Habari Zote
Na hapo ndipo hutimia
neno la kitaalamu lisemalo: `life is a process’ au maisha ni mchakato, hatua.
Laibai Kallaghe haisau hatua za
maisha yake kutoka wazo la biashara ya kutengeneza na kuuza mabegi ya shule
aliyoyatengeneza kienyeji kwa kutumia vipande vya makasha (maboksi) zaidi ya miaka 50 iliyopita
huko Korogwe mkoani Tanga hadi kuwa Mkurugenzi mtendaji katika miaka ya hivi
karibuni.
![]() |
| Mkuregenzi wa SKUVI, Laibai Kalaghe (Mwenye shati jeupe kulia,) akiteta jambo na muasisi wa vikundi vya SKUVI Mwenyekiti mtendaji wa IPP Dk. Regnard Mengi (kushoto). |
Kwake yeye, biashara huanza na wazo kisha kulichakata kwa kutumia
juhudi zako binafsi kwasababu unalipenda wazo hilo na lazima uishi kwalo ili
kufikia malengo ya wazo hilo.
Kwa msingi huyo, anasema yeye si mtu mwenye kuzembea wazo lazima
alifuatilie na bila kukata tama hata kama zitajitokeza tambo ambazo huweza
kuangusha wazo lake.
Kallaghe alianza wazo la biashara tangu akisoma shule ya msingi
huko kijijini kwake Korogwe baada ya kubaini kuwa katika shule alimokuwa akisoma
kuna hitaji la mabegi kwa wanafunzi wenzake.
Hiyo ikamsukuma kutafuta maboksi ya karatasi ngumu, kuyaunda na
kupata mabegi ambayo alianza kuwauzia wanafunzi wenzake shuleni hapo na shule
za jirani baada ya kuvutiwa na mabegi hayo.
Baadaye aliogundua kwamba mabegi hayo ya makasha yanahitaji
kuongezewa kitu fulani, kuyafanya yapendeze zaidi na kuongezeka thamani. Yeye
aligundua kwamba ili mabegi hayo yapendeze, kupendwa zaidi na kuongezeka
ayapambe kwa nje kwa kuzungusha vipande vya magazeti ya kichina aliyopatiwa na
marafiki zake waliokuwa Jijini Dar es Salaam.
Ubunifu wake huo ulimsaidia kuongeza kipato na kufanikiwa kupata
mtaji wa kuanzisha biashara nyingine ya kuuza bidhaa ndogondogo kama vile
mbogamboga, aliyoendelea nayo hadi ilipoanza elimu ya sekondari katika kituo
cha elimu ya watu wazima, Korogwe.
Yungali yupo sekondari, anasema aliendelea na biashara yake hiyo
na kufanikiwa kugawa mtaji kwa kuanzisha biashara ya kuuza peremende kutoka
Kenya zilizojulika kama BigG na sigara kwa njia ya uchuuzi. Aliuza sana wakati
wa sherehe kwa kutembea hadi huko hasa wakati wa usiku kwenye muziki maarufu
kama disko hadi mwaka 1979 alipohitimu elimu ya sekondari huku akiendelea na
biashara zake.
Kallage alihamia jijini Dar es Salaam mwaka 1984 na kujiunga na
chuo cha ufundi Dar es Salaam (DIT) kwa kozi ya kuu ya uhandisi (General Course
Engeneering) katika fani ya uchoraji.
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, alijiunga na Chuo cha Ufundi Stadi
(VETA) katika chuo cha Tanzania Motor Service kilichopo cha mkoani Arusha na
kupata cheti cha Motor Cycle technical daraja la kwanza na baadae elimu
mbalimbali ya ujasiriamali.
“Pia nilifanikiwa kusoma stashahada ya elimu ya usimamizi wa
biashara kwa ujasiriamali wangu niliweza kusoma na kufanya kazizangu, saa kumi
na moja jioni nafunga kazi na kuelekea darasani hadi saa tatu usiku…wengi
waliniona kama anacheza kwa kuwa mtu anawezaje kusoma huku anajishughulisha na ujasiriamali,”alisema.
Mwaka 1995 alianza ufundi wa magari mtaani. Alikuwa hana uhakika
wa kupata kazi, jambo lililomsukuma kubuni njia ya kupata kazi.
Anasema aliamua kupanga makopo matupu ya oili pembeni mwa barabara
ya zamani ya Bagamoyo ili kuwavuta watu, hasa walioharibikiwa na magari. “Ndipo
siku moja, raia mmoja wa kigeni, akaona yake makopo na kushuka kutoka ndani ya
gari.
Kisha nilimsogelea na kugundua kuwa gari yake ilikuwa na hitilafu
ilisababisha isiwake, niliitengeza na kulipwa pesa, ambayo kwangu ilianza kuwa
mtaji,”alisema.
“Baadae Dk. Reginald Mengi alitangaza kukutana na vijana kwa hiari
kwa kauli mbiu yake aliyoiita `NIFANYE NINI?’ ambayo ni fursa. Alifanya nao
mkutano kwa dhamira ya kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri wenyewe na kutoa
fedha kwa vikundi 550 vya Shujaa wa Kupiga Vita Umasikini (SKUVI) yeye akiwa
kikundi namba 141 na kila kikundi kilipatiwa Sh.25,000.
Anasema aliamua kwenda Kariakoo kununua mashine ya kuchaji betri
za magari na kwa kujiunga na mwenzake mmoja ili tufanye biashara pamoja.
“Wakati huo umeme ulikuwa bado haujasambaa maeneo mengi hivyo
nilikuwa nauza oil na kuchaji betri ya magari, baada ya faida na nikaenda
kununua mashine za uchomeleaji” Kwa mtaji huo walifanikiwa kuanzisha kituo cha
kutengeneza magari (gereji), kununua mitungi ya gesi na kupaka rangi magari na kupokea
oda kwa watu mbali mbali.
