8th Regional Oversight
Mechanism for the Peace, Security and Cooperation Framework of the DRC and the
Region).
Taasisi zingine za kimataifa zilizoalikwa kwenye Mikutano hii ni pamoja
na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) ambapo ujumbe wake uliongozwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk.
Stergomena Tax.
AFISA Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Hamis Lissu
ameahidi kutatua kero zote zinazowakabili baadhi ya wamiliki wa Shule
Binafsiinafsi wa mkoa ikiwemo ya tozo kubwa za biashara zinazotozwa shule
hizo .
| Afisa elimu wa mkoa wa Dar es salaam akizungumza na washiriki wa mkutano uliowakutanisha wamiliki wa shule binafsi mkoa wa Dar es Salaam |
Pia amewaomba wamiliki wa shule hizo kipindi cha likizo wajitolee
kuwafundisha masomo ya sayansi wanafunzi wanaotoka shule za serikali kwa kuwa
wana walimu wengi wa masomo hayo.
Ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua Mkutano Maalumu
uliowakutanisha wadau mbalimbali na wamiliki wa shule zilizopo jijini hapa.
Amesema wamiliki wa shule hizo pamoja na shule zao wanapaswa watambaue
huduma wanazopewa ni stahiki hivyo ni sawa wanazopatiwa shule za
Serikali.
“Natamani kuziona shule zote binafsi zikiwa zinazoongoza kutokuwa na
changamaoto zozote kwani tunatambua mchango wa uwekezaji hapa nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wamiliki wa Shule
Binafsi nchini (TAMONGSCO), Charles Totela ameishukuru Serikali ya mkoa huo
kwani imekuwa ikiwapa ushirikiano wa kutosha.
Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali ya mkoa huo kuwaundia dawati la
pamoja litakalowakutanisha viongozi wote wa shule binafsi, za serikali na
watendaji wao ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana baadhi ya changamoto ambazo
zimekuwa hazifanyiwi kazi.
Naye Mkurugenzi wa Shule za Al-Muntazir, Mahmood Ladack
amewashukuru wamiliki wa shule hizo kwa kuhitisha mkuatano huo ambao anataraji
utakuwa na manufaa makubwa kwao na taasisi wanazosimamia katika kupambana na
changamoto mbalimbali zinazowakabili.
UONGOZI wa mkoani
Simiyu umembadilishia majukumu ya kazi Tabibu, Laurent Biyengo na
kuwa mlinzi katika lango kuu la kuingilia hospitali kutokana na kushindwa
kuyamudu majukumu ya kitabibu.
Biyengo ambaye anadaiwa kushindwa kuingia kazini
na kwenda kulewa saa za kazi alipokuwa zamu septemba 27 mwaka huu na
kusababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John kutoka kwa kushindwa kupatiwa
huduma.
Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika kutoka ndani
ya hospitali hiyo na kuthibitishwa na baadhi ya matumishi wenzake zinaeleza
kuwa tangu aanze majukumu yake hayo mapya sasa ni kipindi cha majuma mawili
akilinda getini.
Wakizungumza na hivi karibuni, baadhi ya
madaktari hao walisema kuwa adhabu aliyopewa ni ya haki kutokana na kitendo
alichokifanya ambacho kinakiuka maadili ya taaluma yao ya utabibu.
“Huyu mwenzetu amepata adhabu ya haki na hii
wamemsaidia sana maana alipaswa kufukuzwa kazi haiwezekani umepangwa kutoa
huduma za kitabibu katika hospitali kubwa kama hii halafu unakwenda kulewa na
kusababisha wagonjwa kutopata huduma, nikukiuka maadili ya kitabibu,”alisema
Daktari mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Walisema kuwa kitendo alichokifanya
kimewapotezea imani kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu katika hospitali
hiyo, huku wengine wakitumia lugha za kuwakejeli na kuwadhihaki jambo ambalo
linawashusha molali ya kazi.
Kwa mujibu wa habari za kuaminika kutoka chanzo
ambacho kilifika katika hospitali ya wilaya ya Maswa na kumshuhudia daktari
huyo akiwa katika lango kuu la kuingilia hospitalini hapo, na
kumwona akufungulia magari na pikipiki zinazoingia na kutoka
sambamba na watu wanaokuja kupata matibabu hata hivyo jitihada za kuongea naye
hazikuzaa matunda baada ya kugoma kuongea.
