Habari Mpya

Habari Zote

Archive for August 2017


Matukio na Mabari

Serikali imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo katika kikao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Eng. Angelina Madete.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.

“Mfuko huu unaendelea kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo Takwimu zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano   yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939  kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”, amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu miradi ya maendeleo ya mawasiliano vijijini katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma.

Ameongeza kuwa tayari Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine 75 na vijiji 154.

Pia, ametanabaisha kuwa hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Moshi Kasoso, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kilichowakutanisha na uongozi wa Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso, amezitaka kampuni za simu za mkononi zinazopeleka mawasiliano vijijini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ambazo zinapatiwa ruzuku na Serikali kuhakikisha kuwa zinatoa taarifa sahihi kwa Mfuko huo ikiwemo hatua zilizofikiwa za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji husika.

 Amewataka UCSAF kujitangaza na kuweka mabango yao kwenye minara yote nchini iliyojengwa kupitia ruzuku ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kutambua uwajibikaji wa Serikali katika kufikisha mawasiliano kwa wananchi wake.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Dua Nkurua, akitoa maoni  kuhusu ufikishaji wa mawasiliano vijijini kwa viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (hawapo pichani) katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kushoto kwake ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Bhagwanji Meisuria na kulia ni Katibu wa Kamati hiyo Bw. Richard Masuke.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete, amesema kuwa Wizara kupitia UCSAF itahakikisha kuwa kila mwananchi anafikiwa na mawasiliano kuendana na jukumu la msingi la Mfuko huo la kufikisha mawasiliano kwa wote.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu maeneo ya vijijini yaliyofikiwa na mawasiliano katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kulia ni Mhe. Dua Nkurua na kushoto ni Mhe. Rita Kabati wajumbe wa Kamati hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Eng. Peter Ulanga, amewahakakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuwa Taasisi yake itashirikiana na wataalam kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuhakiki kazi zilizofanywa na kampuni za simu za mkononi za ujenzi na usimikaji wa minara na uwepo wa mawasiliano kwenye vijiji mbalimbali nchini.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es salaam leo Agosti 29, 2017. Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi. (PICHA: Na Ikulu)

Mtendaji Mkuu Wa Mahakama Ya Tanzania, Hussein Kattanga Akizungumza Jambo Na Mtaalam Kutoka Benki Ya Dunia, Waleed Malik Walipotembelea Ujenzi Wa Kituo Cha Mafunzo Cha Mahakama Kinachojengwa Kwa Ushirikiano Kati Ya Mahakama Na Benki Ya Dunia. Kituo Hicho Kinajengwa Katika Mahakama Ya Kisutu Jijini Dar Es Salaam.  
Mahakama ya Tanzania inakusudia kuanzisha kituo cha Mafunzo kwa ajili ya watumishi wake pamoja na wadau ili kuwaongezea ujuzi utakaosaidia kuboresha huduma zinazotolewa na Mahakama.


Kituo hicho kinachojengwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam kitawaunganisha watumishi wa Mahakama na wadau katika mafunzo kwa njia ya video (video conferencing).

Akizungumzia Kituo hicho, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya Maboresho ya huduma za Mahakama ambacho pia wadau wa Mahakama watakuwa ni sehemu ya mafunzo yatakayokuwa yakitolewa.

Alisema badala ya Majaji, Mahakimu, watumishi na wadau wa Mahakama kwenda kupata baadhi ya mafunzo kwenye chuo cha Uongozi wa Mahakama- Lushoto (IJA), baadhi ya mafunzo watakuwa wakiyapata katika kituo hicho.

Naye Mratibu wa Mpango Mkakati wa Mahakama pamoja na maboresho ya Huduma za Mahakama Mhe. Zahara Maruma alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa nguzo ya tatu ya mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambapo kupitia nguzo ya pili ya Mpango huo, Majaji na Mahakimu hupatiwa mafunzo mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Akizungumzia nguzo ya tatu ya Mpango huo, Mhe. Maruma alisema nguzo hiyo inahusiana na urejeshaji wa imani ya wananchi kwa Mahakama na ushirikishwaji wa wadau katika shughuli za Mahakama ambapo kupitia kituo hicho wadau wa Mahakama watahusishwa kwenye Mafunzo mbalimbali ili kurahisisha suala la upatikanaji wa Haki.

