Habari Mpya

Habari Zote

Archive for October 2017

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amekagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na yakisasa itakayotoa huduma za usafirishaji katika  Ziwa Victoria.
Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Bw. Erick Hamissi,akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa(Wa pili kulia), hatua zilizofikiwa za ukarabati wa meli ya Mv. Clarius na Mv. Umojakatika Bandari ya Mwanza.

Akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Prof. Mbarawa, amewataka wafanyakazi wa Kampuni hiyo kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi ili kazi hiyo ianze mara moja na kukamilika kwa wakati.

“Mkandarasi ameshapatikana hivyo hakikisheni mnatoa ushirikiano na mnafanya uhakiki wa kimahesabu vizuri ili kazi hii ifanyike kwa gharama nafuu, ubora na muda mfupi”, amesema Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa, amekagua maendeleo ya ukarabati wa meli ya Mv. Clarias na Mv. Umoja ambapo ameeleza kuridhishwa kwake na hatua zilizofikiwa, na hivyo kuwataka MSCL kutafuta mizigo ya kusafirisha kutoka Bandari ya Mwanza kwenda Bandari  ya “Port Bell”, nchini Uganda.

“Kukamilika kwa meli kuwiane na kasi ya kutafuta mzigo mwingi ili meli hizi zifanye biashara wakati wote na kuhakikisha Kampuni yenu inapata mapato mengi yatakayowawezesha kujiendesha kwa faida”, amesisitiza Waziri Mbarawa

Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Erick Hamissi, amemhakikishia Prof. Mbarawa, kuwa wamejipanga kufanya ukarabati mkubwa wa meli za Mv. Victoria, Butiama na Liemba ili kuziwezesha meli hizo kufanya kazi katika ubora wake wa awali na kupunguza tatizo la usafiri katika ziwa Victoria na Tanganyika.

“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunazikarabati meli zetu zote ili ziwe katika ubora unaostahili wakati wote”, amefafanua Bw. Hamissi.

Katika kuhakikisha maendeleo ya kibiashara na kuichumi  yanafikiwa katika Ukanda wa maziwa makuu  nchini, Serikali imejipanga kuhakikisha inafufua usafiri wa meli za abiri na mizigo katika ukanda huo.
TUME ya uchaguzi imeahirisha uchaguzi katika kaunti za Kisumu, Siaya, Migori na Homa Bay.
Vituo vya kura katika baadhi ya maeneo tayari vimefungwa.

Kinyume na uchaguzi wa mwezi Agosti, katika vituo vya kupigia kura hakukuwa na foleni ndefu.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesusia uchaguzi huo na kuwataka wafuasi wake wasalie manyumbani

Uchaguzi huu unatokana na hatua ya Mahakama ya Juu kufuta uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti

UCHAGUZI NI VURUGU KENYE

HOSPITALI ya rufaa ya mkoa wa Tanga, Bombo, haina chumba cha kuwalaza wagonjwa mahututi (ICU) hali inayosababisha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa matibabu, hulazimsihwa kuwekwa katika wodi za wagonjwa wengine, wakiwa na mitungi ya mashine za gesi za kupumulia.
 
Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga, Bombo
Uchunguzi uliofanywa na Majira takribani mwezi mmoja katika hospitali hiyo ya rufaa inayopokea wagonjwa kutoka katika vituo vya afya na hospitali za wilaya nane zilizopo mkoani hapa, na kuthibitishwa na Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga (RAS) Injinia Zenna Said, Mganga Mkuu wa mkoa wa Tanga, Dk. Asha Mahita na Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. Jumanne Karia kwa pamoja walielezea jitihada za mkoa za kuhakikisha wanajenga chumba hicho.