Akizungumzia suala hilo Mkuu wa wilaya ya Maswa
Dk. Seif Shekalaghe alikiri kwa daktari huyo kubadilishiwa majukumu ya kazi na
kusisitiza kuwa hiyo ni hatua ya awali walizozichukua kutokana na kitendo
alichokifanya.
“Nimeambiwa ya kuwa amebadilishiwa majukumu ya
kazi kutoka kutoa huduma za kitabibu na kuwa mlinzi lakini nahisi kuna hatua
zaidi ya hiyo inatakiwa kufanywa nipeni muda tutapata majibu sahihi,”alisema
Shekalaghe.
Kufuatia tukio hilo,Waziri wa Afya ,Ustawi wa
jamii,Wazee,Jinsia na Watoto,Ummy Mwalimu alimwelekeza Naibu Katibu Mkuu
TAMISEMI Dk. Zainab Chaula kumchukulia hatua.
MAKAMISHINA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
wametembelea eneo la Njedengwa Mjini Dodoma yanapojengwa majengo ya makao makuu
ya NEC na kuelezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC) Jaji (R), Simistocles Kaijage, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan
Kailima na Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Yohana Mashausi
wakiwaongoza makamishna wa NEC kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa majengo ya
ofisi za NEC jana. Mradi huo unafanyika katika eneo la Njedengwa Mjini Dodoma.
(Picha na Abdulwakil Saiboko)
Akizingumza mara baada ya ziara hiyo
iliyoongozwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji (R) Semistocles Kaijage, Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema kwamba maendeleo ya ujenzi
yanaridhisha na ujenzi utakamilika kwa muda uliopangwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R),
Simistocles Kaijage (wa pili kulia) akifurahia jambo na Mhandisi kutoka Wakala
wa Majengo (TBA), Bw. Yohana Mashausi (kulia) baada ya kupewa maelezo ya mradi
wa ujenzi wa majengo ya ofisi za NEC jana wakati makamishana wa NEC
walipotemdelea mradi huo. Mradi huo unafanyika katika eneo la Njedengwa Mjini
Dodoma na unatarajiwa kukamilika mwakani. (Picha na Abdulwakil Saiboko)
Kailima amesema kwamba awamu ya kwanza ya
ujenzi wa mradi huo ambao unajumuisha majengo matatu utakamilika mwezi Julai,
mwakani.
“Mradi huu una awamu mbili za ujenzi lakini
utatoa majengo makubwa matatu, jengo la kwanza ni jengo kubwa la ofisi litakua
na ghorofa nane, la pili ni jengo la ukumbi wa kutangazia matokea ambao utakua
na uwezo wa kuchukua watu 800, uchaguzi mkuu ujao wa 2020 tunatarajia kutangaza
matokeo kwenye ukumbi huu na pia kuna jengo la maghala ya kuhifadhia vifaa vya
uchaguzi,” amesema Kailima.
Aliongeza kusema “Mradi huu unakwenda vizuri
kwa sababu gharama yake ni takribani shilingi bilioni 13, awamu ya kwanza
itagharimu bilioni 11/- ambayo itahusisha ujenzi wa jengo la ofisi, pia
itajumuisha ujenzi wa sehemu ya jengo la kituo cha kutangazia matokeo na
maghala.
Awamu ya pili ambayo itagharimu bilioni 2/-
itakua imekamilika mwaka 2018. Kuanzia mwenzi Agosti 2018 Tume tutaanza kuhamia
Dodoma,” amesema.
Kutoka kushoto ni Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Yohana
Mashausi akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kwa makamishna wa tume
hiyo walioongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R),
Simistocles Kaijage, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima na Makamu
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid. Ujenzi huo unaoendelea
katika eneo la Njedengwa Mjini Dodoma unatarajiwa kukamilika mwakani. (Picha na
Abdulwakil Saiboko).
Akizungumzia suala la bajeti ya ujenzi wa
majengo hayo, Kailima amesema fedha zipo na zitakua zikitolewa kadri
zitakavyohitajika.
Mwanzoni akiwatembeza makamishna wa tume
kwenye eneo la mradi, Mkandarasi Msimamizi kutoka Wakala wa Majengo (TBA),
Mhandisi Yohana Mashausi amesema ujenzi huo umechukua muda mrefu kwenye eneo la
msingi kwa kuwa eneo hilo lina ardhi yenye mwamba mgumu sana.