Kuhusu suala la matumizi ya Teknolojia ndani ya Mahakama, Mratibu huyo alisema hivi sasa Mahakama inao mpango wa kujenga vituo vya aina hiyo kwenye maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuunganisha Mahakama zote nchini kwa njia ya video (video conferencing).


Ujenzi wa kituo cha Mafunzo cha Mahakama ulioanza hivi karibuni kwa ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 78. Aidha, Jengo la kituo hicho cha mafunzo linajengwa kwa kutumia teknolojia ya gharama nafuu iitwayo Moladi na linatarajiwa kukamilika ndani ya wiki nane. 

WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.
Mji wa Cuba

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumapili, Agosti 20, 2017) wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.

Majaliwa ambaye yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa Taifa ni jambo muhimu kwa sababu ya kukosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.

Kutokana na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo na washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini zinaendelezwa.

Alisema Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka chini kwenda wa katikupitia ushirikiano.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuzingatia sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara wamalizapo masomo yao.

Alisema Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo yao.

 “Nawaomba msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe wengine.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha wanatangaza vivutio vya utalii.

Alisema Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema Mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Miongoni mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina tofauti tofauti.

Awali Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Goodchance Tarimo alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao nchini humo.

Alisema wao wana imani kubwa na Serikali na wanaunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo pamoja na kukuza uchumi.


“Tunapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika  kujenga uchumi wa viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya kisasa”
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ameiomba Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kukopesha wakulima wa mazao ya ufuta na mihogo ili waweze kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara hasa kwa wakulima wadogo wadogo wa mkoani humo.
Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi

Zambi alitoa wito huo wakati wa mkutano wa Wadau wa Korosho na Ufuta Mkoa wa Lindi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Zambi alisema kuwa mkoa wa Lindi ni mkoa uliojaaliwa katika kuzalisha mazao ya ufuta na mihogo lakini changamoto kubwa ni mtaji wa kulima kibiashara ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

“Wakulima wa mkoa wa Lindi wapo tayari kushiriki katika kuleta mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara lakini kwa sasa suala la mtaji wa kilimo cha kibiashara ni changamoto kubwa,” alisema Zambi.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Lindi alisema kuwa ili kuwezesha wakulima hao kulima kibiashara Benki ya Kilimo ina wajibu wa kutoa mikopo yenye riba nafuu ili kuhamasisha wakulima hao wa mkoa wa Lindi waweze kuongeza uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini mkoani humo.

Aliongeza kuwa kama TADB itaboresha upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko kutawezesha wakulima wa Tanzania kufikia uchumi wa kati kama ilivyolengwa na Serikali ifikapo mwaka 2015.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Francis Assenga alisema kuwa Benki ya kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa wakulima wadogo wadogo waliokuwa kwenye vikundi ili waweze kukopeshwa.

Assenga aliongeza kuwa Benki ya Kilimo pia ipo tayari kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ya Kilimo kwa kuipatia mikopo yenye riba nafuu zilizo chini ya viwango vya kibiashara kwenye soko.

“Kwa kutambua umuhimu wa wakulima wadogo wadogo nchini TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa Benki yake inaandaa mfumo mahususi wa uratibu kwa kushirikiana na halmashauri za mikoa ili kuhakikisha kuna upatikanaji wa fedha kwa ajili ya minyororo ya ongezeko la thamani kwa mazao ya Kilimo nchini.

“Tupo tayari kusaidia uzalishaji kwenye hatua mbali mbali za uongezaji wa thamani, hadi masoko ya bidhaa za mwisho  hadi kumfikia mlaji na kusaidia kuwaunganisha wakulima na masoko kupitia halmashauri zao,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa TADB, Augustino Chacha alisema kuwa TADB inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma zisizo za kifedha kwa wakulima kama vile kujengewa uwezo juu ya uandaaji wa andiko la miradi ya Kilimo, pamoja na upatikanaji wa taarifa za masoko, usimamizi wa biashara, mafunzo juu ya miradi ya Kilimo na mbinu za majadiliano ya mikataba.