Hospitali hiyo kongwe hapa nchini, imekuwa na tatizo hilo takribani miaka 7 sasa, kwa chumba hicho kukosekana ambapo awali walikuwa wakitumia chumba kimoja kabla ya kusitisha kualza wagonjwa, kikawa kinatumiwa na watoto wadogo lakini baadaye kikawa kinatumiwa na wagonjwa wanaotumia kadi za huduma ya Bima ya Afya, lakini sasa kinatumika kwa shughuli nyingine za hospitali.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Tanga, wamekuwa wakilalamikia hali hiyo wakieleza kwamba wagonjwa Mahututi kuwachanganya na wagonjwa wengine huku wakiwa na mitungi ya gesi ni kutowatendea haki, kwa kuwa wanaporuhusiwa ndugu kuona wagonjwa kunakuwa na msongamano mkubwa na kelele za hapa na pale za kufariji wagonjwa wengine.

“Nilishtuka nilipoingia wodi ya Galanosi kule kwa akina mama nilimkuta mke wa diwani wa Kirare, Saleh Mwagilo akiwa amewekewa mashine ya gesi huku akiwa mahututi, nilishangaa nilipouliza nikaambiwa hospitali haina chumba cha wagonjwa mahututi,” alisema Haruna Magembe aliyekuwa na mgonjwa katika wodi hiyo ya Galanosi.

Alisema kuwa licha ya kuwepo mgonjwa huyo katika wodi nyingine mbalimbali zimekuwa na wagonjwa mahututi wengi wanaochanganywa na wagonjwa wa kawaida haliambayo imekuwa ikileta tafsiri mbaya ya suala la viongozi wa mkoa kuwajibika katika kuhakikisha chumba hicho kinapatikana ili kuwawezesha wagonjwa hao kupata tiba stahili kwa mujibu wa taratibu na sera ya wizara ya afya.

Alipotafutwa diwani huyo kwa ajili ya kuelezea suala la mgonjwa wake huyo, hakuweza kupatikana lakini mtu wake wa karibu aliyejitambulisha kwa jina la Kasirani kasirani, alisema amemhamishia mkewe huyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako anaendelea na matibabu baada ya kulazwa takribani wiki mbili akiwa na mtungi wa oksijeni bila mafanikio.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo Katibu Tawala wa mkoa wa Tanga, Injinia Zena alikiri kukosekana kwa chumba hicho, lakini alisema kwa taarifa za jitihada zinazofanyika kupata chumba hicho, alimwelekeza mwandishi wa habari hizi akakutane na Mganga Mkuu wa mkoa Mahita ambaye atakuwa na majibu kuhusu kukosekana kwa ICU katika hospitali hiyo.

“Ni kweli lakini sisi kama mkoa tumekuwa na mipango mbalimbali ya kupatikana lakini nenda kwa Mganga Mkuu atakupa tumefikia wapi kuhusu kupatikana kwa ICU,” alisema Injinia Zenna.

Dk. Mahita alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kuwa ni kweli hawana ICU katika hospitali hiyo lakini wagonjwa wenye mahitaji hayo wamekuwa wakiwahudumia vizuri licha ya kukosa chumba kinachofaa kwa huduma hiyo na kwamba hawawezi kuwazuia watu wanaokuja kuwaona wagonjwa waliowachanganya na wagonjwa wengine.

Hata hivyo, Dk Mahita ambaye alisema pamoja na kukosa huduma hiyo hospitali hiyo katika kipindi cha hivi karibuni wameweza kuboresha huduma mbalimbali na kuhusu ICU wamekuwa na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanamaliza tatizo hilo baada ya kuomba mkopo kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

“Tumeomba mkopo NHIF kwa ajili ya ICU, lakini kwa sasa wagonjwa wanaokuja kwa mahitaji ya huduma ya ICU tunawapa huduma, tunachokosa ni eneo la kutolea huduma hiyo tu,” alisema na kuongeza “Hatuwezi kuwazuia watu wasiende kutazama wagonjwa wao waliokuwa na oksijeni, lakini ukitaka taarifa zaidi nenda kamuone Dk. Karia ambaye ni Mganga Mfawidhi wa hospitali, atakupa hadi sasa tumefikia wapi katika suala hilo,”.