Mhandisi Mashausi amesema kwamba TBA pia
imechukua tahadhari kubwa katika ujenzi wa msingi imara kwa kuzingatia hali ya
kijogirafia ya Dodoma ambako kuna hatari ya kukumbwa na matetemeko ya ardhi.
SERIKALI imesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA), unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa
sasa umefika zaidi ya asilimia Tisini.
Meneja Miradi wa Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi, akimuonesha
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius
Kwandikwa (Mb), (Kushoto), upanuzi wa maegesho ya ndege uliofanyika uwanjani
hapo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elius
Kwandikwa, mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la kupumzikia abiria na
upanuzi wa maegesho ya ndege katika uwanja huo leo mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elius Kwandikwa (Mb),
akikagua maboresho ya mfumo wa majitaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za
ukarabati wa uwanja huo.
"Nimeridhishwa na ukarabati unaoendelea katika uwanja huu na nafikiri
mmejionea wenyewe kazi inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii
kazi itakamilika hivi karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa ukarabati huo ambao pia umehusisha
maboresho ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa
ujumla kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.
Mafundi wakiendelea na
ukarabati katika jengo la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA). Ukarabati huo umefika zaidi ya asilimia Tisini na unatarajiwa kukamilika
mwezi Desemba mwaka huu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya
ndege nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo
likiwa ni kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika
uchumi wa kati.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa,
akifafanua jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Arusha,
Mhandisi Johny Kalupale, alipokagua barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1) na
Barabara ya Mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass KM 42.4) mkoani Arusha.
Kwa upande wake, Meneja Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi,
amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha jumla ya
ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.
Ameongeza kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka laki nane kwa mwaka
hadi kufikia milioni moja na laki mbili mara baada ya kukamilika kwa uwanja
huo.
Muonekano wa Barabara ya
Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha, ambayo imekamilika kwa kiwango cha
lami. Kukamilika kwake kumesaidia kupunguza ajali na msongamano katika eneo
hilo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina
- Tengeru (km 14.1) na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4)
ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru ni
mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia katika mkoa
huo kwani kumepelekea kupungua kwa ajali na msongamano wa
magari katika eneo hilo.
Ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara na kutunza mazingira
yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa vizazi vya
sasa na vijavyo.
Muonekano wa Daraja la
Ndurumo lililopo katika barabara ya Sakina
– Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha.
Awamu ya pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny Kalupale, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa
Kilimanjaro na Arusha ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na
Wizara yake.
Serikali imelipa madeni
ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi cha
shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi
Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali inayodaiwa na
wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.
Naibu Waziri wa Wizara
ya Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na
badhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera
alipowasili katika Ofisi hiyo ili kuzungumza na watumishi wa Mamlaka
hiyo.
Hayo yamesemwa Mjini
Bukoba mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dok. Ashatu Kijaji
(Mb), wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa huo akiwa katika
ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala
wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Naibu Waziri wa Wizara
ya Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na watumishi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera kuhusu masuala ya kiutendaji
alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani humo.
Kijaji alisema kuwa
wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa
shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Shilingi bilioni 38,
watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai wengine wakilipwa
shilingi bilioni 24.
Meneja Mkuu wa Mamlaka
ya Mapato (TRA) Mkoani Kagera, Adam Ntoga, akiwasilisha taarifa ya utendaji
ya Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji
(Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani Kagera.
Amesema katika bajeti ya
mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1 kwa ajili ya
kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa madeni yote
yaliyohakikiwa.
Baadhi ya Maafisa wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera wakimsikiliza kwa makini Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumzia kuhusu uadilifu katika kazi na utoaji wa elimu
kwa mlipakodi baada ya Naibu Waziri huyo kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi
hiyo.
Aliiambia Jumuiya ya
Wafanyabiashara mkoani Kagera kwamba Serikali inatambua mchango wao mkubwa
katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia kuboresha
miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.
Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati)
akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Mkoani Kagera, alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo ambapo amewaasa kuwa
waadilifu katika kazi zao.
Alitoa wito kwa
wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao, kutoa
stakabadhi wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai stakabadhi
wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi hizo zinaonesha
kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.
Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati -walioketi) akiwa katika picha ya
pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera na
baadhi ya Maafisa Waandamizi katika Mkoa huo.
Akizungumza kwaniaba ya
Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Seif
Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna
inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.