Wakabuni utengenezaji wa matoroli kwa ajili ya kusambazia maji na
wanaofanya usafiKutokana na kukua kwa biashara hiyo baadhi ya benki kama
Baclays na Akiba walimuamini na kumkopesa mtaji ambao ulimuwezesha kuteneneza
matokoli hayo ya aliyoyapeleka kwenye maonesha ya biashara sabasaba, na
kufanikiwa kukuza mtaji.
Kallaghe ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Skuvi 141
inayotamba kwa jina la Mr. Oil anasema alianza kujenga mahusiano ya kibiashara
kwa kushirikia maonyesho ya biashara nchini China ambako alijifunza mbinu
mbalimbali ya biashara yake ya uchomeleaji wa kisasa.
Ziara hizo zilimpa nafasi ya kujuana na watu mbalimbali ambao hadi
sasa anashirikiana nao, yeye akiwa sehemu ya wakala wa kuuza bidhaa kutoka
nchini humo, huku yeye akiagiza na kuuza katika soko la ndani.
Katika taasisi yake ya SKUVI ameweza kuwafundisha vijana zaidi ya
20 kwa kazi hiyo ya uchomeleaji ambao wengi wao kwasasa wanajitegemea na kuwa
tegemeo
kwa familia zao. Pia ni mwalimu wa ujasiriamali.
Juhudi hizo zimemfanya kuendesha maisha yake, kumiliki gari,
nyumba, kusomesha watoto hadi elimu ya chuo kikuu. Pia Kujenga mahusiano
makubwa na kampuni za ndani na watu mbalimbali. Anashauri vijana na watu
wengine, kuwa wabunifu, kutumia mawazo yao vizuri na kufanya kazi bila kukata tamaa.
PIA UNAWEZA SOMA ZAIDI HAPA
WATU
40 wa Kitongoji cha Isumbi katika Kijiji cha Igung’hwa Kata ya Kinaga katika
Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga, wamelazwa katika Hospitali ya
Wilaya hiyo baada ya kudaiwa kula kiporo na mboga za majani aina
ya mgagani.
Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Kinaga, Paul Damasi alisema wananchi waliolazwa katika
Hospitali ya Mji wa Kahama ni wale waliokula kiporo cha ugali na mboga za
majani aina ya mgagani waliouita “mchicha.”
Aliyasema
hayo juzi wakati akizungumza na wananchi katika msiba uliotokea nyumbani kwa
Salum Manyanda na kuongeza kuwa asilimia kubwa ya watu waliougua ghafla baada
ya kula chakula hicho ni wanawake.
Ofisa
Mtendaji wa Kata huyo alisema tukio hilo lilitokea juzi saa tano asubuhi baada
ya waombolezaji kula chakula kilichobakia jana ya siku hiyo huku akieleza kuwa
wote waliougua ghafla walikimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Kahama
kupatiwa matibabu.
“Idadi
ya watu haijafahamika ila nimepewa taarifa kuwa ni zaidi ya wakinamama arobaini
ndiyo waliokimbizwa katika Hospitali ya Mji wa Kahama, msiba ulitokea Novemba
14, kama unavyojua vijijini bado kuna ile tabia ya msiba unapotokea akinamama
wanapika chakula nyumbani kisha wanapeleka msibani.
SPIKA
wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori wanapokuwa bungeni,
badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na maswali kutoka kwa wabunge.
Ndugai
alitoa onyo hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu baada ya kuwataja
baadhi ya manaibu ili wajibu maswali lakini walishindwa kusimama kwa kuonyesha
hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa na wabunge.
“Waheshimiwa
mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana mnashindwa kusikiliza
kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite katika kusikiliza,” alisema
Ndugai.
Kiongozi
huyo alianza na naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ambaye
alimtaka ajibu swali la nyongeza la Mwantumu Dau Haji (viti maalum - CCM)
ambalo lililenga katika suala zima la upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo
cha umwagiliaji.
Kabla
ya swali hilo, tayari mbunge huyo alishauliza swali la msingi ambalo
lilielekezwa ofisi ya Makamu wa Rais na lilijibiwa na naibu waziri wa wizara
hiyo, Kangi Lugola likihusu masuala la mabadiliko ya tabia nchi.
Aweso
alisimama asijue nini cha kujibu huku akiendelea kutazamana na Spika Ndugai kwa
sekunde kadhaa ndipo akaamuliwa kuketi kwa kuwa alikuwa hajui swali gani
liliulizwa.
“Tatizo
lenu mawaziri hamsikilizi kinachoendelea ndani ya Bunge, mnapiga stori tu. Haya
naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais okoa jahazi hilo,” alisema Ndugai.
Baada
ya maswali kadhaa kupita aliwataka naibu mawaziri ofisi ya Rais (Tamisemi),
Joseph Kakunda na Joseph Kandege kujibu swali la nyongeza kuhusu umaliziaji wa
majengo ambayo yanaanzishwa na wananchi.
“Haya
naibu mawaziri Tamisemi, Josephat Kandege naomba ujibu swali hilo. Kama
hujajipanga naomba mwenzako Joseph Kakunda ajibu, jamani ndiyo haya niliyosema
wapo hapa tu lakini wanapiga stori na hawasikilizi kinachoendelea,” alisema
spika.
Ndugai
aliwaonya pia wabunge kutozungumza na waziri mkuu na kumtaka kiongozi huyo wa
shughuli za Serikali kuzungusha macho ili kuona namna ambavyo wabunge walikuwa
wamesimama na kutaka kuuliza maswali kuhusu maji.
“Mheshimiwa
waziri mkuu, naomba hao wanaozungumza na wewe wakuache kwanza, hebu geuka nyuma
na uangalie pande zote uone namna ambavyo wabunge wamesimama kutaka kuuliza
maswali kuhusu maji majimboni kwao, Serikali iangalie jambo hili,” alisema.
Wakati
huo spika aliitaka Serikali kutafakari namna ambavyo imekuwa ikitoa maagizo na
amri kila wakati kupitia mabaraza ya madiwani akisema siyo afya na haijengi.
Alikuwa
akitolea majibu mwongozo ulioulizwa na mbunge wa Babati Mjini (Chadema),
Pauline Gekul kuhusu mpango wa Serikali kuagiza wananchi kuendelea kumalizia
majengo ya zahanati, maabara na madarasa waliyoyaanzisha.