 “Tupo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo,” alisema.

Chacha aliongeza kuwa kwa upande wa mikoa ya kusini Benki ya Kilimo imejipanga kueendeleza miundombinu ya umwagiliaji na maghala pamoja na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo na kuimarisha viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta, mihogo.
Chacha aliongeza kuwa Benki imejipanga kuwezesha uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya mihogo, korosho na ufuta mkoani Lindi.


KUTOKANA na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kuendelea kutokea katika jamii yetu, katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mashirika na asasi mbalimbali, zikiwemo za serikali na binafsi zimekuwa zikiendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuachana na vitendo hivyo unavyovota ni vikinyama
 
 Mwanamke mmoja akitoka shambani kulima huku akiwa amebeba mzigo mkubwa wa kuni, mtoto mgongoni na mwingine akiwa amemshikilia mkono. mume wake amemwachia kufanya kazi zote. Huo ni ukatili wa kijinsia
Mbali na kutoa elimu hiyo pia asasi na mashirika hayo yamekuwa yakitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanajamii madhara ya ukatili huo, ikiwa ni pamoja na adhabu inayotolewa kwa mtu au kikundi chochote kilichofanya ukatili wa kijinsi dhidhi ya mtu au watu furani.

Lakini pamoja na kutolewa kwa elimu ndani ya jamii yetu baadhi ya watu wamekuwa na vichwa vigumu kuachana na vitendo hivyo na badala yake kila kukicha wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wananchi wenzao, wasiostahili adhabu hiyo.

Mara kwa mara vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikisikika kutokea kwa wanawake, pamoja na watoto. Lakini pia kwa siku za hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu tunaambiwa baadhi ya wanawake nao wameonekana kuwa wanyama kwa kufanyia ukatili wa kijinsia waume zao.

Baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwafanyia ukatili wa kijinsia wake zao, kwa sababu ya mfumo dume, kwa kuwapa kipigo kikali, ukatili wa kingono na ukatili wa kila aina kwa kutumia mfumo huo dume.

Aidha, watoto nao wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, vikiwemo vya kupigwa pindi wanapopatikana na makosa ambayo hata adhabu yake ilitakiwa kuonywa tu, kwa mfano mtoto anapokomba mboga chunguni ama kwa kusikia njaa ama vinginevyo, ama anapopoteza fedha alizopewa kwa ajili ya kununua kitu furani dukani, utakuta mzazi au mlezi anampatia adhabu kali ambayo haiendani kabisa na umri wake.

Wazazi au walezi wengine wamekuwa wakiwapatia adhabu ya kuwafunga na kamba mikono watoto wao na kisha kuwachoma na kuwasababishia majeraha mwilini.

Hali hiyo ya ukatili ndiyo inayoweza kumshinda mtoto husika na kuamua kukimbilia mitaani, na kuzalisha mtoto wa mitaani ambaye kwa namna nyingine maisha yanavyozidi kuwa magumu kwake hataimaye uamua kujiingiza kwenye makundi ya kiuharifu na kasha kuiishia jela au kuuawa na wananchi wanaojichukulia sheria mikononi pindi wanapomtuhumu kutenda kosa lolote la kiuharifu.

Lakini pia wazazi ama walezi wengine wamekuwa wakifanya ukatili kwa watoto, ambao ni wakuwanyima haki yao ya msingi ya kuwapatia elimu, ambayo ingemsaidia katika maisha yake ya baadaye.

Ama wazazi na walezi wengine wamekuwa wakiwatumikisha watoto wao ambao umri wao hasa unafaa kuwa shule kwa kazi ambazo haziendani na umri wao, kwani baadhi yao uwatumikisha katika kazi za mashambani, uwatumikisha katika kazi za uvuvi, uchungaji wa mifugo, kazi za migodini na kazi nyingine hatarishi kwa maisha yao.