Akizungumzia kuhusu hali hiyo Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Karia alisema kuwa ni kweli chumba hicho kwa sasa hakipo katika hospitali hiyo baada ya chumba kilichokuwa kikitumika zamani hakina mfumo wa kutumia gesi pamoja na vifaa vya ICU, hivyo wakaamua kuwachanganya wagonjwa wenye mahitaji hayo na wagonjwa wengine, lakini tangu mwaka 2013 wameanza ukarabati wa jengo ambalo litatumika kwa huduma hiyo.

Alisema chumba wanachokifanyia ukarabati sasa ili kitumike kuwa ICU ni kile kilichokuwa kikitumika kama chumba cha Upasuaji (Theatre) baada ya mradi wa KfW kutoa fedha za ujenzi wa chumba cha Upasuaji kipya kinachotumika sasa na kwamba sasa wanaendelea kutafuta fedha ili waweze kukamilisha katika kipindi kifupi kijacho.

“Ni kweli kile chumba cha mwanzo kilichokuwa kikitumika kama ICU hatukitumii tena na tunachanganya wagonjwa huko katika mawodi, lakini chumba kile kilikuwa hakina mfumo wa gesi, pia hakikuwa na vifaa vinavyohitajika kwa wagonjwa mahututi ikiwemo vitanda,” alisema Dkt Karia.

Aliongeza kusema kwamba katika bajeti yam waka 2017/2018 itatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ICU na kiasi cha shilingi milioni 231 ilitengwa mwaka 2016/2017 kwa jili ya kutengeneza mfumo wa gesi katika chumba hicho ambapo hospitali kwa kushirikiana na ofisi ya Katibu Tawala, imeanza kushughulikia suala hilo la gesi ambayo pia wataiuza katika hospitali nyingine baada ya kuanza kazi.

“Vile vile kuna vifaa vya msaada kutoka nchini Ujerumani Mwenyekiti wetu wa bodi ya Hospitali Zahra Noor kwa kushirikiana na kaka yake Habib Noor na baadhi ya wafanyabiashara wa hapa Tanga akiwemo Selemani Rahaleo, watasaidia hiyo ICU yetu ikianza kazi,” alisema Dkt Karia na kuongeza kwamba wameomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 560 kutoka NHIF.

Akizungumza na gazeti hili Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afy (NHIF) mkoani Tanga, Ali Mwakababu alisema ni kweli hospitali hiyo imeomba mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 560 kwa ajili ya ukarabati wa wodi ya akina mama na watoto pamoja na chumba cha magonjwa mahututi (ICU).

“Tutawapa mkopo wao huo, bahati nzuri mradi wao huo wa ICU umepitiwa hivi karibuni na Mwenyekiti wetu wa Bodi Mama Anna Makinda hivyo ni matumaini yetu kwamba watapewa wakati wowote fedha hizo ili kufanikisha suala hilo,” alisema Mwakababu na kuongeza kwamba mfumo wao hospitali hiyo inakopesheka kwa vile kwa mwezi huwa wanawalipa zaidi ya shilingi milioni 200 wanazotoa matibabu kwa wanachama wao.
SERIKALI inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.



Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na watumishi wengine wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga, alipofanya ziara ya kikazi kukagua namna Mamlaka hayo inavyokusanya kodi.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu kufanya juhudi ya kukusanya mapato ili azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kikamilifu itimie.

Ahadi hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.

Dk. Kijaji amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu kufanya juhudi ya kukusanya mapato ili azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kikamilifu itimie.
“Tunatambua changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema .

Alisema kuwa pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.

Dk. Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.

Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Jumbe Samson, alieleza kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba wanauhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Beatus Nchota alisema kuwa Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila wilaya hapa nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17 liweze kufikiwa.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo itahakikisha kuwa TRA inatimiza malengo yake ya kukusanya kodi na kumhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji kwamba watasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimetoa mkono wa pole kwa familia iliyopata ajali ya kuungua moto nyumba na kusababisha vifo vya watu wanne huko katika kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla  Mabodi wakati wa kuifariji familia hiyo amesema CCM Zanzibar imesikitishwa sana na tukio hilo kwani limegharimu maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwafariji ndugu na jamaa wa marehemu wa familia iliyopata msiba huo katika kijiji cha Fumba Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
 Dk. Mabodi alisema kwa niaba ya Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  anatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia hiyo na kuwasihi waendelee kuwa  na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha msiba huo.
“ Kupoteza watu  Wanne katika familia moja  ni jambo zito linalotia huzuni lakini tuendelee kuwa wavumilivu kwani Allah amewapenda zaidi na sisi tuliobaki tuendelee kuwaombea  dua ili wapate makaazi mema na kusamehewa madhambi yao”, alitoa nasaha hizo kwa maskitiko makubwa Dk. Mabodi.”
Mapema Sheha wa Shehia ya Fumba, Mohamed Suleiman alifafanua kuwa nyumba hiyo ilianza kuwaka moto majira ya saa 6:15 usiku Oktoba 21 mwaka huu, ambapo wananchi mbali mbali walianza juhudi za kuzima moto huo na kushindwa kuokoa watu waliokuwa ndani kwani uliku ni mkubwa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi  Akisalimiana na baadhi ya wananchi na viongozi mbali mbali walioudhuria katika msiba huo.
Suleiman alisema wakati juhudi za kuzima moto huo zikiendelea waliwasiliana na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar ambacho kilifika na kusaidiana na wananchi hao ambapo walizima moto huo na kukuta watu wanne tayari wamefariki dunia.
Akithibitisha tukio tukio hiloalisema chanzo cha moto huo ni hitilafu za umeme zilizoanzia katika waya wa jokofu (Friji) lililokuwa likifanya kazi wakati wa usiku.
Kamanda Nassir aliwataja watu waliofariki katika tukio hilo kuwa ni Bahati Ali Ameir (40), Sinawema Abdalla Ali, Hashim Abdalla Ali (6) na Latifa Mohamed Ali (8).

Alitoa wito kwa wananchi kujenga utamaduni wa kuzima vifaa vya umeme wakati wa usiku ambavyo havina umuhimu wa kutumiwa wakati huo ili kuepuka majanga yanayoweza kuhatarisha maisha ya watu.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amezungumzia umuhimu kwa wafanyakazi wote waliopata fursa ya kujenga reli ya kisasa (SGR) kufanya kazi kwa moyo na uzalendo mkubwa ili kuandika historia katika maendeleo ya Tanzania.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa kampuni ya Yapi Merkezi Abdullah Kilic, anayejenge reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam-Morogoro  yenye urefu wa KM 205 eneo la Soga, mkoani Pwani. 

Mbarawa amesema hayo alipokuwa anakagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), inayojengwa usiku na mchana kuanzia Dar es Salaam-Morogoro  yenye urefu wa KM 205 ambayo kwa kiasi kikubwa ameonesha kurizishwa na kasi ya ujenzi huo.
“Hii ni fursa kubwa ambayo mmeipata kujenga mradi mkubwa utakaocha historia katika nchi hii hivyo fanyeni kazi kwa bidii, weledi na uzalendo”, alisema.
Amewataka viongozi wa Shirika Hodhi la Rasilimali za Reli (RAHCO), kuwa katika eneo la mradi wakati wote ili kuhakikisha mkandarasi anapata ushirikiano wa kutosha na hivyo kuwezesha mradi kukamilika kama ilivopangwa.

Meneja Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Mhandisi Maizo Mgedzi, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, alipokagua ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam-Morogoro yenye urefu wa KM 205 eneo la Soga, mkoani Pwani, inayojengwa usiku na mchana.