Mwenyekiti wa
Wafanyabiashara Mkoa wa Kagera Seif Mkude (kulia) akielezea kuhusu utayari wa
wafanyabiashara wa Mkoa huo kulipa kodi wakati wa Mkutano kati ya
wafanyabiashara wa Mkoa huo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk.
Ashatu Kijaji (Mb) (katikati).
Alisema wafanyabiashara
wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa kikamilifu na kutekeleza
miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea kulipa kodi hizo ili
kujenga uchumi wa nchi.
Mfanyabiashara wa Mkoa
wa Kagera Taimur Manyilizo, akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo
wafanyabiashara Mkoani humo ikiwemo kile alichoeleza uwepo
wa taasisi nyingi zinazodai kodi nyingi ikiwemo OSHA, TFDA, Zimamoto
ambapo aliiomba Serikali iziangalie na kuzifanyia kazi.
Amewashauri kuendelea
kulipa kodi kwa hiari ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli huku akiishauri Serikali kuondoa kero ndogondogo zilizotolewa
na wafanyabiashara wakati wa mkutano huo.
Mfanyabiashara wa Mkoa
wa Kagera Taimur Manyilizo, akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo
wafanyabiashara Mkoani humo ikiwemo kile alichoeleza uwepo
wa taasisi nyingi zinazodai kodi nyingi ikiwemo OSHA, TFDA, Zimamoto
ambapo aliiomba Serikali iziangalie na kuzifanyia kazi.
Akizungumza kwa niaba ya
Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Deodatus Kinawiro, aliwahsa wafanyabiashara
hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze kunufaika na uwepo wa soko huru
katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda,
Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa Daraja la
Mto Momba linalounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe kutafufua fursa za kiuchumi
katika mikoa ya magharibi na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na
mifugo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo leo alipokagua ujenzi wa
daraja hilo na kuwahakikishia wananchi wa Wilaya ya Sumbawanga kuwa Serikali
imejipanga kuhakikisha daraja hilo linakamilika mwezi Agosti mwakani.
“Toeni ushirikiano unaostahili kwa
mkandarasi ili Daraja hili la Momba na madaraja madogo saba yanayojengwa katika
barabara ya Kasansa-Kilyamatundu yenye urefu wa KM 210.38 yakamilike kwa wakati”,
amesema Prof. Mbarawa.
Mafundi wakiendelea na kazi
ya ujenzi wa daraja la Kinambo lililopo katika
barabara ya Kasansa-Muze KM 31.90
wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa.
|
Amesisitiza nia ya Serikali ya kujenga
barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 na Stalike-Kilyamatundu-Mloo KM 500
kwa kiwango cha lami ili kuongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa mazao ya
kilimo na mifugo katika Bonde la Mto Rukwa kwenda maeneo mingine ya nchi.
Muonekano wa mitambo ya
kuchimbia nguzo za Daraja la Mto Momba unaounganisha mikoa ya Rukwa na Songwe.
|
“Wale wote ambao wamewekewa alama za
kubomoa nyumba zao ili kupisha ujenzi wa barabara nawaomba wafanye hivyo mapema
ili kuwawezesha wakandarasi kufanya kazi zao kwa uhuru na kuiwezesha TANROADS
kufanya usanifu wa kina”, alisisitiza.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara
Nchini (TANROADS) mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina, amemhakikishia Prof. Mbarawa
kuwa watamsimamia kikamilifu mkandarasi anayejenga Daraja la Momba na madaraja
madogo saba katika barabara ya Kasansa-Kilyamatundu KM 210.38 ili kazi ujenzi
huo ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la
Kwela Ignas Malocha, amewataka wananchi watakaopata fursa za ujenzi wa madaraja
hayo kuepuka vitendo vya wizi na hujuma kwa wakandarasi.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa
Kilymatundu mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mto Momba,
wilayani Sumbawanga.
Amesema kukamilika kwa Daraja la Momba
kuna manufaa mengi kiuchumi, kijamii kwa kuwa daraja hilo litawaunganisha
wakazi wa jimbo lake na mkoa wa Songwe na hivyo kuharakisha shughuli za
kimaendeleo.
Mmoja wa wananchi wa
kijiji cha Kilyamatundu kilichopo wilayani Sumbawanga akimkabidhi Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ushahidi wa picha za
miti iliyokatwa katika shamba lake kupisha mradi wa ujenzi wa Daraja la Mto
Momba, mkoani Rukwa.