Kwa mfano mimi hainiingii akilini kumtumikisha mtoto mwenye umri wa miaka saba katika kazi ya uvuvi, kwani ajali ya kuzama mtumbwi ikitokea, kamwe mtoto huyo hawezi kujiokoa kwa sababu hajui hata kuogelea kulingana na umri wake kuwa mdogo. Kwa jinsi hiyo hicho ni kitendo cha kumtoa kama sadaka mtoto mwenye umri huo.

Pia baadhi ya wanaume wanawafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia wake zao, kwani utakuta mwanaume kazi yake ni kukaa vijiweni tu muda wote akipiga soga, kuanzia asubuhi hadi jioni. Na kazi ya shambani au ya uzalishaji mali anamwachia mwanamke na watoto wake pekee.

Baadhi ya wanaume hao wamekuwa  ama wakikalia kulewa pombe tu na muda wa chakula unapowadia urejea nyumbani na kudai chakula tena kwa sauti kubwa, ilihali hajui chakula hicho kimedhalishwa kutoka wapi na hata hiyo mboga anayoitumia kulia hajui imenunuliwa na nani? Lakini bila soni mwaume mtu mzima ujikalisha kwenye meza na kuanza kubugia chakula hicho kana kwamba kakizalisha yeye.

Na kibaya zaidi anapokuta mwanamke hajaandaa chakula, ugeuka kuwa mbogo na kuanza kumtolea matusi na kejeri na hata kumshushia kipigo kikali kama kwamba ni mbwa mwizi.

Wakizungumza kwa nyakati na maeneo tofauti na mwandishi wa makala hii, baadhi ya wanawake wilayani Bunda, Mara, walisikika wakisema kuwa hata wakati wa mavuno, licha ya waume zao kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo hicho, waume zao wamekuwa wakinyang’anywa fedha zote walizouza mazao yao na kupewa kamgao kidogo tu, nyingi zikichukuliwa na waume zao na kwenda kufanyia mambo ya starehe ukiwemo unywaji wa pombe na vimwana vingine vya pembeni maarufu nyumba ndogo.

Mashirika pamoja na asasi mbalimbali za hapa nchini na hata nje ya nchi zimekuwa zikijitahidi  sana kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa ndani ya jamii yetu, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaoendesha vitendo hivyo.

Nao baadhi ya kina mama wamekuwa wakiwafanyia unyama usiovumiliwa watoto wao, tena wengine wakisikika wakisema si ni mwanganu hata kama ni kimuua. Labda hapa niwakumbushe akinamama wa aina hiyo kwamba mtoto ukisha mzaa ni wa serikali, iwapo ukimfanyia ukatili wa aina yoyote sheria itachukuliwa dhidi yako bila kujali kwamba wewe ndiye uliyemzaa.

Kutokana na elimu inayotolewa na mashirika, pamoja na asasi hizo, hivi karibuni serikali wilayani Bunda mkoani Mara, ililipongeza shirika lisilokuwa la kiserikali la Zinduka lililoko wilayani humo, linalofadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society, kwa kuwapatia wananchi elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia ili vitendo hivyo viweze kukomeshwa ndani ya jamii.

Pongezi hizo zilitolewa na mkuu wa wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili, aliyewakilishwa na katibu tarafa cha Nansimo, Jonas Nyaoja, kwenye mafunzo ya kupinga vitendo hivyo.

Mafunzo hayo ambayo yalikuwa ni mwendelezo wa mafunzo mengine ambayo yamekwishafanyika, yalifanyika katika ukumbi wa kituo cha walimu katika mji mdogo wa Kibara, uliko katika makao makuu ya jimbo la Mwiabara.

Mkuu huyo wa wilaya ya Bunda alisema kuwa serikali wilayani hapa inatambua mchango mkubwa wa shirika hilo katika kutoa elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ili jamii iweze kupata uelewa na kuachana na vitendo hivyo.

 “Serikali wilayani Bunda inatambua mchango mkubwa unaaotolewa na shirika hili la Zinduka katika kutoa elimu kwa jamii juu ya ukiukwaji haki na unyanyasaji wa kijinsia. Sasa elimu hii wananchi wetu wakiipata itawasaidia kubadilika na kuacha vitendo hivyo” alisema Nyaoja kwa niaba ya DC Bupilipili.