Pia amemuagiza Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Edward Malima, kuhakikisha wanafunzi wa uhandisi wanapata nafasi ya kutosha ya kushiriki kwa vitendo katika ujenzi huo ili kuiwezesha nchi kuwa na wataalamu wa kutosha wenye uzoefu kwenye ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli.
“Ongezeni wahandisi wanafunzi katika mradi huu, nia yetu ni kupata reli lakini pia na wataalamu wengi katika ujenzi na uendeshaji wa reli”, alisisitiza.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akimpongeza mwanamke anayeendesha mtambo wa kutengeneza tuta la reli ya kisasa (SGR), Miriam Juma alipomkuta saa 4 za usiku akichapa kazi katika eneo la Soga, mkoani Pwani.

Kwa upande wake Malima, amempongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kufanya ziara ya kustukiza usiku ambayo imechochea hamasa kwa wafanyakazi na mkandarasi na kuahidi  kumsimamia mkandarasi kikamilifu ili mradi huo ukamilike kwa wakati na uwiane na thamani ya fedha.
Muonekano wa Mitambo ya kisasa inayojenga Reli ya Kisasa (SGR), kutoka Dar es Salaam-Morogoro yenye urefu wa KM 205 eneo la Soga mkoani Pwani, inayojengwa kwa saa 24.
Takribani shilingi trilioni 2.8 zinatarajiwa kutumika kkstika ujenzi wa reli hiyo awamu ya kwaza kati ya Dar es Salaam na Morogoro yenye urefu wa KM 205 itakayowezesha treni ya umeme yenye kasi ya KM 160 kwa saa kupita na hivyo kuhuisha mfumo wa usafiri wa reli hapa nchini.


MKUTANO wa Saba wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) umefanyika leo tarehe 19 Oktoba, 2017 mjini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Mkutano huo umetanguliwa na ule wa awali ngazi ya Wataalamu wa Masuala ya Fedha, Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Majeshi na Waratibu wa Nchi (ICGLR National Coordinators) pamoja na Mawaziri wa Mambo ya Nje.
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augustine Mahiga
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Augustine Mahiga, ametoa ujumbe akimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli mkutanoni hapo.

Mkutano huu umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali na Wawakilishi wao kutoka nchi za Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Kenya, Rwanda, Sudani, Sudani Kusini, Tanzania, Uganda na Zambia ukiwa na ajenda kuu ya kupitia na kujadili hali ya Siasa, Ulinzi na usalama katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu hasa katika nchi za Burundi, Kongo, Jamhuri ya Kongo, Afrika ya Kati na Sudani Kusini.

Ajenda zingine zilikuwa ni pamoja na kupokea taarifa ya Michango ya nchi wanachama ambapo Kuhusu hali ya usalama katika Nchi hizo kwa ujumla iliripotiwa kuwa inaendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa isipokuwa nchini DRC ambapo kwa sasa operesheni zinaendelea kufanywa na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC- MONUSCO (FIB) dhidi ya vikundi vya waasi  ndani na nje ya DRC.

Mkutano huu ulifuatiwa na Mkutano wa Nane Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mpango wa Amani na Usalama katika Maziwa Makuu (8th Regional Oversight Mechanism for the Peace, Security and Cooperation Framework of the DRC and the Region).


Taasisi zingine za kimataifa zilizoalikwa kwenye Mikutano hii ni pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo ujumbe wake uliongozwa na Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax.
AFISA  Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Hamis  Lissu  ameahidi kutatua kero zote zinazowakabili baadhi ya wamiliki wa Shule Binafsiinafsi wa mkoa ikiwemo ya  tozo kubwa za biashara zinazotozwa shule hizo .
 
Afisa elimu wa mkoa wa Dar es salaam akizungumza na washiriki wa mkutano  uliowakutanisha wamiliki wa shule binafsi mkoa wa Dar es Salaam
Pia amewaomba wamiliki wa shule hizo kipindi cha likizo wajitolee kuwafundisha masomo ya sayansi wanafunzi wanaotoka shule za serikali kwa kuwa wana walimu wengi wa masomo hayo.