“Ndugu
zangu Serikali, anachokisema mbunge ni sahihi maana sasa imekuwa ni kero kubwa,
hebu angalieni jambo hilo kwani kila mahali ni maagizo maagizo na hata tukienda
kwenye baraza la madiwani utasikia kuna ajenda ya kudumu ambayo ni maagizo, hii
inakera jamani,” alisisiza Ndugai.
Pia,
aliwataka viongozi kuangalia namna bora ya kufanya ili kufikisha ujumbe kuliko
kuagiza kila mara ambako kunaondoa imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Hata
hivyo, alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya viongozi kujiona kama miungu
watu na wanaamini kuagiza kila wakati kwa kutumia amri ndiyo itakuwa maendeleo
wakati si kweli.
SIKU
mbili zikiwa zimepita tangu Dk Louis Shika kuelezea siku 28 za mateso
aliyoyapata nchini Urusi, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo wakati huo,
Patrick Chokala amefichua siri jinsi walivyomsafirisha kijasusi ‘bilionea huyo
wa nyumba za Lugumi’ kurudi Tanzania.
Balozi
Chokala aliyekuwa Urusi kati ya mwaka 2002 na 2008 katika kipindi ambacho
sakata la utekwaji wa Dk. Shika lilijitokeza, amethibitisha kuwa ni kweli
Mtanzania huyo ni daktari na kwamba ni kweli amewahi kutekwa.
Dk.
Shika anatuhumiwa kuvuruga mnada wa majumba ya mfanyabiashara maarufu, Said
Lugumi uliofanywa na kampuni ya Yono baada ya kufika bei ya kuzinunua nyumba
hizo tatu kwa Sh3.2 bilioni, lakini akashindwa kutimiza sharti la kulipa
asilimia 25 ya fedha hizo.
Baada
ya kushindwa kulipa kulisababisha awekwe rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi
Dar es Salaam kwa siku sita hadi alipoachiwa kwa kujidhamini mwenywe Novemba 14
na kutakiwa kuripoti kila siku.
Mara
baada ya kutoka polisi kwa dhamana, Dk Shika ambaye anaishi nyumbani kwake
Tabata Mawenzi alieleza mambo mbalimbali ikiwamo kutekwa na kuteswa akiwa Urusi
Juni 2004, ikiwa ni pamoja na kukatwa vidole viwili mkono wa kushoto na kimoja
mkono wa kulia.
Pia
alieleza jinsi alivyofanikiwa kuwatoroka watekaji hao.
Katika
mahojiano na gazeti hilo Balozi Chokala alisema analikumbuka vizuri tukio la
kutekwa kwa Dk. Shika na jinsi ubalozi ulivyomsaidia asipatwe na kadhia kubwa
zaidi. “Ni kweli huyo jamaa ni daktari wa binadamu. Alisoma Chuo Kikuu cha
Lumumba kilichopo Moscow, Urusi,” alisema Balozi Chokala.
Alisema
kutokana na upekee wa yaliyomsibu Dk. Shika, ubalozi ulilazimika kuingilia kati
ili kunusuru maisha yake.
Alisema
Dk. Shika alitekwa na majambazi waliokuwa wanataka fedha ambazo yeye mwenyewe
(Dk. Shika) alikuwa anajigamba kuwa nazo na kuwashawishi watekaji hao
kumfuatilia. “Majigambo ya kumiliki fedha nyingi hajayaanza leo.
Tangu akiwa
Urusi alikuwa anasema anamiliki fedha nyingi. Watu walimuamini kwa sababu
alikuwa daktari anayetambulika, matokeo yake alitekwa,” alisema Chokala, ambaye
amewahi kuwa mwandishi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Balozi
huyo alisema baada ya kufanikiwa kuwatoroka majambazi hao ambao baadaye
walikamatwa na polisi nchini humo kisha kufunguliwa mashtaka, Dk. Shika
alipelekwa hospitali kwa matibabu akiwa amepoteza vidole kadhaa vya mikono yote
miwili.
Alisema
majambazi hao walimtesa kwa muda mrefu kwa kuwa mpaka anapatikana vidole hivyo
vilikuwa vimeanza kuoza.
“Walimshikilia
kwa muda mrefu kwa kuwa walihitaji fedha ambazo Dk. Shika hakuwa nazo,”
anakumbuka balozi huyo aliyestaafu mara baada ya kurudi nchini.
Alisema
baada ya ubalozi kupewa taarifa zake, ulifuatilia na kugundua kwamba alipelekwa
nchini humo na Wizara ya Afya, na alikuwa amelipiwa kila kitu ikiwa ni pamoja
na tiketi ya ndege.
Wakati
anatekwa, alisema Dk. Shika alikuwa ameshahitimu lakini hakuwa na nauli ya
kurudi nyumbani, hivyo akawa anahangaika kupata nafasi ya kuendelea na shahada
ya uzamili. “Tulipowasiliana na wizara walithibitisha kuwa ni mtu wao.
Tuliandaa utaratibu wa kumrudisha bila yeye kujua kwa sababu hakuwa anataka
kufanya hivyo,” alisema.
Akiwa
anaendelea kuhudumiwa, ubalozi ulimuandalia safari ya kurudi bila yeye kufahamu
kuepuka asitoroke. Balozi Chokala alisema ilikuwa ni lazima Dk. Shika arudishwe
kuepusha janga jingine linaloweza kumkuta endapo angeendelea kuishi nchini
humo. “Kujirudia kwa tatizo kama hilo kungeupa ubalozi lawama. Hatukutaka
kujiweka kwenye nafasi hiyo,” alisema.
Baada
ya mipango yote kukamilika, askari wa ubalozini walimpeleka uwanja wa ndege na
kumkabidhi kwa wahudumu wa ndege iliyokuwa inakuja Tanzania wakiwaelekeza
wasimshushe popote isipokuwa Dar es Salaam ambako Wizara ya Afya ilikuwa
inamsubiri.