Aidha, baadhi ya wadau mbalimbali wanaopinga vitendo hivyo wilayani hapa, pia wamelishukuru shirika hilo kwa kuwapatia mafunzo hayo kwa sababu vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekithiri sana ndani ya jamii yetu, ukiwemo ukatili wa kiuchumi pamoja na ule wa tendo la ndoa.

Wadau hao ambao ni pamoja na wazee wa mila, wazee maarufu, viongozi wa madhehebu ya dini, vyama vya siasa, watendaji wa vijiji na kata, pamoja na wenyeviti wa vijiji, walisema kuwa Shirika la Zinduka limejikita sanan katika kutoa elimu hiyo kwa jamii.

Waliyaomba mashairika mengine kuiga mfano huo, kwani wananchi wengi wamekuwa wakiendesha vitendo hivyo kwa sababu ya kukosa uelewa na kwamba ni shirika la kwanza kufika mkatika maeneo yao na kuwapatia elimu hiyo.

Walisema kuwa ukatili mwingine ni ubakaji wa wanawake, utumikishaji wa watoto wadogo kwenye shughuli hatarishi ambazo haziendani na umri wao, ukatili wa kutokupeleka watoto shule hususani wa kike, pamoja na unyanyasaji wanawake na wanaume ndani na hata nje ya ndoa.

Waliongeza kuwa ukatili mwingine ufanywa na wanaume kuachia shughuli za kilimo na uzalishaji mali wanawake tu, huku wanaume wengi wakikalia ulevi na uzululaji, ambapo nyakati za chakula ufika majumbani mwao na kudai chakula tena kwa kuamrisha, ambapo wanawake wanaposema hakuna chakula uambulia kichapo au matusi ya uzalilishaji.

Walisema kuwa wamridhika na mafunzo hayo ambayo yamewapatia mwanga, ambapo wataisambaza elimu hiyo katika maeneo yao ili jamii iweze kubadilika.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa shirika la Zinduka, mhasibu wa shirika hilo, Godfrey Anatory, alisema kuwa wanatoa mafunzo hayo kwa makundi mbalimbali ya kijamii katika kata tisa za jimbo la Mwibara na kwamba katika awamu ya kwanza walitoa mafunzo hayo katika kata 13 za majimbo ya Bunda na Bunda mjini.

“Mafunzo haya tunayaendesha kwa kata tisa za jimbo la Mwibara, lakini pia mafunzo kama haya tulikwishayaendesha katika kata 13 za majimbo ya Bunda na Bunda mjini. Na baadaye tuendesha mafunzo haya kwa viongozi mbalimbali wakiwemo maasikari polisi, mahakimu na wanasheria, ili jamii iweze kujua athari za ukatili wa kijinsia na adhabu yake” alisema.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Dk. Stanely Maendeka, alisema kuwa malengo ya mafunzo hayo ni kupata uelewa sahihi wa dhana za kijinsia na dhana ya ukatili wa kijinsia, na kupata uelewa na uwezo wa kutetea na kukomesha ukatili wa kijinsia ndani ya jamii.

Dk. Mahendeka aliyataja maelengo mengine kuwa ni pamoja kurekebisha mapendekezo ya awali ya mradi, ili ibebe shughuli zinazogusa kukomesha ukatili wa kijinsia, kurekebisha bajeti iweze kuingiza au kuchukuwa shughuli zilizopendekezwa, kukomesha ukatili wa kijinsia na kuweza kutekeleza mradi vizuri zaidi na kupata matokeo yaliyotarajiwa.

Mkurugenzi wa shirika la Zinduka Maximillian Madoro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekuwa wakitoa mafunzo na elimu mara kwa mara kwa jamii, ili kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsi katika wilaya ya Bunda, mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla vitokomezwa.