Ameyasema hayo  leo alipokuwa akifungua Mkutano Maalumu uliowakutanisha wadau mbalimbali na wamiliki wa shule zilizopo jijini hapa.

Amesema wamiliki wa shule hizo pamoja na shule zao wanapaswa watambaue huduma wanazopewa  ni stahiki  hivyo ni sawa wanazopatiwa shule za Serikali.
 
Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa shule binafsi (TAMONGSCO), Charles Totela Akizungumza 
“Natamani kuziona shule zote binafsi zikiwa zinazoongoza kutokuwa na changamaoto zozote kwani tunatambua mchango wa uwekezaji hapa nchini,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi nchini (TAMONGSCO), Charles Totela ameishukuru Serikali ya mkoa huo kwani imekuwa ikiwapa ushirikiano wa kutosha.

Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali ya mkoa huo kuwaundia dawati la pamoja litakalowakutanisha viongozi wote wa shule binafsi, za serikali na watendaji wao ili waweze kukaa pamoja na kujadiliana baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa hazifanyiwi kazi.
 
Miongoni mwa wamiliki wa shule binafsi pamoja na wawakilishi waliofika kwenye mkutano  huo 
Naye Mkurugenzi wa Shule za Al-Muntazir,  Mahmood Ladack amewashukuru wamiliki wa shule hizo kwa kuhitisha mkuatano huo ambao anataraji utakuwa na manufaa makubwa kwao na taasisi wanazosimamia katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.


UONGOZI wa mkoani Simiyu umembadilishia majukumu  ya kazi Tabibu, Laurent Biyengo na kuwa mlinzi katika lango kuu la kuingilia hospitali kutokana na kushindwa kuyamudu majukumu ya kitabibu.
 
Waziri wa Afya ,Ustawi wa jamii,Wazee,Jinsia na Watoto,Ummy Mwalimu
Biyengo ambaye anadaiwa kushindwa kuingia kazini na kwenda kulewa saa za kazi alipokuwa zamu septemba 27 mwaka huu na kusababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John kutoka kwa kushindwa kupatiwa huduma.

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika kutoka ndani ya hospitali hiyo na kuthibitishwa na baadhi ya matumishi wenzake zinaeleza kuwa tangu aanze majukumu yake hayo mapya sasa ni kipindi cha majuma mawili akilinda getini.

Wakizungumza na hivi karibuni, baadhi ya madaktari hao walisema kuwa adhabu aliyopewa ni ya haki kutokana na kitendo alichokifanya ambacho kinakiuka maadili ya taaluma yao ya utabibu.

“Huyu mwenzetu amepata adhabu ya haki na hii wamemsaidia sana maana alipaswa kufukuzwa kazi haiwezekani umepangwa kutoa huduma za kitabibu katika hospitali kubwa kama hii halafu unakwenda kulewa na kusababisha wagonjwa kutopata huduma, nikukiuka maadili ya kitabibu,”alisema Daktari mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Walisema kuwa kitendo alichokifanya kimewapotezea imani kwa wagonjwa wanaofika kupata matibabu katika hospitali hiyo, huku wengine wakitumia lugha za kuwakejeli na kuwadhihaki jambo ambalo linawashusha molali ya kazi.

Kwa mujibu wa habari za kuaminika kutoka chanzo ambacho kilifika katika hospitali ya wilaya ya Maswa na kumshuhudia daktari huyo akiwa katika lango kuu la kuingilia hospitalini hapo, na kumwona  akufungulia magari na pikipiki zinazoingia na kutoka sambamba na watu wanaokuja kupata matibabu hata hivyo jitihada za kuongea naye hazikuzaa matunda baada ya kugoma kuongea.