Mpango
huo ulitekelezwa kama ulivyopangwa na wizara ikathibitisha kumpokea mtumishi
wake huyo ambaye balozi Chokala anasema alipewa nyumba na akawa anaendelea na
majukumu yake. “Akiwa Urusi, nilielezwa kuwa alikuwa ana matatizo ya kijamii
ambayo yaliendelea kumuandama hata aliporudi. Nasikia kuna wakati alienda kwao
na hakurudi tena kazini,” alisema.
Kuhusu
Dk. Shika kuwa ni Rais wa kampuni ya Lancefort aliyoianzisha akiwa Urusi ambayo
Serikali ya nchi hiyo ilitilia shaka mwenendo wake, hivyo kuifuatilia, Balozi
Chokala alisema hafahamu chochote.
MBUNGE
wa Singida Mashariki (Chadema), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amefanyiwa upasuaji wa 18.
Upasuaji
huo ulifanyika jana katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako Lissu
anaendelea na matibabu tangu Septemba 7, baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi
ya 30 akiwa katika makazi yake, area D mjini Dodoma.
Akizungumza
na gazeti la Mwananchi kwa simu, kaka yake Lissu, Alute Mughwai alisema, “Lissu
leo (jana) amefanyiwa upasuaji ambao ulianza asubuhi na umemalizika salama.
Nimeambiwa muda mfupi uliopita (ilikuwa saa 9.32 alasiri wakati akizungumza na
Mwananchi) kuwa ameshatoka chumba cha upasuaji.”
Alute
alisema, “Nimeambiwa upasuaji ulikwenda vizuri na sasa atapaswa kupumzika kama
siku nne kisha ataendelea na mazoezi kama kawaida.”
Ingawa
Alute hakueleza huo ni upasuaji wa ngapi, Oktoba 17 mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari alisema Lissu alikuwa
amefanyiwa upasuaji mara 17 hivyo kama hakufanyiwa mwingine huo wa jana utakuwa
ni wa 18.
“Lissu
mpaka sasa amefanyiwa upasuaji mkubwa mara 17, ameongezewa damu nyingi kuliko
mgonjwa yeyote aliyewahi kutibiwa hospitali hiyo ya Nairobi kwa miaka 20
iliyopita,” alisema Mbowe siku hiyo.
Alute
alisema mpaka sasa bado hawajaanza mipango ya kushughulikia matibabu ya awamu
ya tatu ambayo yalielezwa na Mbowe kuwa yatafanyikiwa nje ya Kenya.
“Nilisema
nitazungumza na waandishi, lakini sijafanya hivyo kwani hakuna taarifa zaidi ya
hizi na utaratibu wa matibabu ya awamu ya tatu bado hayajaanza ndio maana niko
kimya,” alisema.
TIMU ya Dodoma FC ya mkoani hapa, wamejinasibu kuwa
hakuna kitu kitakachoweza kuwazuia kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Dodoma FC imefikia hatua ya kusema hivyo kama kujibu
malalamiko ya wadau wa soka mkoani hapa walioingiwa na mashaka kuhusu kupanda
VPL msimu ujao kwa timu yao kufuatia kufanya vibaya katika mechi zake mbili za
mwisho kabla ya mapumziko ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili.
Dodoma FC ilijikita kileleni mwa kundi C' kwa
kipindi chote cha mechi za Ligi Daraja la Kwanza, kufuatia matokeo mazuri
waliyokuwa wanayopata, lakini mzunguko wa pili umewaanzia vibaya mara baada ya
kufungwa mechi mbili mfululizo ikiwemo ya hivi karibuni dhidi ya pamba huko
Mwanza.
Katibu mkuu wa Dodoma FC Fourtnatus Johnson alisema
kuwa nafasi yao ni namba moja hivyo mapema mechi ya Desemba 16 mara baada ya
dirisha dogo la usajili kufungwa lazima warudi katika nafasi yao kwa kuvuna
pointi tatu.
"ligi daraja la kwanza ni ngumu asikuambie mtu,
lakini Tunashukuru Mungu hatuko katika nafasi mbaya, hivyo niwaambie wadau wetu
wa Dodoma wasiwe na wasiwasi kwani mwakani lazima tucheze ligi kuu hivyo
matokeo yasiwatishe"
Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri ripoti ya kocha wao
Jamhuri Kiwelu "Julio" juu ya wachezaji watakaofanikiwa kubaki na
wanaondoka ili kujua nafasi za kufanya usajili ili kukazia kikosi chao katika
makali ya kuhakikisha wanatimiza ndoto za wana Dodoma kushuhudia Ligi Kuu
"Niwaombe Shirikisho la Soka nchini waache timu
zicheze mpira na matokeo yaamue siyo kuangalia kanda wanazotoka iwe kigezo cha
kupigania timu husika zipate hata kama kiwango chao cha kucheza ni mbovu."
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ifanye utafiti wa kina ili kupata
aina bora ya mbegu za pamba zitakazowanufaisha wakulima.
Amesema ni
lazima utafiti huo ufanyike kwa kuzingatia aina ya udongo unaopatikana katika
kila mkoa unaolima pamba.
Ametoa kauli
hiyo (Jumanne, Novemba 14, 2017) alipozungumza na wabunge wanaotoka
katika mikoa inayolima pamba, Bungeni mjini Dodoma.
“Mbegu za
pamba ziko nyingi na zina migogoro. Mbegu nyingine zina manyoya, nyingine zina
vipara hivyo lazima utafiti wa kina ufanyike ili kupata aina bora.”
Alisema
Wizara ya Kilimo itumie taasisi zake vikiwemo vyuo kufanya uchunguzi na kubaini
ni aina gani za mbegu zinafaa kutumika kulingana na eneo husika.
Alisema
utafiti huo ambao utabainisha aina ya mbegu inayofaa kulingana na aina ya
udongo katika kila eneo ili kumuwezesha mkulima kupata mazao ya kutosha.
Pia aliwataka
Maofisa Kilimo katika mikoa inayolima mazao makuu ya biashara waweke kipaumbele
katika kuyasimia mazao hayo.
Waziri Mkuu
alisema Maofisa hao lazima wahakikishe wanayasimamia vizuri mazao hayo ambayo
ni korosho, chai, pamba, kahawa na tumbaku ili yawe na tija.
Alisema Serikali
imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake
umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.
Waziri Mkuu
alisema Serikali inataka kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa zao la pamba
kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.
“Tunataka
kulifanya zao hilo ambalo lilikuwa likijulikana kama dhahabu nyeupe lifikie
kiwango cha juu cha uzalishaji, hivyo kuongeza tija kwa wakulima.”
Pia Waziri
Mkuu aliwaagiza Maofisa Kilimo katika mikoa hiyo wafanye sensa ili kutambua
idadi ya wakulima wa pamba na ukubwa wa mashamba yao.
Alisema lengo
la sensa hiyo ni kutambua idadi ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili
kurahisisha usambazaji wa pembejeo kulingana na mahitaji.
Wakizungumza
katika mkutano huo baadhi ya wabunge waliiomba Serikali kuhakikisha zao hilo
linaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuwafikishia wakulima pembejeo kwa wakati.
Kwa upande
wake Mbunge wa Itilima Njalu Silanga aliiomba Serikali izibane Halmashauri
ili kuhakikisha fedha za miradi ya kilimo zinatumika ipasavyo.
Silanga
alisema msukumo wa Serikali wa kufufua zao la pamba umeanza kuzaa matunda,
hivyo aliiomba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutafuta masoko ya
kutosha.
Naye Mbunge
wa Tarime Mjini, Ester Matiko ameiomba Serikali kuwaelimisha wananchi na
kuwahamasisha kulima kilimo hicho ili waachane na kilimo cha bangi.
“Serikali
ikitilia mkazo katika usimamizi wa mazao hayo tutasonga mbele na Tanzania ya
viwanda tutaiona. Wakulima waelimishwe kuwa mazao hayo yana tija, hivyo
wataachana na kilimo cha bangi.”
Ester alisema
kati ya mazao makuu matano ya biashara manne yanalimwa katika jimbo lake ambayo
ni chai, pamba, kahawa na tumbaku, hivyo wakulima wakipewa elimu ya kutosha juu
za mazao hayo watapata tija.
MAAFISA kutoka Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Abeid Amani Karume cha Zanzibar (AAKIA), wamefurahishwa na namna ulinzi na
usalama wa abiria na mali zao unavyofanywa kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), imeelezwa.
Maafisa hao kutoka Idara mbalimbali walitoa kauli
hiyo jana katika ziara ya siku moja ya mafunzo JNIA, ambapo walitembelea maeneo
mbalimbali na kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa husika.
Mkuu wa msafara wa maafisa hao, ambaye ni Mkuu wa
Kitengo cha Ulinzi na Usalama cha AAKIA, Shaaban Kombo alisema JNIA inaulinzi
madhubuti kwa abiria na mizigo hukaguliwa kwa kutumia mitambo maalum kabla ya
kupanda ndege au kuingia ndani ya jengo kwa kazi mbalimbali, ambapo wameahidi
kufuata nyayo hizo ili kuzuia uhalifu unaofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu.
Kombo alisema pamoja na kupata mambo mengi ya msingi
ya uendeshaji wa viwanja vya ndege, JNIA imekuwa darasa tosha, ambapo pia
katika upande wa utoaji wa vitambulisho wamejifunza namna utoaji wa
vitambulisho unavyofanyika, ukiwa ni tofauti na AAKIA ambao hutoa vitambulisho
vya kudumu mara baada ya taratibu kukakamilika, wakati JNIA hutoa vitambulisho
vya muda kwa muombaji ili aweze kuendelea na kazi, wakati akisubiri cha kudumu kikamilike
kutengenezwa.
“Tumefaidika na mambo mengi ukiangalia sisi kwetu
hii ya vitambulisho ni tofauti kabisa, ila kwetu kwa kipindi chote mteja
anasubiri kitambulisho cha kudumu anakuwa hawezi kuendelea na kazi zake eneo la
kiwanja hadi atakapopata cha kudumu, lakini hapa anakuwa na cha muda
kinachomfanya aendelee na shughuli zake huku cha kudumu kikiwa katika
matengenezo,” alisema Kombo.
Naye Mkuu wa kitengpo cha Ulinzi na Usalama cha
JNIA, Lugano Mwansasu alisema ziara ya maafisa wa AAKIA imewafariji na kuanza
ukurasa wa mahusiano katika ushirikiano, ambapo nao wamejifunza kulingana na
maelezo ya uendeshaji wa AAKIA.
Lugano alitoa wito kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Tanzania (TAA), kuiga mfano huu wa kupeleka maafisa wake kwenye viwanja
mbalimbali vya nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza utendaji kwa lengo la
kuboresha huduma za viwanja kwa ujumla. TAA inasimamia viwanja 58 vilivyopo
chini ya serikali.
“Kila siku mambo ya uendeshaji yanabadilika, basi
tunaiomba mamlaka yetu itusaidie na sisi kwenda kutembelea viwanja vya wenzetu
tujifunze huko, zipo changamoto labda sisi hatujui zinatatuliwaje lakini kwa
ziara za mafunzo tunaweza kupata mbinu kutoka kwa wenzetu,” alisema Lugano.
Katika hatua nyingine, Meneja Uendeshaji wa JNIA, Vedastus Fabian alisema faida ya ziara ya mafunzo ni kujijengea uwezo na
mahusiano mazuri baina ya kiwanja kimoja na kingine.
Fabian alisema ziara hizo zinasaidia katika
kutatua matatizo yanayovikumba viwanja vya ndege, ambapo kwa sasa kumekuwa na
masuala ya ugaidi, uvushaji wa dawa za kulevia na nyara za serikali.
HUJAFA hujaumbika,
msemo huu wa lugha ya Kiswahili unawiana na hali ya kijana, Joseph Chacha,
aliyezaliwa akiwa mzima mwenye kutembea kwa kutumia miguu yake
miwili, lakini leo hii amejikuta akihitaji msaada wa kutumia baiskeli ya
walemavu kwa ajili kumsaidia katika matembezi yake.
Kijana Chacha
alizaliwa mwaka 1995 Bunda, mkoani Mara, ambapo mwaka 1998 alipata homa ya
kichocho na kumsababishia ulemavu wa kupooza viungo vyote mpaka hivi sasa.
Anasimulia kuwa
umasikini wa kipato unao ikabili familia yake unamchango mkubwa katika ulemavu
alionao, kwani kulikua na uwezekano mkubwa wa kupona nakumaliza tatizo hilo
kama angepata matibabu stahiki.
“Magonjwa mengi
nchi za Afrika yanasabisha kukwamisha ndoto za watu wengi hususan sisi masikini. Tatizo
langu lilikuwa gumu na kuniathiri siku hadi siku kutokana na umasikini,
kama familia yangu ingekuwa na pesa basi ningepata matibabu
yanayostahili,” anasema Chacha.
HARAKATI ZA
MATIBABU
Katika mahojiano
na mwanasafu wa kurasa hii (Tuishivyo), kijana huyo anaeleza baada ya kutokea
kwa tukio hilo wazazi wake walimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Bunda ambako
alipata matibabu, lakini hayakumsaidia, ndipo wakaamua kwenda kwa mganga wa
tiba za asili kwa ajili ya kupata matibabu lakini nako hakupata nafuu
badala yake wakaamua kurudi nyumbani kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya
kuendelea kupata matibabu.
“Nilipelekwa
hospitali nikapata matibabu madaktari wakasema nina homa ya kichocho nikapata
nafuu lakini baadae homa iliendelea ndipo wazazi wangu wakaamua kunipeleka
kwenye tiba za asili homa ikaisha bali viungo vyangu vikaanza kushindwa kufanya
kazi mpaka hivi sasa.”
HARAKATI ZA
MAISHA
Pamoja na hali
yake hiyo ya ulemavu, umasikini wa familia yake, kushindwa kumudu matibabu na
mahitaji ya kila siku ya nyumbani kutokana kuishiwa kabisa pesa ya kupata
mahitaji, alimuomba mama yake ampeleke katika shule za wanafunzi wenye ulemevu
ili ajue kusoma na kuandika kwa ajili ya kuendeleza ndoto zake.
Mwaka 2007
alipelekwa Shule ya Msingi Nyansror iliyopo Bunda ambako alijifunza kusoma na kuandika lakini mwaka 2012 aliacha
kusoma akiwa darasa la tano kutokana na wazazi kushindwa kumudu gharama
za mahitaji ya shule pamoja na kumwongoza kutokana na uzee.
“Sikupenda
kuacha shule kwani nilikuwa na ndoto za kuendelea na shule ndio maana
nilichelewa kuanza lakini nikaona bora nisome ili niweze kufanikisha malengo
yangu, sikukata tamaa kwasababu ya hali yangu ila ilinilazimu kuacha
masomo baada ya mama yangu ambae ndio msaidizi wa maisha yangu kufariki, hapo
ndipo ugumu wa maisha ulipoanza kutokana baba yangu alikuwa mzee pia alikuwa
mlemavu wa mguu mmoja,” anasema.
CHANGA MOTO ZA MAISHA
Kijana Chacha anaeleza
katika maisha yake amepitia changamoto nyingi sana, ikiwamo baada ya kufiwa na
mama yake akanza kuombaomba misaada mbalimbali ikiwamo kanisani ili apate fedha
kwa ajili ya kusukuma maisha yao. Anasema alipoona hali inazidi kuwa ngumu
aliamua kwenda kutafuta maisha jijini Dar es Salam.
Anasema
alifika Dar es Salaam mwaka 2012 na kuanza kuombaomba na kwamba alipata changamoto mbalimbali ikiwamo kukoswa
kugongwa na magari alipo kuwa barabarani, huku akilala na kuomba misaada stendi
ya mabasi ya mikoani ya Ubungo.
Anasimulia kuwa
alipatwa na ugonjwa wa kifua kikuu (TB) hivi karibuni kutokana na kulala nje
kila siku.
WITO
Chacha anatoa
rai kwa wanajamii wote wanaoguswa na changamoto zinazowakabili walemavu kumsaidia
kwa kumchangia fedha ili aweze kupanga
na kuishi katika chumba chake na kupata mahitaji muhimu ya kila siku.
Aidha, anaiomba
serikali na wadau mbalimbali kumuonea huruma na kumnunulia bajaji pamoja na kumpatia
mtaji wa kufanyia biashara ili aweze kufanya biashara na kuendesha maisha yake.
“Nawaombe wadau
mbalimbali na serikali kunisaidia kupata mtaji ili nifanye biashara
nijimudu kimaisha, Watanzania wenzangu mimi sikupenda hii hali naumia
kulala nje kila siku nalazimika kuishi barabarani sina pa kukaa, nakula kwa
kutegemea wasamaria wema ambao wanafanyakazi maeneo hayo, pia namshukuru Mbunge
wa Ubungo, Saidi kubenea, alinipatia baiskeli hii kipindi cha kampeni ingawa
hivi sasa imeisha matairi yamepasuka kama unanyo yaona,” alisema Chacha kwa
huzuni kubwa.
TAHARIRI:
HAKUNA
mashaka kwamba sasa tatizo la mafuriko sio kadhia kwa `watu wa mabondeni’ au wanaoishi karibu na mkondo wa
maji pekee.
Hata
hivyo, nguvu kubwa imekuwa ikiwekwa katika
kuwahamisha watu wanaoishi kwenye maeneo hayo bila kutafuta na kuthibiti
chanzo cha mafuriko hayo.
Mathalani,
katika jiji la Dar es Salaam, tumekuwa
tukishuhudia wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi, Mkwajuni, Jangwani na kwingineko jijini humo wakihamishwa, baadhi nyumba zao
kuvunjwa.