Madoro amesema kuwa kupitia elimu hiyo kwa kiasi furani jamii imekwisha badilika na kuachana na vitendo hivyo ingawa bado kuna changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika baadhi ya wanajamii na kwamba pamoja na changamoto hizo wanaendelea kutoa elimu hiyo ili kufikia malengo yao ambayo kikubwa ni kutokomeza vitendo hivyo.

Kwa kumalizia makala yangu napenda kuwakumbusha wananchi wote kwamba tushirikiane na serikali pamoja na mashirika kama haya ya Zinduka, kupinga vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia, kwani pia vinavunja haki za msingi za binadamu.

Wote kwa pamoja tukipiga kelele  na kukemea vitendo hivi, ikiwa ni pamoja na kuwafichua ama kuwataja bayana wale wote wanaoendesha vitendo hivi, vikiwemo na vile vya kukata watu wenye ualbino viungo vyao na kukata mapanga na kuwaua wazee wenye macho mekundu eti kwa imani ya ushirikina, hakika vita hii tutaishinda. Na kuwa na jamii iliyostarabika.

Pia tutowe ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, pindi tunaposhuhudia matukio kama hayo ndani ya jamii yetu, basi tuwe mstari wa mbele kutoa ushahidi mahakamani ili mhusika au wahusika waweze kuchukuliwa hatua na kuhukumiwa adhabu anayostahili kulingana kosa lake alilotenda kwa mjibu wa sheria za nchi yetu.


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imewaasa wakulima wa korosho nchini kuongeza uzalishaji wa korosho ili kuchangamkia fursa za masoko ya zao hilo linalohitajika zaidi katika masoko ya Marekani, Vietnam na India.
 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Francis Assenga 
Wito huo umetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga wakati akifungua Warsha ya Siku ya Wadau wa Vyama vya Ushirika inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara.

Assenga alisema kuwa mahitaji ya korosho ni makubwa sana katika soko la dunia hivyo wakulima wa zao hilo hawana budi kujizatiti ili kuhakikisha wanazalisha kiasi kikubwa cha korosho ili kufikia au kuzidi malengo ya mavuno kwa msimu ujao ambayo yanakadiriwa kufikia kati ya tani laki tatu (3) hadi laki nne (4) ukilinganisha na takribani tani laki mbili na nusu kwa msimu uliopita.

Assenga alisema kuwa korosho ni zao la kimkakati ambalo likiwekezwa kwa usahihi linaweza kunyanyua uchumi na kipato kwa wakulima wa mikoa ya kusini na pwani ambao niyo ni wazalishaji wakuu wa zao hilo.

“Nawaasa mujitahidi kulima kisasa ili kuweza kufikia au kuvuka malengo ya mavuno ya msimu huu hali itakayowaongezea kipato hivyo kufikia malengo ya serikali ya kuwanyanyua wakulima nchini,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi huyo wa TADB aliongeza kuwa Benki yake imejipanga kusaidia mfumo wa Stakabadhi ya maghala ili kuhakikisha kuwa malengo ya mavuno ya korosho kwa msimu huu yanafikiwa.

“TADB iko tayari kuratibu mfumo wa malipo ya fedha zitokanazo na mauzo ya korosho kwa njia ya TEHAMA, pia kwa kushiriakiana na soko la mazao (TMX), kusimamia ununuzi wa mazao kwa njia ya mtandao (electronic auction),” aliongeza

Aliongeza kuwa Benki ipo tayari kusimamia uuzaji wa mazao kwa mifumo ya salama ya kimataifa ya malipo kama vile dhamana ya malipo.
Naye Mkurugenzi wa Biashara wa Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha alisema kuwa Benki ya Kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji na maghala na uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya korosho na mihogo.

Aliongeza kuwa TADB pia ipo tayari kuviwezesha  viwanda vya kubangua mazao ya korosho, na kusindika ufuta, mihogo pamoja na uanzishaji wa mashamba mapya na ya kisasa ya korosho na ufuta.

“Tupo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kuwanyanyua wakulima kama ilivyolengwa na Serikali kupitia mikopo ya pembejeo kuongeza tija kwenye uzalishaji, miundo mbinu ya umwagiliaji na ununuzi wa zana za kilimo (kama matrekta, pump),” alisema.