Akizungumzia suala hilo Mkuu wa wilaya ya Maswa Dk. Seif Shekalaghe alikiri kwa daktari huyo kubadilishiwa majukumu ya kazi na kusisitiza kuwa hiyo ni hatua ya awali walizozichukua kutokana na kitendo alichokifanya.

“Nimeambiwa ya kuwa amebadilishiwa majukumu ya kazi kutoka kutoa huduma za kitabibu na kuwa mlinzi lakini nahisi kuna hatua zaidi ya hiyo inatakiwa kufanywa nipeni muda tutapata majibu sahihi,”alisema Shekalaghe.


Kufuatia tukio hilo,Waziri wa Afya ,Ustawi wa jamii,Wazee,Jinsia na Watoto,Ummy Mwalimu alimwelekeza Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Dk. Zainab Chaula kumchukulia hatua.
MAKAMISHINA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wametembelea eneo la Njedengwa Mjini Dodoma yanapojengwa majengo ya makao makuu ya NEC na kuelezea kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.
 
Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R), Simistocles Kaijage, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima na Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Yohana Mashausi wakiwaongoza makamishna wa NEC kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa majengo ya ofisi za NEC jana. Mradi huo unafanyika katika eneo la Njedengwa Mjini Dodoma. (Picha na Abdulwakil Saiboko)
Akizingumza mara baada ya ziara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji (R) Semistocles Kaijage, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema kwamba maendeleo ya ujenzi yanaridhisha na ujenzi utakamilika kwa muda uliopangwa.
 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R), Simistocles Kaijage (wa pili kulia) akifurahia jambo na Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Bw. Yohana Mashausi (kulia) baada ya kupewa maelezo ya mradi wa ujenzi wa majengo ya ofisi za NEC jana wakati makamishana wa NEC walipotemdelea mradi huo. Mradi huo unafanyika katika eneo la Njedengwa Mjini Dodoma na unatarajiwa kukamilika mwakani. (Picha na Abdulwakil Saiboko)
Kailima amesema kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ambao unajumuisha majengo matatu utakamilika mwezi Julai, mwakani.
“Mradi huu una awamu mbili za ujenzi lakini utatoa majengo makubwa matatu, jengo la kwanza ni jengo kubwa la ofisi litakua na ghorofa nane, la pili ni jengo la ukumbi wa kutangazia matokea ambao utakua na uwezo wa kuchukua watu 800, uchaguzi mkuu ujao wa 2020 tunatarajia kutangaza matokeo kwenye ukumbi huu na pia kuna jengo la maghala ya kuhifadhia vifaa vya uchaguzi,” amesema Kailima.

Aliongeza kusema “Mradi huu unakwenda vizuri kwa sababu gharama yake ni takribani shilingi bilioni 13, awamu ya kwanza itagharimu bilioni 11/- ambayo itahusisha ujenzi wa jengo la ofisi, pia itajumuisha ujenzi wa sehemu ya jengo la kituo cha kutangazia matokeo na maghala.

Awamu ya pili ambayo itagharimu bilioni 2/- itakua imekamilika mwaka 2018. Kuanzia mwenzi Agosti 2018 Tume tutaanza kuhamia Dodoma,” amesema.
 
Kutoka kushoto ni Mhandisi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Yohana Mashausi akitoa maelezo ya mradi wa ujenzi wa ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa makamishna wa  tume hiyo walioongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R), Simistocles Kaijage, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima na Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid. Ujenzi huo unaoendelea katika eneo la Njedengwa Mjini Dodoma unatarajiwa kukamilika mwakani. (Picha na Abdulwakil Saiboko).
Akizungumzia suala la bajeti ya ujenzi wa majengo hayo, Kailima amesema fedha zipo na zitakua zikitolewa kadri zitakavyohitajika.
Mwanzoni akiwatembeza makamishna wa tume kwenye eneo la mradi, Mkandarasi Msimamizi kutoka Wakala wa Majengo (TBA), Mhandisi Yohana Mashausi amesema ujenzi huo umechukua muda mrefu kwenye eneo la msingi kwa kuwa eneo hilo lina ardhi yenye mwamba mgumu sana.