Oktoba
26 mwaka huu, ilinyesha mvua kubwa nchini
na kusababisha madhara makubwa hasa jijini Dar es Salaam, kwa mafuriko ya mvua hizo kuua
watu kadhaa, kuharibu mali zenye thamani
kubwa.
Kila
mtu atakuwa shahidi kupitia vyombo vya habari kuwapo kwa malalamiko ya athari
za mafuriko hayo kila kona ya jiji na
maeneo mengine nchini.
Kama
tulivyosema nguvu kubwa huelekezwa kwenye kuhamisha watu, hakuna juhudi za kukabiliana na chanzo cha mafuriko.
Ni kuokoa au kuhamisha tu.
Sisi
tunaikumbusha serikali wajibu wake wa kuwalinda wananchi wake dhidi ya majanga
kwa kutambua kwamba chanzo cha mafuriko ni ongezeko la maendeleo ya watu
(Human
Development Expansion) tunayoyataka!
Yapo
maendeleo ya ongezeko la nyumba, shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, biashara na viwanda ambazo
watalaamu wanasema vimekuwa chanzo cha ongezeko la mafuriko na kina cha maji ya
bahari.
Kwa
hiyo matatizo kama mmomonyoko wa udongo unaotokana na maji mengi yasiyovunwa
kwenye nyumba, kukosekana kwa vizuia kasi ya maji kama vile miti kutokana na mabadiliko
ya tabia nchi hujitokeza.
Matokeo
yake ni kupanuka kwa makorongo, mito, bahari na maziwa kila uchao na kupatikana kwa mabonde.
Bila
kutambua wajibu wake katika kukabiliana na hali hiyo, serikali hukimbilia
kuwaondoa watu kwa kigezo cha kisheria kwa kuwaita wavamizi wa mita 60 za mito, bahari na maziwa tena wengine sheria ya mazingira ya (EMA) ya
mwaka 2004 iliwakuta.
Sisi
tunaona kwamba kuna kila sababu ya serikali kutafuta chanzo cha mafuriko na kukithibiti.
Hii ni pamoja na kujenga kingo za mito, bahari na maziwa ili kutopanuka na
kufuata makazi ya watu.
Huu
ni wajibu kulingana na mikataba ya kimataifa ambayo serikali yetu ilisaini na
ni haki ya wananchi wa nchi husika.
Tunapokimbilia
kuwahamisha watu wakati mabonde yalitokea kwa kutojengwa kingo, ni wazi kwamba
hata wale ambao leo wako nje mita 60 kesho watakosa uhalali wa kuishi humo
kutokana na mmomonyoko unaoendelea kuwafuata. Tutawahamisha wangapi? mwisho
tutahamisha mtaa mzima!
Pia
tunaishauri serikali kuimarisha miundombinu kwa kujenga au kufufua mitaro
kutokana na ukosefu wa mitaro kusababisha kuzagaa kwa maji na kuwa chanzo kwa watu wengine ambao sio wa mabondeni nao
kuingia katika kadhia hiyo.
Sisi
tunaamini kwamba hayo yakitiliwa mkazo tutapunguza au kumaliza tatizo la mara
kwa mara la mafuriko. Haina maana kwamba waliojenga baada ya sheria waachwe.
Msisitizo wetu ni jamii kutii sheria sambamba na kuthibiti chanzo cha tatizo
kama haki ya jamii.
Kuwahamisha
watu sio suluhisho na kukomesha tatizo. Ni sawa na kugawa vyandarua badala ya
kuua mazalia ya mbu!
KILA
mtu ana ndoto ya kufikia lengo fulani katika maisha yake. Na hapo ndipo hutimia neno
la kitaalamu lisemalo: ‘Maandalizi ya leo ni mafanikio ya kesho’ au maisha ni
mchakato, hatua’.
Kijana Joas Yunus kwa muda mrefu amekuwa na ndoto ya kuwa
mwandishi wa wa vitabu kwa ajili ya kuielimisha jamii kupitia fasihi andishi
iliyoianza tangu akiwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi
Nzovwe iliyoko wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Anasema tangu akiwa darasa
la nne alipenda kufundisha japo hakujua atafundisha kwa njia gani, hivyo aliamua
kujitolea kuwafundisha wanafunzi wenzake walio madarasa ya chini yake, baadaye kuanzisha kituo cha mafunzo kwa watoto wadogo ambacho
aliendelea nacho hata baada ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2003.
Alisema ili kutopoteza ndoto yake, aliendelea
kujitolea kuwafundisha hata baada ya kuendelea na masomo ya sekondali ingawa
alipatwa na changamoto nyingi kwa kuwa haikuwa rahisi kuwafundisha aliokuwa
anasoma nao darasa moja na wakamkubali wote.
Hata hivyo, pamoja na changamoto
alizopata hakukata tama na alipohitimu sekondari aliendelea kufundisha masomo
ya jioni katika kituo alichokianzisha nyumbani kwao kabla ya kupata nafasi ya
kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Pugu mwaka 2008.
Baadaye alipogundua kwamba kufundisha kuna tija kwa jamii, akaamua
kuwashirikisha baadhi ya wenzake ili kuandika vitabu.
Aligundua kwamba ili vitabu viwe bora, kusomwa zaidi na kuongeza soko
anatakiwa atafute watu wenye uwezo wa kusanifu hasa upande wa marafiki zake.
Ubunifu wake huo ulimsaidia kuongeza kipato na kufanikiwa kupata
mtaji wa kuzalisha matoleo mengine zaidi huku akiendelea na masomo yake pamoja
na kuendeleza kituo chake alichokuwa amekianzisha mkoani Songwe hadi alipoanza elimu
ya juu.
Anasema aliendelea na kituo chake hicho na kufanikiwa kugawa mtaji kwa kuanzisha kituo
kingine cha elimu kwa
vijana na watu wazima pasipo gharama zozote kwa nia ya kuisaidia jamii yake.
Baada ya kurudi kijijini kwao alifanya
ibada zake katika kanisa la FPCT na kuchaguliwa kuwa katibu wa vijana kanisani
baada ya kumpenda kutokana na uandaaji, uandishi na mpangilio mzuri wa taarifa
za vikao vya kanisa.
Kazi yake ya kuisaidia jamii ikamfanya apate umaarufu zaidi na kuchaguliwa
kuwa katibu wa vijana katika kanisa la FPCT alilokuwa akifanya ibada.
Yunus alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2010 na
kupata Shahada ya Sayansi ya Kompyuta na
baadae elimu mbalimbali ya ujasiriamali.
“Pia nilifanikiwa kusoma shahada ya elimu sayansi ya kompyuta na
baadaye ujasiriamali. Niliweza kusoma na kufanya kazi zangu
kuhakikisha tu kwamba vitabu vipo katika usahihi,” alisema.
Anasema akiwa katibu alipata wazo jingine
katika kutoa huduma kwa vijana wengine nje ya kanisa hivyo akamua kusajili kitabu
chake alichokiita ‘Kijana jitambue’
kilichokuwa na maudhui ya kutoa elimu mbalimbali kwa rika ili waweze
kujitathmini na kujitambua hasa katika kuziona fursa mbalimbali na
kuzichangamkia.
Mwaka 2015 aliandika kitabu kingine
alicho kiita ‘Inuka’ kwa maana ya inuka katika dimbwi la umasikini na kujifunza
ufundi wa magari mtaani.
Anasema alikuwa hana uhakika wa kupata
kazi, jambo lililomsukuma kubuni njia ya kupata kazi. Anasema aliamua kupanga
makopo matupu ya oili pembeni mwa barabara ya zamani ya Bagamoyo ili kuwavuta
watu walioharibikiwa na magari.
“Ndipo
siku moja, raia mmoja wa kigeni akaona yake makopo na kushuka kutoka ndani ya
gari. Kisha nilimsogelea na kugundua kuwa gari yake ilikuwa na hitilafu iliyosababisha
isiwake, niliitengeza na kulipwa pesa ambayo kwangu ilikuwa mtaji,”anasema.
Anasema changamoto zilizopo katika kazi
yake ya uandishi ni pamoja na kutokuwa na watu wanaoweza kumuwezesha pamoja na
kukosa vitendea kazi kama vile kompyuta
Yunus kwa sasa meamua kujiajiri kupitia
fani yake ya uandishi wa vitabu na kuwashauri waandishi wengine kuandika kwa
ajili ya jamii na Tanzania ya viwanda iweze kuendelea mbele pamoja na kuanzisha
vituo vingi vya kutoa mafunzo kwa vijana
katika kila wilaya.
JAMII imeshauriwa kujiunga kwenye vikundi ili
kuunganishwa kwenye mfumo wa teknolojia ya usafishaji wa maji taka kwa ajili ya matumizi mengine ili
mfumo huo uwasaidie kutumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali zenye tija badala
ya kuyateketeza baada ya matumizi.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya maji taka
(OSWAMS), Juma Mohamed Nasoro katika ziara ya maofisa mbalimbali wa
serikali walipokuwa wakitembelea mradi
huo unaotekelezwa katika nyumba za maofisa wa jeshi la polisi, mikocheni jijini Dar es Salaam.
Alisema tekonolojia ya usafishaji wa maji taka ni
muhimu wakati huu taifa likihitaji watu wake kuwajibika ipasavyo kwa kuanzisha
miradi ya uzalishaji mali kufikia uchumi
wa kati kwa njia ya viwanda.
Kwa bahati mbaya, sehemu kubwa ya watu hawajatambua
fursa zilizopo katika matumizi ya teknolojia hiyo na kusababisha maji taka yanayozalishwa
kuteketezwa wakati yangetumika kwa ajili
ya shughuli za kilimo, ufugaji wa samaki, ujenzi na bustani.
“Maji machafu ni fursa sio tatizo. Kwa hali ilivyo
sasa kila hitaji la maji lazima yatumike maji ya Dawasco. Tunataka maji taka
yasafishwe na yatumike kwa shughuli za kuongeza kipato sio kutegemea maji ya
Ruvu chini na Juu. Ili kufikia malengo haya ni lazima elimu ipelekwe kwa
wananchi ya umuhimu wa teknolojia hizi ambayo pia huzuia magonjwa hasa ya
mlipuko,”alisema.
Akifafanua kuhusu mfumo huo wa kutibu maji taka,
Nasoro alisema kabla ya maji hayo kutumika hupitia hatua kadhaa kuanzia
utengenezaji wa chemba ambayo ni ya kwanza ya matibabu ya maji hayo.
Kisha maji taka hupitishwa kwenye mfumo wa pili wa tiba unaojulikana kitaalamu kama
anaerobic (ABR) na U-Flow Anaerobic (UAF ) ambapo wadudu hula takataka kabla ya
kufikia kiwango cha juu cha udhibiti, alisema.
“Maji yanayotibiwa kwa njia hizo yanakuwa yametibika
kwa asilimia 85 na kiasi kingine huenda aridhini. Kwa hali hii sio rahisi
kusababisha magonjwa, ni salama kwa matumizi kwani yamesafishwa kitaalamu.
Yanafaa sana kwa kilimo na ufugaji kwani yana mbolea, nitrogen na
phosphorus,”alisema.
Alisema kampuni yake imefanikisha teknolojia hiyo
katika taasisi za umma na shule binafsi ya Libermann ya pia ya jijini Dar es
Salaam.
Baadhi ya maofisa waliotembelea mradi huo kutoka
wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia Wazee na Watoto, Jiji la Dar es
Salaam na Manispaa za Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo waliridhishwa na
utekelezwaji wa mpango huo na kusema hatua inayotakiwa ni jamii kuhamasishwa
kujiunga baada ya kuutathimini na kuingizwa kwenye mipango ya ya serikali.
Afisa afya wa Manispaa ya Ubungo Wilson Msangi
alisema teknolojia hiyo ni hupunguza gharama ya ukusanyaji wa maji taka,
huchukua nafasi ndogo na kushauri Halmashauri kuihamasisha kwenye maeneo kama
shule na hospitali kutokana na maeneo hayo kuzalisha kiasi kingi cha maji taka.