Chacha aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazao ya kilimo, Benki ya Kilimo ipo tayari kutoa mikopo kwa ajili ya kujenga maghala mapya au kuboresha yaliyopo pamoja na kununua mizani ya kisasa na ununuzi wa magari ya usafirishaji mazao.

Akizungumzia nafasi ya taasisi za kifedha katika kudhibiti upotevu wa mapato kwa wakulima, Mkuu wa Kilimo na Fedha Vijijini wa Mfuko wa Kukuza Sekta ya Fedha (FSDT), Bw. Mwombeki Baregu alisema taasisi na mitandao ya simu nchini zina wajibu wa kubuni teknolojia rafiki wa wakulima itakayosaidia kudhibiti utapeli na wizi wa fedha za wakulima.

Baregu alisema teknolojia duni na ukosefu wa elimu sahihi juu ya matumizi na uhifadhi wa fedha umepelekea wakulima wengi nchini kupoteza mapato yao kwa kushindwa kufahamu uwekezaji sahihi wa fedha hizo.


“Naziomba taasisi za kifedha na mitandao ya simu za mkononi kuwasaidia wakulima katika kuhifadhi fedha zao ili kujiwekea akiba itakayowasaidia wakati wa maandalizi ya kilimo kwa msimu ujao na shughuli nyingine za kimaendeleo,” alisema.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wametakiwa kuongeza jitahada za kuwasajili wanachama wengi wa mfuko huo ili vituo vya serikali viweze kutoa huduma kwa wananchi wengi

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Afya,maendeleo ya jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ummy mwalimu wakati alipotembelea kituo cha afya cha Mazwi kilichopo katika Manispaa ya Wilaya ya Sumbawanga mwishoni.

Alisema Mkoa wa Rukwa umefikia asilimia 27 ya wananchi wanaotumia bima ya afya Kitaifa,hivyo waongeze kuwashawishi wananchi wengi zaidi kujiunga na mfuko huo pamoja na mfuko wa afya ya jamii(CHF)

“nimesema kuanzia sasa ninaanza kuwapima kwa kusajili wananchi ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa ajira,ninataka vijana wengi wajiunge kwa wingi kwa kwa kujiunga kama kikundi na kujiunga na bima inayojulikana kama  ‘Kikoa” kwa kujiunga kikundi cha kuanzia watu kumi,wafikieni huko huko walipo

Kwa upande wa Mfuko wa Afya ya jamii(CHF) waziri huyo hivi sasa kuna CHF iliyoboreshwa hivyo kadi hiyo inatumika kwenye vituo vyote vya halmashauri  na si pale mwanachama alipokatia,”ni bora tuwachangishe elfu kumi kumi za watanzania ili tuweze kufikia usajili wananchi wengi na kupata huduma za afya bila vikwazo

Hata hivyo alishauri Manispaa hiyo kutengezea kadi ambayo itakua rafiki kwa mwanachama kuweza kuiweka kwenye waleti au mahali pengine ambayo itakua rahisi kwa kutunza na siyo kadi za hivi sasa ambayo ni mzigo kwa mwanachama kuibeba kwani kadi hiyo ni kubwa

Pia, alisema wizara yake inataka kuongeza gharama ya CHF iliyoboreshwa ya  shilingi elfu ishirini ambapo mwenye kadi hiyo ataenda kupata huduma hivyo hadi  hospitali ya mkoa,

“ tunazungumzia kila mtu apate huduma za tiba bila kikwazo,leo una hela,kesho huna na una umwa bora tunasema utoe elfu kumi na utibiwe ndani nya manispaa tena siyo peke yako bali na watu wako watano,alisema waziri ummy.


Hata hivyo alisema ni  marufuku  kwa mtu mwenye kadi ya CHF anapoenda kwenye vituo vya huduma ya afya kuambiwa akanunue kipimo au dawa bali wanatakiwa kupata vipimo vyote.

- Copyright © Mito Ya Baraka Morogoro - Mito Ya Baraka Morogoro - Powered by Blogger - Designed by Peter Mwamkamba -