Mhandisi Mashausi amesema kwamba TBA pia imechukua tahadhari kubwa katika ujenzi wa msingi imara kwa kuzingatia hali ya kijogirafia ya Dodoma ambako kuna hatari ya kukumbwa na matetemeko ya ardhi.
SERIKALI imesema ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA),   unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa sasa umefika zaidi ya asilimia Tisini.
Meneja Miradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mhandisi Mathew Ndossi, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa (Mb), (Kushoto), upanuzi wa maegesho ya ndege uliofanyika uwanjani hapo. 
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elius Kwandikwa, mara baada ya kukagua ukarabati wa jengo la kupumzikia abiria na upanuzi wa maegesho ya ndege katika uwanja huo leo mkoani Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elius Kwandikwa (Mb), akikagua maboresho ya mfumo wa majitaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za ukarabati wa uwanja huo.
"Nimeridhishwa na ukarabati unaoendelea katika uwanja huu na nafikiri mmejionea wenyewe kazi inaendelea vizuri, hivyo naamini kutokana na hali hii kazi itakamilika hivi karibuni, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elius Kwandikwa (Mb), akikagua maboresho ya mfumo wa majitaka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alipofika uwanjani hapo kujionea hatua zilizofikiwa za ukarabati wa uwanja huo.

Naibu Waziri huyo amefafanua kuwa ukarabati huo  ambao pia umehusisha maboresho ya mfumo wa maji taka unalenga kuleta tija kwa mkoa huo na Taifa kwa ujumla kutokana na kuwepo ongezeko la abiria, huduma za kijamii na kibiashara.
Mafundi wakiendelea na ukarabati katika jengo la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Ukarabati huo umefika zaidi ya asilimia Tisini na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kukarabati na kujenga viwanja vya ndege nchini ili kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wananchi wake lengo likiwa ni kuchochea fursa za kiuchumi ambazo zitasaidia kulipeleka Taifa katika uchumi wa kati.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mheshimiwa Elius Kwandikwa, akifafanua jambo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Arusha, Mhandisi Johny Kalupale, alipokagua barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1) na Barabara ya Mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass KM 42.4) mkoani Arusha.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa KIA, Mhandisi Mathew Ndossi,  amesema kuwa maegesho yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kuegesha jumla ya ndege kubwa 11 kwa wakati mmoja badala ya 6 zinazoegeshwa sasa.
Ameongeza kuwa abiria wanatarajiwa kuongezeka kutoka laki nane kwa mwaka hadi kufikia milioni moja na laki mbili mara baada ya kukamilika kwa uwanja huo.
Muonekano wa Barabara ya Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha, ambayo imekamilika kwa kiwango cha lami. Kukamilika kwake kumesaidia kupunguza ajali na msongamano katika eneo hilo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua barabara ya Sakina - Tengeru (km 14.1) na barabara ya mchepuko ya Arusha (Arusha Bypass km 42.4) ambapo amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya Sakina - Tengeru  ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na wageni wanaoingia katika mkoa huo kwani kumepelekea  kupungua kwa  ajali na msongamano wa magari  katika eneo hilo.

Ametoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara  na kutunza mazingira yanayozunguka barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Muonekano wa Daraja la Ndurumo lililopo katika barabara ya  Sakina – Tengeru (KM 14.1), mkoani Arusha.

Awamu ya pili ya mradi huo sehemu ya barabara ya mchepuo ya Arusha (Arusha Bypass), inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajiwa kukamilika mwakani na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 67.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Arusha Mhandisi, Johny Kalupale,  amemhakikishia Naibu Waziri huyo kufanya kazi kwa ubora na kwa weledi ili kutimiza malengo ya Serikali ya kuwajengea wananchi miundombinu bora na ya kisasa.


Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro na Arusha ambapo amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -